Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania,Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, ameweka wazi kuwa, licha ya kuwa na kibarua mbele ya Burundi lakini akili na mawazo yake ni juu ya mchezo wao dhidi ya Tunisia.
Stars itakuwa na kibarua ugenini cha kukabiliana na Tunisia, mchezo utakaochezwa Novemba 13 mwaka huu kabla ya marudiano kufanyika Novemba 17 jijini Dar es Salaam.
Michezo hiyo ni kwa ajili ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika, lakini kabla ya kuumana na Tunisia, Stars itashuka dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam, Jumapili hii kuumana na Burundi.
Akizungumza na MTANZANIA,Ndayiragije , alisema mechi dhidi ya Burundi ni ya kirafiki ambayo haina umuhimu mkubwa katika suala la matokeo kama ilivyo ile na Tunisia.
“Mechi na Burundi kwangu ni kipimo cha kuangalia nina wachezaji wa aina gani wa kwenda nao nchini Tunisia, ambako ndiko kuna mechi ngumu na muhimu kwa nchi.
“Hata nilipowaomba TFF(Shirikisho la Soka Tanzania)wanitafutie mchezo mmoja wa kirafiki kulingana na kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa(Fifa) linavyotaka sikutaka watumie nguvu kubwa kuzishawishi timu bali niliwaambia nchi yoyote itakayokuwa tayari kucheza nasi tutacheza nayo.
Mechi na Burundi itanipa mwanga wa nini anatakiwa kufanya ili kuwa na timu itakayotoa changamoto mbele ya Tunisia.
“Baada ya mechi yetu na Burundi, Tunisia nao watakuwa na mchezo na hiyo ndio nafasi yangu ya kuangalia nini wanafanya na kisha kulinganisha na kile kitakachojitokeza kwa Burundi na kuanza mpango wa kujenga timu ya ushindani,”alisema Ndayiragije
from Author
Post a Comment