Mwandishi Wetu, Lindi
Mgombea Ubunge Jimbo la Mchinga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwalimu Salma Kikwete, amesema safari ya upatikanaji wa maendeleo katika jimbo hilo inaanza rasmi Oktoba 28, mwaka huu baada ya wapiga kura kuwachagua wagombea wa chama hicho.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni zake zilizofanyika kuanzia Jumatano, juzi na jana kwenye vijiji vya Makumba, Muungano, Mchinga Moja, Ruvu, Kitomanga na Kilangala ‘A’, Mwalimu Salma, amesema maendeleo yatapatikana kwa sababu jimbo hilo si masikini kwa kuwa lina maeneo ya uzalishaji ikiwamo ardhi yenye rutuba, fukwe za bahari, kilimo, utalii, uvuvi na mito inayotiririsha maji mwaka mzima ila tatizo wananchi wa maeneo hayo wanashindwa kujipanga kutumia fursa hizo.
“Mchinga sio masikini hata kidogo tatizo tunashindwa kutumia fursa tulizopewa na Mungu, nimekuja kuleta mabadiliko ya maendeleo, sasa vijana msiwe na mihemuko kwa sababu Oktoba 28, tunaianza rasmi safari ya maendeleo kwa sababu jawabu la maendeleo mnalo ninyi wenyewe.
“Mlichoka maendeleo kwa kuchagua kitu mnachoona kinafaa, sasa hivi wenzenu katika maeneo mengine wakati wanapaa nyinyi ndiyo kwanza ni kama mtoto amezaliwa ana siku mbili, kwa hiyo tutoke katika hali duni na twende mbele katika kuchagua hali ya maendeleo.
“Mmezama katika shimo na mkitaka kujitoa mnatakiwa kuchagua mafiga matatu ambayo ni wagombea wote wa udiwani wa CCM, mbunge wa CCM na Rais wa CCM kwa sababu kiongozi anaweza kutoka chama chochote lakini kiongozi mzuri anatoka ndani ya CCM, chagueni mnyororo wa maendeleo kwa faida ya Mchinga.
“Mkinielewa vizuri mtatoka katika biashara ya shilingi elfu tano, mtapanda juu kwa sababu fursa zinapatikana, vijana wa bodaboda hapa Nangaru tutawatengenezea mpango mzuri wakopeshwe pikipiki ndani ya mwaka mmoja. Nani kama mama? Mimi ndio mama nataka niwabebe na sitaki niwaache katika safari ya maendeleo. Nataka kondoo wangu nitakaowachunga wawe hodari ,” amesema Mwalimu Salma.
Katika hatua nyingine, amesema moja ya kazi ya mbunge ni kusimamia shughuli za maendeleo na akichaguliwa anakusudia kuliunganisha jimbo hilo kwa kupigania ujenzi wa barabara zitakazopitika mwaka mzima ikiwamo zinazopita kutoka katika maeneo ya Kibaoni, Matimba, Nangaru na Milola.
Pia amesema maendeleo yataletwa katika jimbo hilo kwa kuboresha huduma za jamii ikiwamo kusimamia huduma za afya kwa kusaidia ujenzi wa zahanati na vituo vya afya pamoja na kujenga madarasa na maabara.
Amesema akichaguliwa kuwa mbunge amejipanga kuhakikisha atashirikiana na watu mbalimbali kupata majawabu au ufumbuzi wa kutatua kero za jimbo hilo.
“Tutashughulikia eneo la afya kwa sababu bila afya nzuri huwezi kufanya shughuli yoyote ya maendeleo, nitazungumza na wahusika serikalini watusaidie ujenzi wa zahanati, madarasa na maabara na tutazisemea bungeni.
“Na yote haya sio kwamba nafanya propaganda kama wengine, ninayoahidi nitayatekeleza mkinipa ridhaa ya uongozi wa miaka mitano, sifanyi au sisemi bla bla, tunasema ukweli na yanawezekana, hayo yote niachieni kwa sababu nataka kushughulikia kero za Mchinga kwa kuzipeleka kwa wakubwa serikalini,” amesema Mwalimu Salma.
Kuhusu kilimo, amesema kwa Mchinga lazima kiwe cha kisasa baada ya wakulima kuanza kutumia mbegu bora huku wafugaji nao wakitakiwa kufuga kwa mbinu bora.
from Author
Post a Comment