Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM
KIUNGO wa Yanga,Juma Said Makapu,amesema kukosa nafasi ya kucheza hakumuumizi kichwa kwani muhimu kwake timu yake ipate ushindi.
Makapu alipoteza nafasi ya kudumu katika kikosi cha Yanga,baada ya kocha Zlatko Krmpotic kukabidhiwa jukumu la kukinoa aliporithi mikoba ya Luc Eymael.
Eymael alifutwa kazi baada ya msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara kukamilika na mikoba yake kutwaliwa na Krpotic ambaye aliiongoza Yanga kwenye michezo mitano ya msimu huu pekee kisha kibarua chake kuota nyasi.
Katika michezo hiyo, Makapu alikuwa akianzia benchi au kutopata nafasi kabisa.
Akiwa chini ya Eymael,Makapu alikuwa nguo imara katika safu ya ulinzi ya Yanga,akicheza nafasi ya beki wa kati kwa kutengeneza pacha na Lamine Moro.
Lakini pia,wakati Makapu anasajiliwa Yanga misimu kadhaa iliyopita, alikuwa akicheza nafasi ya kiungo mkabaji, nafasi ambayo kwa sasa wamekuwa wakiitumiia ama Feisal Salum, Tokombe Mukoko au Zawadi Mauya.
Katika nafasi ya ulinzi wa kati,Lamine amepanga na Bakar Mwamnyeto, ambaye amesajili msimu huu akitokea Coastal Union.
Kwa sasa Yanga haina kocha mkuu, badala yake kikosi hicho kipo chini ya kocha msaidizi,Juma Mwambusi.
Akizungumza na MTANZANIA,Makapu alisema haoni sababu ya kulalamika kwani anaamini utafika wakati wake nay eye atacheza.
“Kuanza au kutokuanza ni uamuzi wa kocha kulingana na anavyoona katika mchezo husika,kwangu sio tatizo hasa ninapoona tunapata alama tatu kwa sababu wachezaji wote furaha yetu ni kuona tunashinda.
“Kila jambo lina wakati wake, nakumbuka kipindi cha nyuma nilikuwa nacheza na kuna watu walikuwa wanaanzia benchi au kukosa nafasi kabisa,wale pia ni wachezaji kama nilivyo mimi,”alisema Makapu.
from Author
Post a Comment