SIMULIZI-WARIDI LA MAPENZI SEHEMU YA KWANZA


WARIDI LA MAPENZI

Mtunzi: Aidan Shamte

Na:0679784428/07426621952

(Kutokana na Kisa cha Kweli)
Tukusuma Mpoki alikuwa amesimama kwenye baraza la nyumba yake, uso wake ukiwa umekunja ndita, jasho likimtiririka, na macho yake yakiwa yanabubujikwa na machozi. Alikuwa amejifunga kanga moja tu kati ya eneo la kifuani na kiunoni na hivyo kuonesha mapaja yake yaliyonawiri vizuri na hivyo kulidhirisha kwa kadamnasi umbo lake lake la nyigu. Chini ya kanga hiyo alikuwa amevaa chupi ya rangi nyekundu. Licha ya upepo wenye joto la jiji hilo la bandari salama kumpulizikia bila kukoma Suma aliendelea kusimama kwenye baraza la nyumba hiyo. 
Hakujali watu waliokuwa wamesimama upenuni wakimshangaa binti huyo wa Kinyakyusa akiwa katika hali ya hasira na aliyekuwa akipaza sauti yake akimtukana mumewe bila kufunga breki. Mkono wake wa kushoto uliokuwa umevikwa bangiri za rangi ya dhahabu ulikuwa umekunjwa kwenye kiwiko na kuegeshwa kama gari la kijapani kwenye kiuno cha binti huyo kilichokuwa kimehifadhi vyema mviringo wa makalio yake uliokuwa kama vitunguu maji vinavyolimwa kule Tukuyu.

Mkono wake wa kulia ulikuwa umeinuliwa juu, huku kidole cha kati kikining’inia hewani utadhani kimepigiliwa msumari katika staili ya kumzodoa mtu. Kucha zake ndefu zilizopakwa rangi nyekundu inayong’ara zilionesha ni jinsi gani Suma (kama alivyozoea kuitwa mtaani) alivyokuwa anajijali. Nywele zake ndefu zilizosukwa kwa mtindo wa rasta zilining’ia mabegani kama nywele za simba jike. Suma alikuwa amekasirika, na hasira yake ilionekana wazi siku hiyo. Hakuna aliyewahi kuhisi kuwa dada huyo anaweza kuweza kumpaka mtu hadharani namna hiyo.

“Toka hapa, unadhani mwanamme peke yako” Alifoka binti huyo huku sauti yake yenye lafudhi ya mbali ya kinyakyusa ikipasua anga la eneo hilo la Chang’ombe.
“Yaani kukupenda wewe ndio imekuwa nongwa, mwanamme gani huridhiki, kama penzi langu hulitaki si uende huko huko ulikolala jana, firauni mkubwa, kama unafikiri huyo malaya wako anaweza kukupenda kama nilivyokupenda sasa mbona umerudi hapa?” Aliendelea kubwata bila hata ya kumeza mate. Sauti yake ikiwa kavu na isiyoonesha kujali nani anasikiliza au nani anamuangalia. Watu walifurahia sinema hiyo ya bure.

Hatua kama kumi hivi toka mlango wa nyumba yake ambayo ilikuwa ni ya mwisho ikipakana na nyumba za Polisi za Chang’ombe alikuwa amesimama Sospeter Mkiru, mdomo umemdondoka utadhani amemuona mzee Ole wa Usiku wa Balaa, na mkononi akiwa bado ameshikilia shati la lilikuwa limechanika mgongoni baada ya Suma kulishindilia kucha za uhakika.
“Jamani Suma nisamehe mpenzi sitarudia tena” Alisema Sosi huku maneno yake yakitoka kwa kukwamakwama kama maji yanavyotoka kwenye mpira wa kumwaligia maua. Soni zilimshika. Alijikaza kisabuni huku akibembeleza apewe nafasi nyingine.

“Nikusamehe mara ngapi nyang’au mkubwa we!” Dada Suma utadhani ametiwa ufunguo aliendelea kumpaka. “Jamani hata uvumilivu una mwisho. Mimi sasa basi, nenda huko unakokwenda kila siku utanletea magonjwa bure miye”
“Tafadhali Suma nisamehe mke wangu” Sosper alianguka na kupiga magoti kwenye mchanga uliokuwa unajoto. Alijaribu tena kumbembeleza binti huyo.
“Nenda kafilie mbali, hayawani mkubwa” Suma alisema huku akimwelekeza Sosi kwa kidole kuondoka hapo. Hayo yalikuwa ni maneno ya mwisho ambayo Sospeter aliyasikia toka kwa Suma Mpoki. Alimuona Suma akigeuka na kuelekea ndani ya nyumba.

Sosi alijua kuwa safari hii amevurunda kweli kweli. Uchungu ulianza kumpanda pole pole na donge la hasira ya kumpoteza waridi lake na mpenzi wake wa toka shule lilimkaba shingoni. Alijihisi kuwa amejidhulumu penzi na anastahili adhabu hiyo kali. Alitamani amkimbilie Suma na kujiangusha miguuni mwake na kumwomba radhi huku akijigaragaza. Akili yake ilianza kwenda kwa kasi akijiuliza ni shetani gani lilimwingia hadi kumfanya kwenda kulala na mwanamke waliyekutana kilabuni na kumuacha mpenzi wake wa damu? Alijihisi kizunguzungu. Kama mtoto mdogo Sosi aliunganisha vidole vya mikono yake kichwani huku shati lake akilibeba begani. Watu waliokuwa wamesimama kushuhudia tukio hilo walianza kujipangua taratibu huku wengi wakimuonea huruma Sospter na wengine wakisema wazi kuwa “amejitakia” mwenyewe. 

Wachache hawakuficha dhihaka yao kwani walimcheka hadharani na kumuona kweli huyo jamaa wa kuja. Sospeter aliapa hatarudi tena mitaa hiyo kwa aibu aliyoipata Chang’ombe. Akiwa haangaliki anakokwenda, Sosi alijikuta yuko katikati ya barabara ya Chang’ombe huku magari yakijaribu kumkwepa, na watu wakimrushia matusi ya kila aina hata matusi yasiyosajiliwa. Gari aina ya Fuso ambalo lilikuwa limeshehena mashabiki wakitoka uwanja wa Taifa lilijitahidi kufunga breki na kumkwepa kwa ustadi mkubwa. Sauti ya breki zake ziliumiza masikio ya watu. 

Mlio wa mshtuko wa watu ulitanda angani, huku watu wakishika vichwa vyao na wengine kufumba macho wasione kile kilichokuwa kitokee.. Sospeter hakupata nafasi ya kukwepa Fuso hilo, kwani alirushwa juu kama kopo tupu la kimbo. Alipotua kwenye lami yenye mashimo mashimo, mwili wake ulikuwa hauna ishara yoyote ya uhai ndani yake. Watu walikimbilia hapo kuangalia kilichotokea, huku kina mama wakipiga kelele ya kilio wakiwaficha watoto wao wasishuhudie jambo hilo.
Bila kusogea hata sentimeta moja, Suma alijisemea moyoni “Ukome!” Suma aligeuka kwa haraka huku akiangua kilio alichokuwa amekizuia kwa muda na kuingia ndani ya nyumba ambayo alikuwa anaishi na wadogo zake. Mwili wote ulikuwa unamtetemeka huku hisia ya furaha ya kisasi na hatia ya uovu vikimkaba rohoni. Moyo wake ulikuwa umejeruhiwa kwa mapenzi na kumbukumbu ya mapenzi ilimuumiza mtima. Alijihisi amepoteza muda mrefu na kijana Sospeter ambaye walikuwa wakiishi kama mume na mke. Alijidharahau na kujiona kweli “amepatikana” kwa kukubali penzi la kijana huyo chakaramu. Aliapa moyoni mwake kuwa hatopenda tena, kwani wanaume ni kama mbwa. Aliendelea kulala kitandani huku ameukumbatia mto huku moyo wake ukipaza sauti ya kilio chake mbele za Mungu. Aliendelea kulia hadi alipopitiwa na usingizi huku akiwaza jinsi alivyokutana na Sosi kwa mara ya kwanza.
                                                                   * * *
Ilikuwa mwaka 1992 kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo ya Sekondari Tanzania ngazi ya Mkoa ambayo kwa mara ya kwanza yalikuwa yanafanyika kwenye shule ya Sekondari ya Karatu iliyopo pembezoni mwa barabara iendayo mbuga maarufu ya Serengeti nje kidogo tu ya mji wa Karatu. Wakati huo mji wa Karatu ulikuwa bado ni Wilaya ndogo katika mkoa wa Arusha. Shule karibu ishirini za Sekondari kutoka kila kona za mkoa wa Arusha zilikuwa zinawakilishwa kwenye mashindano hayo ambayo hatimaye yangeteua timu ya mkoa ambayo ingewakilisha mkoa wa Arusha katika mashindano ya UMISETA yaliyokuwa yanafanyika baadaye mwaka huo huko Morogoro. 

Sospeter alikuwa ni golikipa namba moja wa timu ya Soka toka shule ya sekondari ya Singe iliyoko Babati. Sifa zake zilienea kwenye mashindano hayo kwani aliokoa penati tano katika mechi mbalimbali ambazo ziliifanya timu yake kushiriki katika mashindano hayo. Hata hivyo sifa hizo hazikumfanya awe anajipendekeza au kujiona yeye bora zaidi. Nje ya uwanja alikuwa ni kijana mcheshi, mwenye kupenda utani, lakini anayeheshimu kila mtu. Akiwa kwenye lango alikuwa ni tishio kwa timu ya ugeni kwani alikuwa na manjonjo ya Juma Pondamali na udhibiti wa goli wa Idi Pazi. Alikuwa na mbwembwe golini kiasi cha kuwafanya washambuliaji wa timu ya ugeni kupenda kujaribu mashuti ya mbali kwani wakimsogelea huwa anawazogoa na kuwatania kiasi cha kuwafanya wakasirike na hivyo kushindwa kutilia mkazo ufungaji magoli. Kwa mtindo wake huo watu walimfananisha na aliyewahi kuwa golikipa wa Coastal Union, Duncan Mwamba.

Upande mwingine kulikuwa na timu ya Netiboli toka shule ya Sekondari ya Kilutheri ya Dongobesh wilayani Mbulu. Kati ya shule zote zilizowakilishwa kwenye mashindano hayo timu ya Dongobesh ndiyo ilionekana kutoka mbali zaidi na wachezaji wake kuonekana ndio washamba zaidi. Hata hivyo watoto wengi wa wakubwa ambao walikuwa watundu huko mijini walitupwa huko kwenye shule hiyo ya bweni iliyozungukwa na kijiji cha kale cha Dongobesh. Timu yao ya Netiboli ilikuwa inacheza vizuri lakini sifa kubwa ilikuwa inatokana na dada aliyekuwa akicheza nafasi ya senta, alikuwa ni gumzo hapo Karatu. 

Kwanza kwa sababu ya uzuri wake na umbo lake la kimalaika. Wenyewe walimpachika jina la Angel hadi wengine walidhania ndio jina lake halisi. Alikuwa na mvuto wa ajabu kwa wavulana na wasichana. Lakini pamoja na sifa zake zote Suma alikuwa anaakili darasani na tangu aingie shule ya Dongobesh hajawahi kushika nafasi chini ya pili. Alikuwa akipishana na kijana mmoja ambaye baadaye alijulikana kwa kazi yake ya uandishi, hadithi, na utunzi mbalimbali kwenye mtandao wa kiintaneti.
Dongobesh walikuwa wanacheza mechi ya mwisho dhidi ya timu ya Madunga ambayo ilikuwa ni mpinzani wa jadi. Sospeter kwa kuitikia mwito wa rafiki zake waliokuwa wanamsifia Suma aliamua kwenda kuangalia mechi hiyo, siyo kwa ajili ya kuona nani atashinda bali kuona kama kweli hizo sifa za Suma zilikuwa ni za kweli au ni porojo tu za kwenye Umiseta. Alipofika na kumuona jinsi binti huyo alivyokuwa anapendeza katika mavazi yake ya netiboli ambayo yalimfanya aonekana kama amepotea toka Mbinguni na wanamtafuta, Sosi alijikuta akimkodolea macho dada wa watu utadhani ameona hazina ya mfalme Solomoni. 
Sosi hakutaka kuangalia kitu kingine chochote na alijikuta anaungana na wadau wengine kushangilia kila Suma alipokuwa akitoa pasi na kudaka mpira. Mara mbili alijikuta anagonganisha macho yake na Suma ambaye na yeye alianza kumwangalia na kila akidaka mpira basi anaweka madoido kidogo kumlingishia Sosi (kama ilikuwa kweli au hayo ni mawazo ya Sosi tu miye sijui).
Mechi iliisha kwa timu ya Dongobesh kushinda na furaha kubwa ilitawala upande wa mashabiki wa Dongobesh wakiongozwa na shabiki aliyejipachika Sospeter Mkiru. Ilikuwa ni furaha kubwa kwani timu ya Dongobesh haijawahi kuifunga Madunga kwa miaka mitano mfululizo hivyo ilikuwa ni furaha kwa mwalimu wa Michezo Michael Tluway wa shule hiyo. Aliyekuwa na furaha zaidi ya Sosi alikuwa ni matroni wao Vera Akonaay. Wakiwa katika shamrashamra za kusherehekea Sospeter alitembelea kumwelekea Suma aliposimama mbele yake alijikuta ananyosha mkono wa pongezi kwa kapteni huyo wa Dongobesh.

“Hongera Sana kapteni” alisema Sosi huku moyo ukimwenda kasi utadhani aliyefukuzwa na simba mwenye njaa.
“Asante sana” Alijibu Suma huku akijaribu kuachilia mkono wa Sosi ambaye alikuwa kama amemng’ang’ania.
“Umecheza vizuri kweli” alijikuta akisema maneno yasiyo na kichwa wala mguu.
“Ndiyo, ila kulikuwa na mtu ananikodolea macho utadhani amepoteza kitu na mimi nimemfichia” Alisema Suma huku mikono yake akiifunga pamoja kifuani. Sosi alishindwa kujizuia kuangalia kifua cha Suma ambacho kilikuwa kimetuna kwa matiti yaliyolala kama paa nyikani na kama midomo ya hua wawili chuchu zake zilionekana kwa mbali. Sosi alimeza fundo la mate kwa aibu.

“Wala usisema maana nilichopoteza nimekipata” Alisema huku akijikaza. Waliweza kuona macho ya watu yakiwaangalia imekuwaje watu hao wawili wazungumze. Na vijana wengi walishangazwa ni jinsi gani Sosi alikuwa na ujasiri wa kuzungumza na binti mrembo kama huyo. Wengine walikiri kuwa kama kulikuwa na mwanafunzi yoyote kwenye mashindano hayo ambaye angeweza kumsimamisha Suma basi alikuwa ni Sospeter.
“Umekipata? Na ulipoteza nini?” alihoji Suma huku macho yake yakimganda kijana wa watu. Moyoni alijisemea kuwa alikuwa ni kijana mzuri, msafi, na jasiri maana vijana wengi walikuwa wanaogopa hata kumsalimia. Walijiona hawafai mbele zake.
“Nimepoteza akili yangu baada ya kukuona, na nadhani nimepata mke kwa maisha yangu yote” Kama mtu aliyepagawa pepo wa mahaba Sosi hakujua maneno hayo yametoka wapi, maana yalibubujika kama chemchemi ifukayo maji ya mapenzi.

“Wacha we!, yaani kuniona tu umeona na mke kabisa!?” Aling’aka Suma huku akikunja uso wake kwa kushangaa na kwa kukutwa hakujiandaa kwa maneno hayo. “Usiniambie umeshaona na watoto na wajukuu?” Aliendelea huku akiangua kicheko.
“Tena watatu, wawili mapacha” Alisema Sosi huku akihesabu kwa vidole vitatu kwanza, kisha viwili. Suma aliendelea kucheka huku akishikilia mbavu zake kwani hajawahi kukutana na mvulana aliyejua anachotaka kama huyo. Mara mmoja wa wanatimu wa Suma walimuita ili waende kubadili nguo na kujiandaa kwa chakula cha jioni.
“Ungependa kula na mimi na tupige soga zaidi” Aliuliza Sosi kabla Suma hajakimbia.
“ah..wenzangu wataningoja” alijibu Suma
“Hapana, tunaweza kwenda kijijini na kununua cha hotelini, mie leo sili dona lao” alijibu Sospeter huku moyoni akiombea kwa miungu yake Suma akubali.
“We, tutawezaje kutoka kambini si ni kujitakia matatizo? Huoni geti kali?”Aliuliza kabla hajakubali baada ya ushawishi wa Sosi. Sospeter alimhakikishia kuwa hawatagundulika na wakakubaliana wakutane saa moja baadaye kwenye lango kuu la shule. Sospeter alianza kutafuta njia ya kuweza kutoka na kurudi jioni hiyo bila kujiletea matatizo yeye mwenyewe na Suma.

Baada ya kuhangaika kufikiri nini cha kufanya aliamua kwenda kwa mzee mmoja wa Kimang’ati aliyekuwa zamu kulinda lango la shule hiyo. Wala hakumchelewesha alimpatia shilingi mia tano na kumuomba chonde chonde amruhusu yeye na Suma waweza kwenda na kurudi kabla ya muda wa kulala ambao ilikuwa ni saa nne kamili za usiku. Mzee wa Kimang’ati kumbe hizo zilikuwa zake. Alizifinyanga hizo pesa kiupole na kuziweka mfukoni. Alimwambia akiwaona wanakuja basi atajifanya anazunguka upande wa pili na geti atalisogeza upande kidogo tu. Na kweli hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani Sosi na Suma walipofika hapo majira ya moja za jioni wakati giza ndio limeanza kuingia kwa nguvu na kunyamazisha sauti za ndege yule mlinzi alizunguka upande wa pili wa kibanda na kujifanya hakuona kitu na pale tu walipotoka alifanya haraka kufunga geti kwa kufuli. Alikaa kuwasubiri warudi.
ITAENDELEA.................................................

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post