LAGOS, NIGERIA
VIWANJA vya ndege nchini Nigeria huenda vikafungwa siku ya Jumatatu huku vyama vinne vikuu vya wafanyakazi vikisema kuwa vitajiungana na mgomo wa kitaifa kulalamika kuhusu ongezeko la bei ya mafuta na gharama ya umeme.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa siku ya Alhamisi ya vyama vinne vya wafanyakazi vinavyowaakilisha marubani, wahandisi na waatalamu wengine wa usafiri wa anga, imesema kuwa vinaunga mkono kikamilifu mgomo huo ulioitishwa na Muungano wa wafanyakazi wa Nigeria unaowaakilisha mamilioni ya wafanyikazi katika karibu sekta zote za taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.
Msemaji wa wizara ya usafiri wa anga amesema kuwa mazungumzo yanafanyika katika kiwango cha juu na kwamba viongozi wa vyama hivyo vya wafanyakazi walikutana jana na mawaziri wa kazi, mafuta na kazi katika makao ya rais lakini hakuna makubaliano yoyote yalioafikiwa.
Wakati huo huo, shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM limeripoti kuwa wahamiaji wasiopunguwa 16 waliokuwa wakijaribu kwenda barani Ulaya wamezama katika bahari ya Mediterenia wakati mashua yao ndogo ilipopinduka karibu na pwani ya Libya.
Hii ni ajali ya hivi karibuni ya meli inayodhihirisha hatari zinazowakabili wale wanaokimbia kutoka nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika inayoathiriwa na vita.
IOM imesema kuwa wavuvi wa Libya waliona mashua hiyo iliyozama siku ya Alhamisi jioni na kuweza kuvuta miili 22 kutoka majini ikijumuisha ile ya wahamiaji kutoka Misri, Bangladesh, Syria, Somalia na Ghana. Walinzi wa Pwani ya Libya wamesema kwamba waliamuru shughuli hiyo ya uokoaji na kuonya kwamba huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka huku shughuli ya kutafuta miili mingine ikiendelezwa katika eneo hilo.
Rais wa Poland asema wahamiaji wanapaswa kuishi karibu na nchi zao
Rais wa Poland Andrzej Duda amesema kuwa wahamiaji wanaotoroka ghasia wanapaswa kuishi katika maeneo ya karibu na mataifa yao na kukosoa mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho kwa sheria za uhamiaji na ukimbizi za Umoja wa Ulaya.
Duda ameliambia shirika la habari la umma nchini humo TVP info kwamba kwa ajili ya nchi hizo ambazo watu hawa wametoroka vita kwa sasa, wanahitaji kuwa karibu na mipaka ikiwezekana ili kuwa na ari kubwa ya kurejea katika nchi hizo na kuzijenga upya.
Duda alikosoa mapendekezo ya Umoja wa Ulaya kugawanya wahamiaji hao miongoni mwa mataifa ya Umoja huo na kusema Poland ilipinga kulazimishwa kuwapokea wahamiaji na wahamiaji hao kukosa uwezo wa kujichagulia wanakotaka kwenda. Mapendekezo hayo yatalazimisha kisheria nchi zote washirika wa Umoja huo kupokea kiasi chao cha wakimbizi ili kuweza kupata ufadhili kutoka kwa bajeti ya Umoja huo.
from Author
Post a Comment