Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amemaliza ziara yake mkoa wa Mara na kuwaeleza wananchi kwamba tarehe 28 Oktoba, 2020 siyo siku ya mzaha.
“Tarehe 28 Oktoba, 2020 siyo siyo ya mzaha na wala siyo siku ya majaribio. Ni siku ya kuchagua Kiongozi atakayetufaa, na huyo si mwingine bali Dkt. John Pombe Magufuli, ” amesema.
Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumanne, Septemba 22, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Kibara, wilayani Bunda, mkoani Mara kwenye mkutano wa kuwanadi wagombea wa CCM uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Kibara.
Amesema kiongozi wa nchi anayefaa kuchaguliwa ni yule anayeweza kusimamia rasilmali za Taifa. “Ni yule anayeweza kusimamia tunu za Taifa… siyo mnapata kiongozi halafu akipewa nchi anabadilisha hadi wimbo wa Taifa.”
“Tunahitaji kiongozi anayeweza kupambana na rushwa, awe mtu wa kutetea watu wake wapate haki bila kuombwa rushwa. Huyo si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Magufuli,” amesema.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la kuwaombea kura Charles Kajege na diwani wa Kibara, Bw. Nyanguli Mtesigwa na madiwani wengine wa jimbo hilo. Jioni hii anaingia mkoa wa Mwanza.
Akielezea umuhimu wa chama kuwa na Ilani ya Uchaguzi, Mheshimiwa Majaliwa amesema Chama cha Mapinduzi kimeandaa ilani yake yenye kurasa 303 ikisimamia yale yaliyokuwemo kwenye ilani iliyopita ambayo ilikuwa na kurasa 236 na mengine mengi mapya.
“Watekelezaji wa hayo yote yaliyoainishwa kwenye Ilani ni hawa watatu ambao nawaombea kura leo. Namwombea kura Dkt. Magufuli ili akamilishe aliyoyaanza na atekeleze yaliyomo kwenye Ilani ya sasa. Ni lazima tumpatie mbunge na diwani wa CCM ili waweze kuzungumza lugha moja.”
Kuhusu uboreshaji kwenye sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema zilitumika sh. bilioni 1.8 za kujenga hospitali ya wilaya hiyo na bado kuna sh. milioni 152 zilitolewa ili kuisaidia Halmashauri kujenga zahanati.
Kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 6.2 zimetumika kukarabati na ujenzi wa miradi mbalimbali kwenye Halmashauri ya wilayani Bunda, ikiwemo uchimbaji wa visima virefu na vifupi, utengenezaji wa matenki ya kuvuna maji na uchimbaji wa mabwawa.
“Vijiji vilivyonufaika na miradi hii ni Nyatwali, Nyamuswa, Mgeta –Nyang’aranga, kinyabwiga, Bulamba na Kibara. Pia jumla ya shilingi milioni 90.1 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na usafishaji wa pampu za mkono 67 na visima vitatu,” amesema.
Mapema asubuhi, akiwa kata ya Kisorya, Mheshimiwa Majaliwa aliwaeleza wananchi hao kwamba Serikali ya CCM ina mpango wa kuboresha kituo chao cha afya kwa kuongeza wodi tatu za wanawake, wanaume na watoto.
Pia alisema zimetengwa sh. milioni 550 za kuimarisha kituo hicho kwa kuongeza majengo ya jiko, chumba cha kufulia na chumba cha kuhifadhia maiti.
Kuhusu barabara, amesema kiasi cha sh. bilioni 2.9 kimetumika kutengeneza barabara za kuunganisha vijiji kwa vijiji, kukarabati sehemu korofi zilizoharibiwa na mafuriko, madaraja, makalvati na matengenezo ya kawaida.
Kuhusu umeme, amesema vijiji 77 kati ya 78 vina umeme isipokuwa kijiji kimoja tu cha Nafubu kilichopo kisiwani, ambacho amesema watapelekewa huduma ya umeme wa jua kwa vile siyo rahisi kupitisha nyaya za umeme majini.
By Author
Post a Comment