UNCDF yazindua ripoti ya uwekezaji kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya jamii |Shamteeblog.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa mitaji ya Maendeleo (UNCDF), limezindua ripoti inayoonyesha namna lilivyowekeza katika miradi ya maendeleo endelevu katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Shirika hilo limesaidia kufanikisha utekelezaji wa miradi yenye thamani zaidi ya dola za kimarekani, milioni 50.6 katika sekta za nishati endelevu, uwezeshaji wa wanawake na vijana kiuchumi, uboreshaji wa mnyororo wa thamani kwenye kilimo, kuhimili mabadiliko ya tabia nchi na miundombinu ya utoaji huduma za kijamii.

Aidha, ripoti hiyo imesheheni taarifa za kina juu ya mafunzo na mafanikio ambayo walengwa na wadau wa UNCDF wameweza kunufaika kupitia programu ya Mpango wa uwezeshaji wa fedha za ndani[Local Finance Initiative] (LFI) kuanzia mwaka 2017 hadi 2019 kwa kushirikiana na wizara na taasisi za serikali, washirika wa maendeleo, mamlaka za serikali za mitaa na sekta binafsi katika kutatua changamoto kubwa za maendeleo zinazozikumba nchi zinazoendelea.

Mafanikio ya Tanzania kuingia kwenye orodha ya nchi zenye uchumi wa kati yamechochea mijadala kuhusiana na maendeleo endelevu na ukuaji jumuishi. Ripoti hiyo imedokeza mbinu zilizotumika katika kuchangia kuleta mabadiliko ya uchumi wa ndani kwenye nchi washirika ikiwa ni sehemu mahususi ya maendeleo endelevu. Hivyo, uzoefu wa UNCDF unatazamwa kama chombo cha maarifa’ kwa ajili ya mabadiliko ya uwekezaji wa ndani na utekelezaji wa mbinu suluhishi za maendeleo.

Tukio hilo liliwaleta pamoja maafisa wakuu serikali na Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa na kutoa fursa ya kipekee kwa washirika, wadau, na vyombo vya habari kusikia juu ya juhudi za UNCDF katika kutekeleza programu zake zilizolenga kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDG) yanafikiwa nchini Tanzania pamoja na mataifa mengine yanayoendelea.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dr Charles Mhina, alisema kuwa, “serikali inatambua mchango wa UNCDF katika kujenga uwezo wa halmashauri kwa kushirikiana nao kubuni na kutekeleza miradi ya kimkakati ya uzalishaji ili kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato yatakayosaidia kukidhi mahitaji ya kimaendeleo”.

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Bw. Zlatan Milisic aliongeza kuwa, Umoja wa Mataifa (UN) unashirikiana na serikali ili kufikia vipaumbele vyake pamoja na malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Mkuu wa UNCDF nchini Tanzania, Bwana Peter Malika, aliishukuru serikali, Umoja wa Mataifa na washirika wa maendeleo kwa mchango na ushiriki wao ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

“Ili kukabiliana na changamoto za wakati huu, tunafanya kazi na taasisisi za umma na sekta binafsi kujenga mnyororo wa thamani ambao utachangia katika kutengeneza ajira, ujasiriamali na fursa za kibiashara – jambo ambalo litaleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii”. alisema.

Aidha, Bwana Malika alisisitiza kuwa jitihada za kuendeleza uchumi zinapaswa kuzingatia matumizi ya rasilimali yenye tija na uwezo wa kitaasisi katika kuleta mabadiliko ya uchumi jumuishi.

 



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post