HOSPITALI ya rufaa ya Haydom Mkoani Manyara, imezidi kuboresha miundombinu yake kwa kuongeza majengo na kununua vifaa tiba vya thamani ya sh1 bilioni hivyo kuzidi kufanikisha kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya rufaa ya Kanda.
Hospitali hiyo hutoa huduma kwa wananchi wa wilaya za Babati, Hanang' na Mbulu za mkoani Manyara, wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Mkalama na Iramba mkoani Singida, Meatu mkoani Simiyu na Igunga mkoani Tabora.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya Haydom, Dk Paschal Mdoe akizungumza jana kwenye uzinduzi wa majengo na vifaa hivyo alisema hospital hiyo ina nyota nne za ubora wa huduma na nyota tatu za ubora wa maabara.
Dk Mdoe alisema jengo la kusafisha figo na mashine saba imejengwa na wadau wao African health Network na wanasubiria kibali cha Wizara ya Afya ili ianze kutoa huduma.
Alisema jengo la maabara (microbiology) wamelikarabati kwa fedha zao za ndani kwa sehemu na fedha toka serikali ya Norway kupitia shirika la Kikristo la misaada Norway (NCA).
"Vitanda 20, magodoro 20, makabati 20 na viti matairi saba ukiwa ni msaada wa rafiki yetu Magna maarufu kama fundi bomba, vya thamani ya sh100 milioni, alivinunua Norway na kuzisafirisha hadi Haydom," alisema Dk Mdoe.
Alisema mashine ya kuwapea wagonjwa dawa za nusu kaputi (Anaesthesia mashine) ya sh45 milioni, mashine ya uchunguzi wa magonjwa ya mfumo wa chakula, haja kubwa na njia ya hewa (Endoscope) ni msaada wa Profesa Levente Diosady na Lorne Heuckrof na mkewe Joyce wa Canada.
Alisema matengenezo na ufungaji wa mashine ya mishipa (Intavenous fluid) umegharimu sh100 milioni na kufadhiliwa na serikali ya Norway kupitia NCA na GE Healthcare ya Norway.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mbulu, Nicholaus Nsangazelu alisema hospital hiyo ina zaidi ya miaka 60 katika kutoa huduma kwa jamii.
Askofu Nsangazelu alitoa wito kwa viongozi wa serikali kuhakikisha wanafanikisha hospitali hiyo kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya rufaa ngazi ya kanda.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga alisema serikali imefanikisha kujenga hospitali ya wilaya na vituo vya afya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa hospitali ya Haydom.
Kamoga alisema wataendelea kusukuma mbele hatua ya hospitali ya rufaa ya Haydom kutangazwa kuwa ya rufaa ngazi ya kanda.
Mkazi wa eneo la Haydom, James Gitonge aliipongeza hospitali hiyo kwa namna inavyotoa huduma kwa jamii.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya rufaa ya Haydom Mkoani Manyara, Dokta Paschal Mdoe akisoma taarifa ya gharama za majengo na vifaa tiba vipya vilivyonunuliwa hivi karibuni
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara, Hudson Starnley Kamoga akizungumza kwa niaba ya Serikali kwenye uzinduzi wa majengo na vifaa tiba kwenye hospitali ya rufaa ya Haydom.
Baadhi ya wauguzi wa Hospitali ya Haydom Mkoani Manyara, wakionyesha namna wanavyotoa huduma kwa watoto.
Askofu wa Dayosisi ya Mbulu Nicholaus Nzangazelu akizungumza wakati alipobariki majengo na vifaa tiba vipya vilivyonunuliwa hivi karibuni vya hospitali ya rufaa ya Haydom.
By Mpekuzi
Post a Comment