Majaliwa aahidi kivuko kisiwa cha Gana Ukerewe |Shamteeblog.

Na CLARA MATIMO-Ukerewe

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kutoa kivuko kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo Kata ya Ilangala, wilayani Ukerewe.

Ahadi hiyo imetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kitongoji cha Gana.

Katika mkutano huo, Majaliwa alimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Ukerewe kupitia tiketi ya CCM, Joseph Mkundi na madiwani. 

Pia Majaliwa aliwataka wananchi wa Gana wamchague mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao wa urais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Akitoa ahadi hiyo mbele ya wananchi wa Kisiwa cha Gana, Majaliwa alisema uamuzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 yenye kurasa 303. Kivuko hicho kitatoa huduma kati ya Kakuru na Gana.

Alisema ilani ya CCM imetoa maelekezo kwa Serikali ijayo itekeleze idadi kubwa ya miradi ya kimkakati ikiwemo kuboresha usafiri wa majini ili kuwandolea adha wananchi wanaoishi katika maeneo ya visiwani.

Majaliwa alisema wananchi zaidi ya 3,000 wa Gana, wanahitaji kivuko bora ambacho kitatoa fursa kwao kufanya shughuli za uvuvi na biashara ili kujipatia kipato.

“Hapa Gana tutaleta kivuko, hiki kisiwa ni kikubwa kina idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji huduma bora ya usafiri wa majini. Serikali yenu imeweka mipango mizuri kwa ajili yenu,” alisema Mheshimiwa Majaliwa.

Alisema chama kitaendelea kutekeleza ilani yake kwa vitendo kwa kuboresha huduma za wananchi katika visiwa vyote nchini ikiwemo wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza yenye visiwa 38.

Mbali na kutoa ahadi ya kivuko, Majaliwa alisema Serikali ijayo itapeleka boti za doria kulinda usalama wa wavuvi ambao wakati mwingine wanafanya shughuli zao kwa mashaka wakihofia uvamizi wa majambazi wanaotoka nchi jirani.

Katika hatua nyingine, alisema chama hicho kitahakikisha wananchi wa kisiwa hicho wanapata umeme.

 “Mkakati wetu ni kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata umeme, Ukerewe vijiji 70 tayari vina umeme vimebaki sita ambavyo vitapitiwa na mradi,” alisema Majaliwa.

Alisema asilimia 80 ya vijiji nchini vimepata umeme baada ya Serikali ya awamu ya tano kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020. 

“Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuendeleza na kuimarisha sekta ya nishati ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali. Mpango wa Serikali ni kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote na maeneo ya pembezoni mwa miji,”

Majaliwa alisema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imepata mafanikio kwa kuzalisha umeme kutoka megawati 1,308 mwaka 2015 hadi 1,602 mwaka 2020 ongezeko ambalo limeifanya nchi kujitosheleza kwa mahitaji ya umeme.

Upatikanaji wa umeme kwa jumla Tanzania Bara umeongezeka kutoka asilimia 36 mwaka 2015 hadi asilimia 70. Ujenzi wa miradi umepunguza gharama za kuunganisha umeme vijijini kutoka wastani wa sh. 454,000 hadi 27,000.



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post