Wataalam wa uhasibu wa Afrika Mashariki waonyesha njia za kufufua uchumi baada ya janga la virusi vya Corona |Shamteeblog.

Dar es Salaam. Wahasibu waandamizi wamezitaka nchi za Africa Mashariki kufanya mambo kadhaa ili kufufua uchumi wa nchi zao ulioathirika kutokana na athari za virusi vya Corona.

Wakizungumza katika mkutano wa Chama cha Wahasibu Ulimwenguni (the Association of Chartered Certified Accountants – ACCA), wataalam hao wamezitaka nchi za Afrika Mashariki kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa mapambano ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Mkuu wa ACCA Tanzania, Bw. Jenard Lazaro alisema mkutano huo uliandaliwa kwa kushirikiana na bodi za wahasibu za nchi za Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) Tanzania.

Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania, NBAA ni mshirika wa kimkakati wa muda mrefu wa ACCA.

Alishukuru na kutambua mchango wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) Tanzania, akisema umekuwa ni wenye umuhimu mkubwa katika kufanikisha malengo ya mkutano huu ukizingatia umuhimu wa kuangalia athari za Covid-19 katika biashara na fedha na majibu kutoka kwa taasisi na mashirika mbali mbali ya Afrika Mashariki.

“Ni katika hatua hii ambapo mbinu na mikakati ya biashara hubadilika na hivyo kutuhitaji kuelewa mabadiliko haya ili kuihudumia vyema Tanzania,” alisema Bw. Lazaro.

Wataalam wanazitaka nchi za Afrika Mashariki kusisitiza uwekezaji katika teknolojia, sambamba na kukumbatia utendaji kazi kidijitali. Uwepo wa ushirikiano thabiti kati ya sekta binafsi na sekta ya umma pia utasaidia nchi hizo kujikwamua na athari za kiuchumi za Covid-19 kwa haraka zaidi. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Bw. Sanjay Rughani alisema ugonjwa wa Covid-19 umebadilisha jinsi biashara zinavyofanyika na kuzilazimu biashara kupitisha matumizi ya teknolojia. Kinachohitajika ni kuhakikisha kuwa sasa biashara zinatumia vyema mabadiliko hayo mapya ili yaweze kuleta manufaa zaidi.

“Ugonjwa umeleta mabadiliko ya kiumahiri katika tabia na kutufanya tuwe watu wanaoweza kubadilika, kudadisi na wabunifu. Haya yote ni muhimu sana katika kuufufua uchumi kutokana na athari hasi za janga la Corona,” alisema Bw. Rughani.

Alizitaka kampuni kuboresha mawasiliano yake na kuweza kuwavutia wadau wake wa biashara.

Hii itasadia kujenga upya kuaminika kwa makampuni miongoni mwa wadau wake muhimu. Hali hiyo pia italeta mtangamano mpya kati ya biashara na wadau wake na hatimaye, uchumi utafufuka.

Japo anakiri kuwa Tanzania ilichukua mbinu sahihi katika kupambana na janga la Corona, Bw. Rughani anasema hali hiyo imechangiwa pia na kuwepo kwa mshikamano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Hata hivyo, alisema ni dhahiri kuwa uchumi umeathirika katika sekta za Utalii, Mauzo ya Nje, Uwekezaji wa Moja kwa Moja kutoka Nje na Pesa zinazotumwa nchini kutoka nje ya nchi. 

“Kwa vile dunia nzima ilipata mafua, uchumi wa Tanzania nao ulipiga chafya,” alisema na kuyataka makampuni kufanya mabadiliko ili kuendana na hali ya kufufua uchumi kama inayohitajika.

Mshirika na mkuu wa kitengo cha ushauri wa kampuni ya KPMG East Africa, Bw. Brian DeSouza alizitaka kampuni kuangalia zaidi teknolojia mpya ya wingu (cloud technology) ili kuweza kujiweka katika hali ya kufufuka kiurahisi kutokana na athari hasi za ugonjwa wa Covid-19.


Naye mjumbe wa Baraza la Uongozi na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) Tanzania, Dk. Neema Kiure-Mssusa alisema wepesi wa kubadilika ndiyo utakaoziwezesha nchi za Afrika Mashariki kufufuka kwa haraka kutokana na athari hasi za janga la Covid-19.

Aliwataka wahasibu kuangalia jinsi ya kuboresha mikakati yao katika teknolojia na haswa kuchochea uwekezaji katika programu za kompyuta kwa faida pana ya biashara.

“Tunapoanzisha mikakati ya teknolojia, hatuna budi kuangalia mahitaji halisi ya huko tuendako na matarajio ya biashara zenyewe na wateja wake,” alisema Dk. Mssusa.

Naye mhasibu mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Mipango na Uchumi ya Uganda, Bw. Lawrence Semakula alisema muda umewadia kwa serikali za Afrika Mashariki kubadili mtazamo kutoka katika mapambano ya virusi vya Corona na kwa kuwekeza katika kuufufua uchumi.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kufufuka rasmi kwa uchumi huenda kukawa ni kwa hatua kwa hatua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ACCA wa Africa, Bw. Jamil Ampomah alisema ni wakati muafaka kwa viongozi wa nchi kuja na mikakati itakayotoa suluhisho la kudumu ili kuondokana na changamoto za kiuchumi zilizotokana na Janga la ugonjwa wa Covid-19. 

“Utafiti uliofanywa na ACCA mwezi Juni unaonyesha kuwa biashara zimeathirika kwa kiasi kikubwa na janga la Covid-19 ambapo kwa Tanzania, asilimia 51 ya walio shiriki katika utafiti walisema wateja wameacha au kupunguza manunuzi ya bidhaa zao,” alisema Mkuu wa kitengo cha ACCA cha usimamizi na ufahamu wa jinsi ya kuendesha biashara kitaalam na pia mwandishi wa ripoti ya Covid-19: The road to recovery, Bw. Jamie Lyon.

Mwisho



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post