Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa wilayani Hanang mkoa wa Manyara imemuamuru Mzabuni Ayubu Iyaka aliyepewa kazi ya kutengeneza na kupachika milango kwenye jengo la kituo cha Afya cha Hirbadaw, kuondoa milango yote 83 aliyoweka kwenye kituo hicho baada ya kubainika haina Ubora.
Takukuru imebaini hayo baada ya maafisa wake kufanya ukaguzi kwenye kituo hicho ambapo aliingia mkataba na Halmashauri hiyo kutengeneza na kupachika milango 83 yenye ubora iliyotengenezwa kwa kutumia mbao ngumu kwa gharama ya shilingi Milioni 28,000,000.
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu Septemba 24,2020, amesema wamejiridhisha kuwa kwa makusudi Mzabuni huyo aliamua kukiuka mkataba akatengeneza na kuweka kwenye jengo hilo la Kituo cha Afya milango hiyo isiyokuwa na ubora.
Pamoja na hayo amesema Halmashauri ilishamlipa shilingi Milioni 14,000,000 ambazo ni nusu ya fedha walizoingia mkataba.
Makungu amesema milango hiyo ambayo inadaiwa kuwa ni mipya, imeonekana ikiwa imepasuka,mingine imepinda na kuvunjika kabla ya kituo kuanza kutumika.
Amesema kufuatia hayo Takukuru wilayani Hanang, imemuamuru Mzabuni huyo kuondoa milango yote 83 na kutengeneza mingine yenye ubora unaokubalika katika majengo ya serikali na kwa mujibu wa mkataba alioingia na Halmashauri, na kwamba ataruhusiwa kuweka milango hiyo baada ya kukaguliwa na kujiridhisha kama ubora wake umekidhi vigezo.
Takukuru imewaasa Wazabuni wanaopenda kufanya kazi na serikali kuwa waadilifu na kuzingatia mikataba ya kazi, huku ikitoa rai kwa watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kusimamia miradi ya Umma kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha miradi inatekelezwa katika ubora unaokubalika.
By Mpekuzi
Post a Comment