DKT. YONAZI AWAASA WATUMISHI WA OFISI YA WAZIRI MKUU KUONGEZA BIDII NA UBUNIFU KATIKA UTENDAJI |Shamteeblog.




Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, ametoa wito kwa watumishi wa ofisi hiyo kuongeza bidii, nidhamu na weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya Taifa.

Dkt. Yonazi alitoa rai hiyo Julai 29, 2025, wakati akifungua mkutano na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, akisisitiza umuhimu wa mshikamano, ubunifu na utendaji kazi kwa viwango vya juu, ukizingatia kuwa huduma wanazotoa zinagusa maisha ya mamilioni ya Watanzania.

“Tunaposhirikiana, tunajenga nguvu ya pamoja ambayo hakuna changamoto inayoweza kutuzuia. Nawaomba tuendelee kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo mmoja. Kumbukeni kuwa kila mchango wenu una thamani kubwa katika kufanikisha malengo ya ofisi yetu na Taifa kwa ujumla,” alisema Dkt. Yonazi.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kushughulikia changamoto zinazohusu maslahi ya wafanyakazi. Pia, italenga kukuza ubunifu, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa maendeleo ya kazi na kuhakikisha kila mtumishi anawajibika ipasavyo.

Mkutano huo pia umewapa watumishi fursa ya kupata elimu kutoka kwa wataalam wa Mfuko wa Uwekezaji wa UTT kuhusu umuhimu wa kuwekeza. 

Vilevile, watumishi wanapewa mafunzo kuhusu uzingatiaji wa maadili ya utumishi wa umma, afya, hususan kinga dhidi ya homa ya ini na magonjwa yasiyoambukizwa.







By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post