Mtunzi:AidanShamte 0679784428/0742621952
Mwanzo
ILIKUWA bahati ya kipekee msichana mrembo kutoka jiji la Kampala alitokea kumpenda.
Walikutana katika tamasha la muziki, alikuwa anacheza peke yake kipweke akasikia sauti ikipasua anga katika himaya ya masikio yake.. ‘tunaweza kucheza wote’ hakujibu kwa maneno akamgeukia wakaanza kucheza, angeweza vipi kumkatalia msichana Yule mtulivu wa umbo na mwepesi kutabasamu. Baada ya kucheza sana, msichana akataka kuaga, mwanaume naye akasema yu njiani kuondoka. Wakatoka wote nje, mwanaume akiwa na pensi chakavu na fulana inayokaribia kufubaa…
Mwanaume hakutegemea kama msichana Yule alikuwa na usafiri wake lakini ilikuwa hivyo.
Alimpatia lifti katika gari lake. Wakafahamiana na huo ukawa mwanzo wa kuwasiliana kiukaribu zaidi.
Msichana yule akajitambulisha kwa jina la Caroline Mduma, naye mvulana hakusita kujitambulisha kwa jina lake la kuzaliwa Benard Ngayoma ama alivyozoeleka Ben.
Kituo cha Magomeni Mikumi ndipo Ben alipoishia, Caro akaagana naye huku akijitambulisha mahali anapoishi ‘Naishi Mbezi ya kimara’
“Asante sana kwa lifti….” Ben alimalizia huku akishuka garini.
Milango ikafungwa gari ikaikamata barabara na kutoweka.
Akiwa katrika kibanda chake cha chumba kimoja alichoishi na rafiki yake, usiku majira ya saa nne simu yake ikaita. Ilikuwa namba ngeni. Akaogopa kupokea akihofia wadeni wake huenda wanamtafuta. Ile hali ya kushindwa kupokea simu ikamfadhaisha sana na kujitambua kuwa alikuwa masikini wa kutupwa.
“Pokea simu kaka…unadhani ukiipotezea nd’o mwisho wa matatizo.” Rapha alimsihi Ben. Alipotaka kuipokea ikawa imekatika.
Alipotaka kuitazama namba kwa makini mara simu ikaita tena.
Ben akapokea.
Sauti ya kike ikamlaki kwa bashasha la aina yake.
“Mh unawahi kulala jamani au nd’o namba mpya hupokei mwenzetu.”
“Aaah…si unajua tena…aah” akajibu kipumbavu bila kujua anataka kusema nini.
“Caro hapa usije ukadhani kidemu chako cha kule Temeke.”
“Caro….Caro…” alijaribu kulitafakari jina.
“Caroline Mduma….tumekutana tamashani.” Alimalizia utambulisho wake.
Ben akakaa kitako hakutegemea kabisa kupokea simu kutoka kwa mrembo yule ambaye alionekana dhahiri kuwa hakuwa na shida ndogondogo.
Mazungumzo yakaendelea…walizungumza kwa takribani dakika hamsini. Wakayazungumzia maisha ya Dar kidogo, wakapitia na adha ya usafiri wa Dar wakikumbushiana foleni kubwa kutoka maeneo ya ‘Faya’ hadi mataa ya Magomeni mapipa. Maongezi yakapaa zaidi na kuufikia ubinafsi. Hapa wakaombana wao kwa wao wasiongee sana wapeane miadi wataongea ana kwa ana.
Wakakubaliana na kuagana.
Benard akamsimulia Rapha. Wakalala wakiwa na tafakari hiyo kichwani. Caro.
*****
LICHA ya kuishi Magomeni, Ben hakuwahi kula wala kunywa katika hoteli ya Travertine iliyopo mkabala na barabara ya Morogoro. Siku hiyo alikuwa anakula kwa bili ya Caroline Mduma.
Caroline alimtazama Ben kwa macho ya kuibia akagundua kuwa kuna mambo kadhaa Ben alikuwa hayajui. Kwanza ni uvaaji, Ben alikuwa amevaa mavazi ambayo huenda kwake yalikuwa stahiki kutokana na uchumi lakini machoni alionekana kama mshamba, shati kubwa kumzidi viatu vya ngozi ngumu visivyong’ara na suruali nayo ilimpwaya laiti kama zisingekuwa jitihada za mkanda wake kiunoni ingeweza kumwadhiri wakati wowote.
Hilo Caro alilimezea…..akaliona jingine wakati wa kula. Ben hakuwa akifahamu kutumia Uma na kisu katika kula chakula, alihangaika sana kula nyama laiti kama asingekuwa Caro huenda angenawa na kutumia mikono. Kama hiyo haitoshi kila Ben alivyotupia tonge mdomoni alikumbwa na ugonjwa unaowakabili waswahili wengi.
Ugonjwa wa kutafuna chakula huku mdomo ukiwa wazi….
Ben hakuwa na staha hiyo…..
Walizungumza mengi baada ya chakula. Caro akasema hili na Ben akaongezea lile. Mara wagonge viganja vya mikono yao mara wacheke vicheko vilivyojaa staha.
Ilikuwa saa kumi hatimaye ikatimia saa tatu usiku.
Kila mmoja alikuwa kimya wakitazamana. Kuna jambo Caro alikuwa ameliweka mezani. Jambo ambalo Ben hakulitarajia….
Mapenzi!! …..Caro alijielezea kuwa anampenda Ben.
Ben hakutaraji…hakika hakutarajia jambo hilo hata kidogo.
Kupendwa na msichana mrembo wa haja muhitimu wa chuo kikuu nchini Uganda. Mwenye kazi yake……
Hakika ilikuwa ngumu kuamini…..
Akatamani kusema ‘nakupenda pia’ akahofia kuonekana mwepesi kulaghaika….
Akataka aseme ‘nitakufikiria’ hili akaona ni jibu la kike kike…akalipuuzia.
“Ben…” Caro akaita kwa sauti tulivu.
“Caro…” Ben akaitika….
“Nisamehe kama nimekukwaza…”
“Hapana Caro hujanikwaza ila….ila….ni kama siamini yaani….”
“Kwanini Ben sifananii ama.”
“Mimi ni masikini ujue, na nimekueleza maisha yangu. Usidhani nimekutania hata jambo moja, yaani maisha yangu ni magumu wewe…acha tu Caro yaani hata chakula na….”
“Pliiz Ben…hayo ni mengineyo. Nakupenda ndo jambo ambalo nimelileta mezani.” Caro akamkatisha.
“Caro sidhani kama nina hoja ya kupingana nawe…sikuwa na mpenzi kwa muda mrefu…sikuwa na wazo la kuingia katika mahusiano, nikisema nipo tayari namaanisha hayupo atakayeumia hakuna nitakayemsaliti…..NIPO TAYARI CARO.” Hatimaye Ben akajitia ujasiri akazungumza. Sauti yake ya upole ilivutia kuisikiliza japo ilihuzunisha.
Usiku huu ukawa wa aina yake. Wakaongozana hadi nyumba anayoishi Ben. Licha ya Ben kumzuia sana Caro asifike ‘geto’ kwake, binti yule aligoma kabisa.
Walimkuta Raphael akiwa amejilaza. Chumba kilikuwa na giza na mbu walishindana kupiga miluzi. Caro hakujali. Aliingia. Taa ikawashwa. Rapha akawakaribisha.
“Rapha mambo…” Caro akawahi kujipa uenyeji. Rapha akatabasamu.
“Poa shem..” akajibu. Ben akaona aibu akainama. Mazungumzo ya hapa na pale, kisha Caro akaaga.
Usiku huu ulikuwa wa mwisho kwa Ben kulala kwa shida.
Caro akamkaribisha nyumbani kwake maeneo ya Mbezi ya kimara.
Rapha akapatiwa pesa kwa ajili ya kupanga chumba kingine ama kukiboresha chumba alichokuwa anaishi.
Ben akaanza maisha mapya akiwa na Caro kama mpenzi wake.
Mambo yalienda upesi upesi. Ben akanunuliwa nguo zilizoendana na mwili wake, akalipiwa ada katika kituo cha kufanyia mazoezi ya viungo. Kila baada ya kutoka katika mazoezi ya viungo alikuwa anaingia kujifunza kuendesha gari.
Mazoezi yakamkubali kifua kikatanuka, mikono ikajaa nguo nazo zikamkubali. Caro akakiri kuwa Ben alikuwa mtanashati haswa. Jambo hili lilimpa furaha kubwa maana alipolenga ndipo penyewe haswaa.
Ben hakuachwa awe baba wa nyumbani ndani ya miezi miwili ya mapenzi motomoto alikuwa amefunguliwa duka la kuuza spea za magari, mitaa ya Msimbazi Kariakoo. Biashara ambayo aliimudu vyema.
Haikupita siku bila Ben kuzungumza na mpenzi wake kuhusu biashara inavyokwenda…..alikuwa mkarimu na mwenye maadili.
Ni jumapili pekee ambayo hakuwa akienda kazini. Siku hii waliitumia kuhudhuria ibada kanisani na kutoka kidogo kwa ajili ya kujiburudisha. Walipendeza kuwatazama.
Wakati huo alikuwa anaendesha gari yake aliyopewa na Caro lakini kadi haikubadilishwa jina ilibaki kuwa mali ya Caro na hakuna aliyejali.
Ben akawa jamali wa sura kutokana na chakula kizuri na upungufu wa mawazo kichwani.
MWEZI WA NNE tangu waanze kuishi pamoja Ben aliyekuwa na pesa za kutosha katika akaunti yake akaanza visa, mara achelewe kurudi nyumbani. Mara alalae kwa rafiki zake ambao Caro hakuwajua. Caro alipouliza majibu yakawa ya mkato.
“Mpenzi leo ni siku ya ibada…”
“Wewe ndo Yesu ama?” Ben alijibu bila kujali lolote.
Zamani simu ya Ben ilikuwa simu ya Caro lakini sasa aliweka ‘password’ na hakutaka kujibu kwanini amefanya hivyo. Zamani simu zilizopigwa alizipokea bila shaka lakini sasa akawa anachagua simu za kupokea.
“Mbona simu inaita unakata.” Caro alihoji.
“Simu yako imekushinda unahamia kwenye simu yangu.” Alijibu kwa jeuri. Kisha akatoweka sebuleni
Caro aliugundua mchezo ule jinsi ulivyokuwa unaenda lakini alijiweka katika upande wa mwanamke mstaarabu hakutaka shari. Akauliza kistaarabu sana na hata alipojibiwa kwa shari hakuacha kumwekea mpenzi wake maji bafuni.
Siku moja alihoji……
“Baba Caro….kuna jambo nahitaji kuzungumza nawe.”
“Nakusikiliza.”
“Ni kuhusu kuoana…” Caro alisema. Ben akashtuka hakutegemea hoja ile...
“Bado mapema Caro….yaani hata mwaka hatujafikisha aisee.”
“Umeniitaje?” Caro alishtuka kwa mara ya kwanza katika uhusiano wao Ben anamuita kwa jina lake la kuzaliwa wakati walizoea kuitana, ‘mama Ben’ na ‘baba Caro’.
“Nimepitiwa tu…” alijibu bila hofu. Caro akakaa kimya.
Caro akajikunyata kama kuku aliyemwagiwa maji ya baridi. Lakini kichwani akitafakari mengi, alikuwa akimtafakari Ben huku akitafakari na swali alilotoka nalo Uganda. Aliona kama jibu linakaribia.
“Maana nina mimba kwa sasa…” Caro alimweleza baada ya kunyanyua kichwa.
“Car…aah mama Ben,,una mimba…mimba ya nini kwa sasa, unataka tupate mtoto nje ya ndoa….” Aling’aka Ben. Caro hakusema neno kwanza akatulia.
“Mara yetu ya mwisho kutumia kinga ni lini unakumbuka.” Caro aliweka msumari. Ben akagundua kuwa tangu wapime na kujikuta hawana virusi hawajawahi kutumia kinga. Soni ikamshika.
KITENDO cha Ben kusikia Caro ana mimba ndo kilimuhamisha kabisa nyumbani. Akawa hakosi kuhudhuria kwa Zulfa, msichana kigoli aliyekuwa amemdatisha. Kila alichokuwa anasema Ben alitii, karibia kila siku alipomtembelea alimwachia shilingi lakini moja hadi moja na nusu. Pesa ilikuwepo kwa nini asimwachie. Alifanya yote haya kwa jeuri ya pesa. Pesa ambayo amesahau chanzo chake.
MWEZI WA TANO wa mahusiano hali ilizidi kuwa tete. Ben akawa na sauti kuu zaidi katika nyumba, Caro akakosa amani, kila mara alikuwa anagombezwa bila kujalisha ni katika simu ama ana kwa ana. Ben alikuwa kama kichaa. Mara akagundulika kuanza kutumia pombe, akawa muhudhuriaji mzuri wa kumbi za starehe zinazosadikika kuwakamua watu wengi pesa hapa mjini. Huko kwenye hizo kumbi Ben akawa mpenda sifa aliwatuza wacheza shoo na waimbaji. Kibaya zaidi Ben akakumbwa na tamaa ya kutembea na wasichana warembo, hakuwakosa kwa sababu alikuwa na pesa wakajikosha akafanya nao mapenzi. Maisha yakaendelea.
Caro alipogundua hili akaamua kuwa makini. Hakuna mapenzi bila kinga la sivyo hakuna kufanya kabisa. Hali hii ikamkera Ben akazidi kujikita kwa kimada wake. Hilo nalo Caro aliligundua kupitia kwa marafiki wa Ben wenye tabia za kishakunaku. Ilimuuma sana lakini alifurahi kwa sababu alikuwa analipata jibu.
MWEZI WA SITA alimbadilikia Ben, akaanza kuwa mkali na muulizaji wa kila kitu kinavyoendelea. Ben hakutaka kutoa ushirikiano alikuwa jeuri na asiyeshaurika. Hata Rapha alikuwa amegombana naye tayari na Ben hakujali lolote kwa sababu alikuwa na pesa. Aliamini kuwa pesa ni kila kitu kwake…
Caro alipohoji juu ya ugomvi wake na Rapha kwa mara ya kwanza akajikuta akipokea kipigo kutoka kwa Ben, kipigo kitakatifu. Masikio yake yalisikia akiitwa jina baya ‘MALAYA’, Caro amekuwa Malaya?
Hakika aliumia lakini bado alitabasamu moyoni maana alikuwa anazidi kulipamba jibu lake…
Zilikuwa zimebaki siku kadhaa mkataba wake wa mkiezi sita katika nyumba ile uweze kumalizika na hakuwa na mpango wowote wa kuongeza muda wa kuishi pale na mwenye nyumba alitambua hilo. Kila kitu ndani ya nyumba ile kilikuwa mali ya mwenye nyumba. Ni nguo pekee na vitu vingine vidogo vya ziada ndo vilikuwa vya wapangaji.
Hizo ni aina ya nyumba za kupanga jijini ambazo malipo yake huwa makubwa sana na mara nyingi familia za kitajiri humudu…..
Ni nyumba ambazo huna haja ya kuhangaika kuhamisha mizigo mingi wakati wa kuhamia na kuhama.
CARO alijikusanyia kilicho chake. Kwa sababu lilikuwa jambo la kawaida sana Ben kuacha kurudi nyumbani hata kwa siku tatu bila taarifa….Caro hakuhangaika. Alifurahi kuyakuta magari yote mawili yakiwa uani. Ben hakuondoka na gari siku hiyo….
Caro akapiga simu kwa watu aliofahamiana nao. Wakayaondosha magari na mizigo yake kidogo pamoja na nguo nyingi za Ben. Akamuaga mwenye nyumba na kumkabidhi funguo zake.
SIKU iliyofuata ndege ikatua katika uwanja wa kimataifa nchini Uganda.
Caro akapokelewa na marafiki zake waliokuwa na shauku ya kuonana naye tena. Wote walingoja majibu kutoka kwa binti huyu.
Caro hakuwa na papara. Walipofika mahali tulivu alianza kuwasimulia. Walianza wao kumkumbusha swali aliloondoka nalo.
“UTAITAMBUA VIPI TABIA HALISI YA MWANADAMU?”
Caro Mduma akatabasamu. Kisha akatoa majibu kwa utaratibu.
“Ukitaka kumjua vyema mwanadamu tabia zake mpe pesa, pesa za kutosha utamfahamu vyema. Mngemuona huyo Ben wallah msingeweza kumdhania kama anaweza kubadilika…alikuwa mshamba hajui kuvaa na mtaratibu tena mnyenyekevu mno. Sijui nilivutika nini kuamua kumtumia katika kulijibu swali langu lakini niliamua kuwa naye. Mwanzoni alikuwa ana mapenzi ya kweli hauwezi amini kidogo mwenzenu nishawishike kuwa awe mpenzi wangu wa maisha kwa jinsi alivyonicare, yaani alikuwa ni husband kweli lakini mambo yakabadilika baadaye. Akageuka mbogo baada ya pesa kumzoea…mshenzi sana kumbe. Nilimzuga nina mimba akaonekana kama anataka kuikataa…..nikamdanganya tuoane yote hayo akakataa, nilikuwa namfuatilia sana viwanja zake. Hakuna mtu anapenda sifa kwa wasichana kama Ben, Ben alinyanyua mikono akanibamiza baada ya kumuuliza kwanini amegombana na rafiki yake…, hakuna mwanaume limbukeni kama yule, alitekwa na manzi mmoja hata Yule msichana alikuwa mbaya class kwetu anamzidi. Akawa anampatia pesa kila leo….eti akagombana na rafiki yake aliyekuwa anamuhifadhi kwa room yake. Akadhani mimi mjinga kumbe nipo katika kutafuta jibu. Nimemwacha solemba. Sijui atachanganyikiwaje tu….amebaki na biashara yake hiyo ndo zawadi kwa kunisaidia kupata jibu. Yaani ningekuwa nimempenda kweli sijui nini kingehappen….” Caro alimaliza. Kila mmoja alikuwa akimtazama katika namna ya kumshangaa. Lakini wakaelewa azma yake. Hakika alikuwa amelipata jibu kwa vitendo.
MWISHO.
Post a Comment