Na SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM
YANGA inashuka dimbani leo, kukabiliana na Mtibwa Sugar, katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara, litakalopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Yanga itaikabili Mtibwa, ikitoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar, katika mchezo wa ligi hiyo uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.
Kwa upande mwingine, Mtibwa itaikabili Yanga ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata ushindi ugenini ilipoichapa Ihefu bao 1-0, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Timu hizo zilipokutana msimu uliopita wa ligi hiyo, mchezo wa mzunguko wa kwanza ulipigwa Uwanja wa Mkapa, ambapo Yanga ilishinda bao 1-0.
Zilipokutana mzunguko wa pili Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, dakika 90 zilikamilika kwa sare ya bao 1-1.
Zinapokutana leo, Yanga tayari imevuna pointi saba, baada ya kushuka dimbani mara tatu na kushinda michezo miwili na sare moja.
Licha ya ushindi wake dhidi ya Kagera, Yanga ilivuna pointi tatu baada ya kuichapa Mbeya City bao 1-0, Uwanja wa Mkapa, lakini kabla ya hapo ilizindua msimu kwa sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons kwenye uwanja huo huo.
Mtibwa kuelekea mchezo wa leo, imefanikiwa kuvuna pointi pointi tano, ilizozipata kupitia michezo yake mitatu iliyoshuka dimbani, ikishinda mmoja na sare mbili.
Ukiondoka ushindi wake dhidi ya Ihefu, Mtibwa ilikata utepe wa Ligi Kuu msimu huu kwa suluhu dhidi ya Ruvu Shooting kabla ya kupata sare ya bao 1-1 na Simba, Uwanja wa Jamhuri.
Kwa kuzingatia matokeo ya timu hizo kwenye michezo yao iliyopita, ni wazi kila moja itaingia uwanjani ikiwa na shauku ya kutaka kuendelea kupata matokeo ya ushindi.
Hata hivyo, hakuna upande unaotegemea kukutana na mteremko kwenye mchezo huo kwani historia inathibitisha timu hizo zinapokutaba hasa Uwanja wa Jamhuri mtanange huwa wakukata na shoka.
Mshambuliaji Michael Sarpong, anatarajia kuendelea kuongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga kusaka mabao, wakati ambao Ditram Nchimbi na Yacoub Sogne wakianzia benchi.
Kwa upande wa Mtibwa, usajili mpya, Ibrahim Ahmad Hilika anategemewa mipango ya kusaka mabao ya Mtibwa Sugar, huku Jafary Kibaya akianza kama mchezaji wa akiba.
Wakizungumza maaandalizi ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Zatko Krmpotic, amesema wamefanya maandalizi ya kutosha, lengo kuhakikisha wanavuna pointi zote tatu.
Naye Zubery Katwila ambaye ni Kocha Mkuu wa Mtibwa, amesema wanawaheshimu wapinzani wao, lakini wataingia uwanjani wakiwa na dhamira moja tu ya kuvuna pointi tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Michezo mingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo, Ruvu Shooting, itaikaribisha Biashara United kwenye Uwanja wa Uhuru jijini hapa, wakati Mwadui itakuwa nyumbani kupepetana na Ihefu, Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.
Michezo mingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Polisi Tanzania iliishikisha adabu Dodoma Jiji FC, baada ya kuitandika mabao 3-0 , mchezo uliochezwa Uwanja wa Chuo cha Ushirika, Moshi.
Mabao ya Polisi yalifungwa na Marcel Kaheza dakika za 11 na 61 na jingine lililopachikwa kwa Tarik Seif dakika ya 38.
from Author
Post a Comment