CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kujenga kituo cha afya kata ya Irugwa, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza ili kuwaondolea wananchi wa kisiwa hicho adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Hayo yamesemwa leo (Ijumaa, Septemba 25, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Mheshimiwa Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa kisiwa hicho kwenye mkutano wa kampeni.
Uamuzi huo unaenda sambamba na ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 kwenye uk. 186 inayosema: “Hadi kufikia 2025 Serikali itaongeza vituo vya kutolea huduma za afya kwa asilimia 20 ya vituo 8,446 vilivyopo sasa; vipaumbele vitawekwa katika ujenzi wa vituo vya afya na ukamilishwaji wa maboma kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia, idadi ya watu na wingi wa magonjwa.”
Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa Serikali ilishatoa shilingi milioni 49.2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo moja la kujifungulia katika zahanati ya Irugwa.
Kuhusu maji Mheshimiwa Majaliwa amesema Ilani ya CCM imeweka mipango imara ya kushughulikia upatikanaji wa maji vijijini, kama hatua ya kutekeleza azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani.
Akizungumzia usafiri wa majini kwa wakazi wa eneo hilo, Mheshimiwa Majaliwa amesema, Serikali ya CCM ikiingia madarakani inakusudia kujenga vivuko mbalimbali kikiwemo kivuko cha Irugwa, Murtanga, Gana, Kakakuru na Lugezi hadi Kisorya.
Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (uk.83-84), Chama cha Mapinduzi kimeielekeza Serikali ikamilishe ujenzi wa vivuko vipya nane kikiwemo cha Irugwa – Murutanga (Ukerewe).
Pia Ilani hiyo imeelekeza Serikali ianze kutekeleza mradi wa ujenzi wa maegesho ya Rugezi – Kisorya (Mwanza), Kome na Nyakalilo (Mwanza), Utete (Pwani), Chato – Nkome (Geita), Iramba na Majita (Mwanza), Irugwa (Ukerewe – Mwanza).
Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi amesema kivuko cha Irugwa kitakua mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo ambao watoto wao hawajawahi kuona gari ikipita katika kisiwa hicho kutokana na ukosefu wa kivuko.
By Mpekuzi
Post a Comment