NORA DAMIAN– DODOMA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaanza ngwe ya tatu ya kampeni katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini huku kikieleza namna kitakavyozitumia siku 30 zilizobaki kuomba ridhaa ya Watanzania ili waweze kukichagua tena.
Akizungumza jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema chama kimetoa maelekezo ya namna ya kuzitumia vyema siku 30 zilizobaki kwa kueleza maono ya chama na maono ya mgombea.
“Tunaanza kuhesabu siku 30 katika mzunguko wetu wa kampeni, mgombea atajikita katika maono ambayo Watanzania tumemwamini sambamba na maono ya kisera na kiilani katika muhula wake wa pili ambao anaomba ridhaa.
“Tunaye mgombea ambaye amepewa heshima na Watanzania, yeye mwenyewe ni mshika maono alipewa ilani mwaka 2015 ameitekeleza zaidi ya ilivyoandikwa. Kwa mfano kuna mambo 2015 – 2020 hayakuwemo kabisa lakini yamefanyika.
“Katika siku 30 zinazokuja Dk. Magufuli atajikita kueleza maono yake kwa Tanzania, corona haikuwepo kwenye ilani ya uchaguzi lakini maono yake akasema tumuombe Mungu, tusikilize Serikali, tuchape kazi…leo hakuna mtu ana barakoa, tumefunga vituo vyote vya corona.
“La pili ni maono ya Chama Cha Mapinduzi kisera yako ndani ya ilani, ni kubwa kuliko ilani ya 2015 – 2020 kwa sababu tumesema tusipuuze kauli za Watanzania, yale mambo mengi huenda yangefanyika katika miaka 20 tumesema tumjazie huyu John Pombe Magufuli…ndani ya miaka mitano hakutakuwa na muda wa kutosha wa kulala ndugu Magufuli,” alisema Polepole.
Aidha alisema katika siku hizo 30 wataeleza namna ambavyo wataibadilisha miji mbalimbali nchini kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Geita, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na mingine.
“Dodoma ndani ya miaka mitatu iliyopita haikuwa namna hii, Dar es Salaam mnafahamu ‘fly over’ ya Mfugale na ile ya Ubungo, tunatandika nyingine Banda la Ngozi inapopita Kawawa/ Nyerere road, kwahiyo utapita juu Tazara, makutano ya Kawawa na Nyerere road, halafu tunakwenda Kamata tunatandika nyingine.
“Maeneo ya Moroco, Mwenge, Tandika, tunataka barabara za lami tuzipeleke kila pahala kwenye miji midogo na mikubwa na taa kila pahala,” alisema Polepole.
INJINI MPYA
Polepole alisema pia wameandaa makada mbalimbali waandamizi ambao watatumika kufanya mashambulizi katika siku zilizobaki.
“Tunaye mjumbe wa kamati kuu na halmashauri kuu taifa, Majaliwa, makada waandamizi Mzee Pinda, Kikwete, Mwinyi, kuna waandamizi wengi wote tutawasambaza.
“Lakini ukishuka chini kwenye ngazi ya mikoa kuna wajumbe wa halmashauri kuu ya taifa, wenyeviti wa chama, tuna wagombea ubunge…kuna makada ambao wapo ‘stand bay’ na hawa wote ni injini tunaziteremsha katika siku hizi 30…kisiasa tunakwenda kumaliza,” alisema.
NYANDA ZA JUU KUSINI
Polepole alisema leo Dk. Magufuli ataendelea na kampeni katika Mkoa wa Iringa ambapo licha ya kusimama njiani pia atafanya mkutano mkuwa utakaofanyika katika uwanja wa Samora.
“Zimebaki siku 30 kabla ya siku ya mwisho ya kupiga kura tunaendelea kusisitiza tukaitumie tarehe 28 kupiga kura nyingi za kishindo kwa ndugu yetu John Pombe Magufuli na wagombea wote wa ubunge na udiwani ili ule utatu utimie mambo yaweze kwenda haraka bila mizengwe.
“Tanzania tumeimaliza yote kama ujenzi wa nyumba tuko kwenye ‘finishing’ tarehe 29 (kesho) ndugu yetu John Magufuli atakwenda Mbeya kupitia Njombe pale Makambako atasimama na njia yote atakuwa anafanya mikutano na wananchi. Septemba 30 tutakuwa na mkutano mkubwa Mbeya,” alisema Polepole.
KUJIBU MASHAMBULIZI
Polepole alisema wataendelea kujibu hoja mbalimbali zinazoibuliwa kwani wagombea wengi wa upinzani wamekuwa wakitumia uongo kama nyenzo ya kampeni.
Alisema taarifa zilizotolewa na mgombea mmoja wa upinzani kwamba wakurugenzi wa halmashauri wameitwa Dodoma ni uongo na kutaka mamlaka zinazohusika kuzitolea ufafanuzi.
“Huu ni uongo, ni uzushi, uzandiki ni fitina ya hali ya juu yenye lengo la kufitinisha watumishi wa serikali wenye dhamana ya kusimamia uchaguzi.
“Rai yetu ni kulitolea jambo hili ufafanuzi ili uongo ukathibitishwe, watu unaowaomba dhamana unatakiwa useme nao kwa unyenyekevu, Watanzania tumpuuze
“Wana CCM na viongozi wale ambao wanasimamia uchaguzi wasiache uongo ukabaki kwenye maeneo yao, tuna utaratibu wetu wa ndani wa kuhabarishana hilo linaendelea kwenye ngazi za kata, majimbo Tanzania Bara na Zanzibar….sasa hivi hata kuzungumza na wanahabari kufafanua haya mambo itakuwa kwa wingi zaidi,” alisema Polepole.
KUSHAMBULIWA MAKADA
Chama hicho pia kililaani kauli za kichochezi na vitendo vya kuwashambulia makada wake na kulitaka Jeshi la Polisi likamilishe upelelezi haraka na kuwachukulia hatua wahusika.
Kwa mujibu wa Polepole vitendo hivyo vinahusisha kuuawa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Seneti ya Vyuo Vikuu Mkoa wa Iringa, kushambuliwa kwa kupigwa risasi kada wao aliyetokea upinzani, kufyekwa kwa mazao ya makada wao na kushambuliwa kwa mapanga baadhi ya makada wao Zanzibar.
“Tumeumizwa sana tumekaa kimya muda mrefu imetosha, kijana huyu (Mwenyekiti wa UVCCM Seneti ya Vyuo Vikuu Mkoa wa Iringa) alikuwa na ndoto yake, angekuwa kiongozi mzuri katika nchi yetu, maisha yake yamekatizwa.
“Songwe wako madiwani wanahamia CCM mazao yao shambani yamekatwakatwa eka kwa eka, mmoja amejenga hoja wale wamechukizwa amepigwa risasi zinakaribia 30 Mungu amelinda uhai wake.
“Mwingine anawaambia wanachama wachukue mapanga, mundu, mawe siku chache baadaye watu wanapigwa mapanga msikitini.
“Hatupendi kuchukua sheria mkononi tunaamini sheria tulizojiwekea, chama chetu msingi wake ni utu, tunalitaka Jeshi la Polisi tafadhali sana haya matukio hayapaswi kuendelea, ushahidi upo wahusika wakamatwe…hatuko tayari kufanya siasa katika nchi hii tunamwaga damu na kupoteza maisha ya Watanzania,” alisema Polepole.
from Author
Post a Comment