UNANIKUMBUSHA VALENTINE DAY?


Mtunzi::Aidan Shamte
Simu: 0679784428/0742621952
Ngoja nikupe kisa kimoja kilichonitokea siku hiyo ya Valentine miaka minne iliyopita.


Naitwa Riziki, nakumbuka siku hiyo nilijiandaa vyema kwani nilishafanya maandalizi ya kutosha siku chache kabla ya siku yenyewe. Uwezo na kipato changu ni kidogo lakini haikunifanya nishindwe kudunduliza kununua tisheti mbili nyekundu zenye maua ya kuvutia ya rangi ya upendo yangu mimi na ya mpenzi wangu Happy, nilinunua na vizawadi kadhaa ambavyo nilitaka nimfurahishe laaziz wangu barafu wa moyo wangu. Niliandaa pia vijihela vya kutosha kwa matumizi ya siku hiyo.

Basi siku ya siku ilifika na kwa kweli niliisubiri kwa hamu kwani sikuwahi kusherehekea siku hii nikiwa na mpenzi wangu. Tangu asubuhi niliziona saa zikijongea taratibu sana kama vile kuna mtu alikua akizishikilia zisisogee. Hatimae muda uliwadia  nikaanza kujiandaa. Mimi nilikua naishi chumba cha kupanga maeneo ya Kambarage Shinyanga mjini lakini mpenzi wangu Happy yeye aliishi Mwadui kilometa kama 25 hivi kutoka shinyanga mjini. Kwakua tulikubaliana na Happy aje Mjini ambako ndipo pamechangamka tofauti na kule Mwadui basi wakati nafikiria kujiandaa nae alinipigia simu ndio anajiandaa kutoka. Basi nilianza kujiandaa taratibu kwani kutoka Mwadui mpaka shinyanga ni umbali wa kama lisaa limoja. Mtoto wa kiume nikaoga mara mbili mbili nikamaliza nikaingia kuvaa nikatupia jinzi langu la mabaka mabaka nililonunua mitumbani soko la Ngokolo juu nikatupia tisheti langu jekundu ambalo lingine nilimpa Happy kwa ajili ya siku hiyo shingoni nikaning'iniza cheni kubwa la rangi ya Silva ambalo nilimtapeli mshkaji wangu Fulani, chini nikatupia raba zangu nyeupe ambazo nilizipiga rangi nyeupe kwa ufundi mkubwa zikang'aa na kunifanya nipendeze nahisi tangu nizaliwe sijawahi kupendeza hivi Riziki Mimi. Nilipomaliza nilichukua vimarashi vyangu nilivinunua buku jero lakini vina harufu nzuri utadhani pafyumu ya gharama sana. Baada ya hapo nikachukua simu yangu ya kichina ambayo niliinunulia kava la bei ghali ikavutia, kisha usoni nikatupia miwani nyeusi ambayo niliiokota kwenye gari siku moja hivi kisha nikatia komeo chumba changu nikaelekea kituoni kumpokea wa ubani wangu. Njiani mwondoko nilibadilisha. Kwa kua kituo hakikua mbali basi niliamua kutembea, basi mwanaume nikatembea nadunda kama viatu vina springi. Mkononi nina kimfuko chenye maua ya kupendeza ambamo ndani yake kuna zawadi za happy.
   Basi nikiwa kituoni niliwasiliana na Happy ambae aliniambia yupo karibu nikavuta subira kumsubiri chaurembo wangu. Kwa kweli mapigo ya moyo yalikua kasi na moyo ulidunda kwa nguvu kama kuna mtu anapiga ngoma ndani ya moyo wangu.
  Wakati namsubiri Mara alishuka dada mmoja katika bodaboda, alikua amevaa gauni jekundu, mkoba mwekundu na chini viatu vyekundu hakika alipendeza sio siri na ukichangia vile alikua mzuri acha tuu Mungu kaumba. Nilimtazama, nikamtathmini akili zikaganda kwa muda, mpaka akaanza kuvuka barabara ndipo nikahamisha jicho baada ya kuona gari ambayo inatoka Mwadui ikiingia kituoni.
Asalaaaleee!!!!! Ghafla kilitokea kishindo na ukelele mkubwa, mamaaaaaaaaa......
      Hapo kila mtu aligeuza macho na mimi nikiwa mmoja wapo. Alikua ni yule dada niliyekua namkodolea macho safari hii alikua chini anagaragara, watu walianza kusogea eneo lile baada ya boda boda iliyomgonga kuondoka kwa kasi. Nami nikajisogeza kushuhudia haraka ili nimuwahi Happy ambae angekua anashuka kwenye gari, nilijipenyeza kwenye kijikundi cha watu hadi pale alipo yule dada ambae alikua anagara gara pale chini. Cha ajabu hakuna aliyeonekana kumpa msaada wengi walishuhudia wakawa wanajitoa mmoja mmoja wanawapisha wengine, cha ajabu wengine badala ya kutoa msaada wao walikua bize kupiga picha, watanzania sijui tumekuwaje siku hizi. Yule Dada pale chini alinitupia jicho la kukata tamaa akanisemesha kwa shida, ka..ka nisa...i..di..ee ta..fa.dhali.. Hapo akili ikafunguka nikajua nini nilipaswa kufanya. Nikauweka mfuko wangu chini nikamnyanyua japo alikua mnene kiasi hakunipa shida, angenipaje shida wakati ninafanya kazi za shuruba kila siku za kubeba magunia ya dengu na choroko kiwandani? Nikambeba kuelekea zilipo taksi, wakati naikaribia taksi macho yangu yakagongana na ya mpenzi wangu Happy aliekua ananitazama. Hapo nikashtuka kidogo nikampa ishara ya macho anifuate, lakini alinitazama tu basi nikaona isiwe shida wacha nimuwahishe  hospital niokoe uhai wake kisha nimuwahi Happy. Tukaondoka mpaka hospitali ya mkoa nikamwacha Happy pale stendi. Tulipofika hospitali eti wakagoma kumpokea eti mpaka twende polisi tukapewe sijui wanaita PPF.... Sijui PF nini hata sikumbuki vizuri. Yaani hizi sheria za Tanzania nazo, eti mgonjwa yu taabani badala ya kupata huduma eti twende polisi. Basi tukafanya hivyo tukafanikiwa akapokelewa hospital, kwa kua sikumfahamu jina Basi nilimwandikisha kwa jina la Happy Riziki. Baada ya taratibu za hospitali niliamua nimuwahi happy wangu kule stendi kwa mgonjwa ningerudi baadae.
Mhhhhhh! Nilizunguka mno pale stendi sikumwona happy wangu. Nikaamua nichukue simu ili nimpigie.
Uuuuufuuuuu!!!! Nilishusha pumzi za uchovu baada ya kuikosa simu yangu mifuko yote ya suruali.
Riziki nilichoka. Nilikumbuka mfuko wa wa zawadi za Happy niliouacha pale nilipomchukua majeruhi nao haukuepo najua walichauchukua "wajasiriachochote". Basi nilibaki natembea tembea nikirusha rusha mikono nisijue pa Kumpata Happy kwani namba zake za simu sikuwa nimezikariri kichwani. Sio kwamba sikutaka kuzikariri bali kichwa changu ni kigumu sana kukariri namba za simu. Hapo sikua na mawasiliano kabisa na Happy na sikujua hata simu imepotelea wapi.
  Baada ya kukaa na kutuliza kichwa majira kama ya saa kumi jioni nilinyanyuka chini ya mti niliokua nimekaa nikaamua niende hospitali kumtazama yule "Happy" majeruhi, bado sikujua kama hali yake itakuwaje maana alipoteza fahamu na alikua ameumia vibaya. Wakati najishauri Mara nilimwona Happy wangu akiwa anatembea kuelekea mwelekeo mwingine na hakua ameniona. Nilipata faraja kubwa na furaha ikanilipuka nikamkimbilia na nilipomkaribia nikamwita.

Happy..... Happy....
    Aligeuka nikitegemea angenipokea kwa kumbatio la nguvu. Oooigh nilikua mnyonge happy aliponigeukia kwa hasira kisha akaongea.
"Nenda kamwite  Valentine wako uliyempeleka hospitali". Loooh! Niliumia sana nikajaribu kumwelewesha lakini hakua ananielewa.
" Hivi Riziki we unajifanya msamaria saana kuliko wote, kama humfahamu kwanini usingewaacha wengine wampeleke hospitali hadi uwe wewe? Usinifanye mtoto Riziki".
Nilijaribu sana kumsihi happy mwishowe kwa shingo upande nilijaribu kumshawishi twende hospitali pengine tungemkuta mgonjwa na fahamu angeeleza ukweli au labda ndugu zake wengine wangenisaidia.
   Tulifika hospitali, tukawakuta wazazi wa happy ambao niliwatambua kwani walikua wanaelezewa na nesi niliyemkuta pale na nilipofika tu nesi alinigeukia sikujua aliongea nini, nami na Happy tukaamua kuwasogelea nilitaka kuwaeleza kuwa mimi ndiye niliyemleta hospitali. Kabla sijaongea akatokea daktari.
"Nyie ndio ndugu wa huyu msichana Happy Riziki?"
    Wazazi walitazamana lakini mimi niliitika nikatoa maelezo kwa wazazi kuwa niliandika lile jina sababu sikuwa namfahamu. Mpenzi wangu Happy alinikata jicho la hasira sana lakini tukatulia kusikiliza dokta anasema nini. Daktari alitueleza Mgonjwa aliumia vibaya sehemu ya kichwani na pia ubongo umeshtuka hivyo hata kama akipona atakuwa hana kumbukumbu au atapatwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu mara kwa mara. Baada ya maelezo nilitaka kuwaeleza wazazi wa binti ambae kumbe aliitwa Angella.
Lahaula!!! Happy wangu hakuwepo!!! Sikujua aliondoka saa ngapi. Niliamua kuwaaga wazazi ningerudi baadae nikaondoka nimtafute happy. Wakati natoka getini nilimkuta pembeni akinisubiri. Alikua na hasira kali, na alinipokea kwa maneno makali.
"Riziki sikujua kama ni mshenzi kiasi hiki, yaani kumbe unao happy wawili unatuchanganya utakavyo......" Happy alikunya mbovu kwa hasira aliniporomoshea maneno bila kunipa nafasi ya kujitetea.
"Kuanzia Leo sahau kabisa kama tuliwahi kuwa na uhusiano tena Leo hii nakuapia utajuta kahaba wa kiume" alinidhihaki sana akaniacha wapita njia wakinitazama wengine kwa huruma, wengine wakicheka wengine wasielewe, nikaondoka kwa aibu na majonzi kichwa chini kwenda kumalizia Valentine yangu chungu kwenye ghetto langu.

   Ni majira ya saa kumi na mbili jioni nikiwa naamka ili niende hospitali kumwona Angella aliyepata ajali ambaye nilimbatiza jina la happy ndipo nilikutana na happy akiwa na kaka yake waliokuja kishari. Niliwakaribisha ndani na nilipoingia tu mlango ulifungwa na nilipokea kipigo kitakatifu kutoka kwa kaka yake Happy. Nilijaribu kujitetea lakini sikuhimili. Nilipigwa nikapigika, nilichapwa nikachapika, waliondoka wakiniacha nyang'anyang'a. Nilibaki nikiifurahia Valentine kwa mtindo huo.

 Baada ya kupata ahueni angalau kidogo basi nilijiburuza nikajikusanya nitafute wapi kilipo kiberiti wapi jiko na wapi sufuria nichemshe angalao maji nikande majeraha yangu.
   Ni wakati nimemaliza kuwasha jiko langu la mkaa ndipo nilisikia gari likipaki nje kwa ghafla, kutahamaki waliingia polisi wawili na bunduki, kabla sijajua nini kinaendelea nilijikuta tayari nina pingu mkononi na vipigo vikitua tena kwenye mwili wangu. Nilitoneshwa upya maumivu niliyopata mwanzo kutoka kwa kaka yake Happy kisha waliniburuza na kunisokomeza kwenye gari yao tukaondoka kwenda kuendelea kusherehekea Valentine day kituoni. Jamani Valentine yangu mimi.
    Kufika kituoni maelezo niliyopata ni kuwa mimi ndiye niliyemgonga Angella na pikipiki kisha nikakimbia. Kumbe yule boda boda alieyemgonga Angella alitambulika kwa jina la Riziki na kumbe polisi walifika hospitali na kukuta jina langu niliyemleta pamoja na maelezo ya wazazi wa Angella na nesi aliyenipokea nikadhaniwa ni mimi. Kesi ikanivaa nikaendelea kusherehekea Valentine. Nikiwa kituoni sikuweza hata kutembea kwa maumivu, nikapelekwa hospitali nikiwa chini ya ulinzi. Baada ya vipimo nikagunduliwa nimevunjika mguu, nikabaki hospitali nikisherehekea valentine yangu.
    Polisi waliniambia nikipata ahueni nina kesi ya kujibu! Kesi ya kupakaziwa! Wema wangu umeniponza! Msaada wangu umekua shubiri! Nikaendelea kusherehekea Valentine!
Majira ya kama saa moja jioni alikuja rafiki yangu ambae nilikuwa nafanya nae kazi akanipa taarifa kwamba bosi amempigia simu akampa maagizo aniletee kwamba sipaswi tena kuonekana kazini! Jamani mimi! Nitaishije! Basi nikaendelea kusherehekea Valentine. Nilimtuma rafiki yangu aende akaweke ghetto langu sawa ambalo nililiacha hovyo anichukulie na visenti vya kunisaidia. Aliondoka akarudi baada ya muda, kumbe hakuruhusiwa kuingia chumbani kwangu. Baba mwenye nyumba alimkatalia, alikifunga chumba akinisubiri nije kuchukua vitu vyangu tu! Nikaendelea kusherehekea Valentine.
  Basi Valentine yangu ikaisha hivyo.
  Baada ya wiki siku nne niliruhusiwa kutoka pale hospitali lakini nilipelekwa moja kwa moja mahabusu kusubiri kesi inayonikabili. Nilikua sijapona ila nilipaswa kuwa narudi hospitali.
Nilikaa mahabusu miezi 6 bila ya kesi yangu kusomwa. Niliteseka sana. Tofauti na ndugu zangu waliokuwa wanakuja kuniona mpenzi wangu Happy hakutokea kabisa! Lakini bora hakutokea, alichonifanyia yeye na kaka yake nisingetamani kumwona. Yaani Happy wewe nakulaani kabisa, sitaki hata nikuone hata ukifa sitakuja kukuzika na hata mtu akinionesha kaburi lako kwa bahati mbaya nitalifuata na kulikojolea mwanaharamu kabisa. Wazazi wa Angella niliyempa msaada na Angella mwenyewe sikuwaona kabisa kwa kipindi chote wala sikupata habari yoyote kuwahusu.
Niliachiwa huru baada ya kukosekana kwa mashtaka dhidi yangu kwa kipindi chote nilichokua mahabusu. Nilitoka nikaingia uraiani, sina pa kuishi, sina hela, sina kazi, sina pa kupata chakula na sina mpenzi wangu Happy. Vyote vilipotea siku ile ya Valentine. Labda bado naisherehekea Valentine. Valentine day ina maana mbaya kwangu. Naichukia Valentine day. Iliniharibia kila kitu Riziki mimi.
Nakuruhusu upige stori zote na mimi lakini ukitaka kuvuruga amani we nitajie siku ya Valentine uone. Nakuhakikishia nitakuonesha hasira yangu. Hata kama sikumudu lazima nitafanya kitu ambacho utajua huwa nina hasira kiasi gani na siku ya Valentine. Naichukia sana, sipendi kabisa kuisikia Valentine day.
Jifunze:
Kuna watu wana historia ya kuumiza ambayo imewatokea kwa kipindi fulani. Inawezekana ni jambo la kuumiza sana ambalo ndani yake linaweza kumpa mtu maumivu au hasira kali. Kila mtu ana namna ya kukabili hasira na maumivu yake, huwezi kujua mtu alivyo unavyojitahidi aidha kumpa faraja au kumshauri pengine unamtonesha kidonda au unaamsha maumivu na hasira, basi njia sahihi ni kuepuka kabisa kulijadili na kubadili mada.

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post