Watu 150 wachunguzwa afya ya moyo Temeke |Shamteeblog.

Jumla ya watu 150 wamejitokeza na kufanyiwa uchunguzi na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), watu 37 kati ya hao wamekutwa na shinikizo la damu, 19 walikuwa hawajijui hali zao hapo kabla.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Samweli Rweyemamu alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari alipokuwa akieleeza tathmini kuhusu huduma ya uchunguzi na tiba waliyoitoa kwa wakazi wa Temeke, Septemba 18 na 23, mwaka huu, Viwanja vya Mwembe Yanga na Zakheem, kwenye Jukwaa la One Stop Jawabu.

“Mwamko na mwitiko wa wananchi umekuwa mkubwa, juzi kule Zakheem tuliona watu 103, pamoja na leo jumla tumeona watu 253, tumepima kisukari, uzito, shinikizo la damu na moyo kwa kutumia mashine ya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG) na kutoa dawa kwa watu tuliowakuta na matatizo ya moyo,” alibainisha.

Dk. Rweyemamu alisema miongoni mwa watu hao walikuwepo wanawake, wanaume, watu wazima, vijana na watoto.

“Wawili tumewakuta tayari moyo umetanuka, mmoja ni binti mwenye umri wa miaka 18, tunahisi alipata maambukizi ya bakteria ambayo baadae inaleta athari ya moyo kutanuka, tumempa rufaa kuja JKCI kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

Alisema watu watatu kati ya hao waliowachunguza wamekutwa wana kisukari hali ambayo baadaye inaweza kuwaletea shida ya shinikizo la damu na kuathiri afya ya moyo kwa ujumla.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post