WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mafundisho na miongozo inayotolewa na viongozi wa dini nchini ndiyo sababu kubwa ya kuifanya Tanzania iendelee kuwa nchi nzuri na yenye amani duniani.
Ameyasema hayo jana (Jumamosi, Oktoba 10, 2020) baada ya kufungua msikiti wa Rahman uliopo katika kijiji cha Kwamndolwa wilayani Korogwe, Tanga na ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa.
Waziri Mkuu amesema Watanzania wanatakiwa waendelee kuwarithisha imani za dini watoto wao ili kuwajenga katika misingi mizuri ya maadili itakayowafanya wawe raia wema.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa dini nchini kwa kuliombea Taifa tangu mchakato wa uchaguzi mkuu ulipoanza.
“Tunawashukuru viongozi wa dini, tuna zaidi ya mwezi mmoja tangu kuanza kwa kampeni na bado amani inaendelea kutawala nchini, hivyo msichoke kuliombea Taifa na kuwaombea wote wanaoshiriki katika mchakato wa kampeni.”
Msikiti huo umejengwa kwa gharama ya sh. milioni 150 kwa ufadhili wa taasisi ya Firdausi ambayo imekuwa ikijenge misikiti, kutoa misaada pamoja na kuchimba visima kwenye maeneo mbalimbali nchini.
By Mpekuzi
Post a Comment