Lukuvi Awashukia Wanasiasa Wanaotuhumu Viongozi Kupora Ardhi |Shamteeblog.


 Na Munir Shemweta,  WANMM IRINGA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekanusha vikali kauli iliyotolewa na baadhi  ya viongozi wa vyama vya siasa kuwa kuna baadhi ya viongozi wamepora ardhi ikiwemo ardhi ya eneo la Mbarari mkoa wa Mbeya na kusisitiza kuwa kati ya viongozi waliotuhumiwa hakuna hata kiongozi mmoja  aliyepora ardhi.


Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema umilikishaji ardhi nchini unafuata sheria na serikali haina ubaguzi katika kumilikisha mtu yeyoye ardhi huku akiweka wazi kuwa  umilikishaji ardhi kwa mtu yeyote hauna kikomo.


Lukuvi amekanusha uvumi huo jana  alipokutana na waandishi wa habari mkoani Iringa akitolea ufafanuzi wa  baadhi ya kauli zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa vyama vya siasa  wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, 2020.


“Serikali ya awamu ya tano haina ubaguzi wa kumilikisha ardhi na mwananchi yeyote bila kujali itikadi ya chama cha siasa anaweza kumilikishwa” alifafanua Lukuvi.


Kwa mujibu wa Lukuvi,  Seriali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kushughulikia masuala ya ardhi ikiwemo lile la kuvibakisha vijiji 920 kati ya  975 vilivyokuwa kwenye hifadhi na kubainisha kuwa, serikali inaangalia namna ya kuvibakisha vijiji vingine 55 vilivyosalia.


Akitolea ufafanuzi suala la Mbarari, Lukuvi alisema wananchi wanaoishi katika vijiji  29 eneo la Mbarari  wameamuriwa kubaki eneo hilo ingawa kwa mujibu wa GN Namba 28 ya mwaka 2008 walitakiwa kuondoka lakini kwa huruma ya Rais John Pombe Magufuli alibatilisha uamuzi huo  na kuagiza vijiji visiondolewe.


“Wananchi wa Mbarari waendelee kuishi kama wanavyoendelea, Mgogoro wa Mbarari ni wa muda mrefu tangu mwaka 2008 na serikali ya awamu ya tano haipaswi  kulaumiwa na Rais Magufuli siyo mtu wa kubeza kwa kuwa vijiji vilitakiwa kuondolewa lakini aliamuru vibaki” alisema Lukuvi.


Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, baada ya uamuzi wa kutoviondoa vijiji 920 kati ya 975 hatua  inayofuata ni kupima upya mipaka sambamba na  kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kubainisha matumizi ya maeneo ya maeneo husika.


Vile vile, Lukuvi alisema serikali katika kuwajali wananchi imeamua pia  kufuta mapori tengefu 12 yenye zaidi ya hekta 707,659.4  sambamba na kumega hifadhi 14 za misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.


Waziri wa Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, serikali ya awamu ya tano imeendelea kuchukua hatua za kupunguza na kufuta mashamba makubwa kwa wamiliki waliokiuka masharti ya umiliki na kubainisha kuwa, kwa sasa serikali imeshafuta mashamba yasiyopungua 49 na kugawiwa kwa wananchi.


Akigeukia tatizo la ardhi katika mkoa wa Morogoro, Waziri Lukuvi amesema kazi ya uhakiki mashamba 11 katika eneo la Kilosa  imekamilika na muda ukiruhusu watatangaziwa mashamba yaliyofutwa kutokana na wamiliki wake kukiuka masharti ya umiliki.


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alihitimisha mkutano wake na waandishi wa habari kwa kutoa onyo kwa wananchi wote waliomilikishwa ardhi kuhakikisha wanafuata sheria na kusisitiza kuwa, sheria za ardhi zimewekwa ili kutekelezwa na wasiozifuta watafutiwa umiliki na kupatiwa watu wengine.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post