TUMEPATA kuandika mara nyingi tukikemea mwenendo wa kauli za makamanda wa polisi wa mikoa kuwa hazijengi, bali zinabomoa.
Makamanda hawa ni watu muhimu mno katika mikoa yao, hivyo kila kauli inayotoka kwenye kinywa chao, basi inapaswa kuwa sahihi ina isitiliwe mashaka.
Mbali ya kutiliwa mashaka, lakini kuzua maswali mengi kwenye jamii hadi kufikia hatua ya watu kujiuliza inakuwaje watu walioamini kusimamia usalama wa wananchi na mali zao wao ndiyo wanakuwa mbele kutoa kauli za ajabu ajabu kiasi hiki.
Tunakumbuka siku za nyuma Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro aliwahi kujitokeza hadharani na kulaani vikali kauli za wasaidizi wake hawa.
Akionekana kuchukizwa na kauli hizo, IGP alisema inashangaza kuona kamanda wa polisi anasimama hadharani na kuonyesha watuhumiwa huku akitoa maeneo ya ajabu.
Alisema utafika wakati amestaafu yuko kijijini akakosa hata nauli, lakini huyo anayemtangaza ndiye atamuokoa siku hiyo.
Pia amewahi kukemea vikali tabia ya makamanda kugeuka nusu wana siasa kwenye majukwaa. Tuliamini maelekezo haya yangesaidia kuwabadilisha baadhi ya makamanda ambao wanaonekana kwa namna moja au nyingine wanakiuka maadili ya utendaji kazi wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto bila amekuwa kina wa utoaji wa kauli za ‘kuudhi’ kwa jamii, lakini hatusikii hata kidogo amechukuliwa hatua gani.
Moja ya kauli yake ambayo imeibua hisia kwa watu wengi ni ile ya wagombea walioshindwa uchaguzi mkuu eti wamepigwa ‘kipigo cha mbwa kachoka’, hivyo wakijaribu kuandamana watakutana na kipigo cha mbwa koko.
Tunasema kauli hii ni hatari kwa ustawi wa jamii, kwanini kiongizi mkubwa kama huyu anashindwa kuzuia ulimi wake katika baadhi ya matamshi.
Miaka nenda rudi sasa, amekuwa hakimu wa maneno ambayo hakika hayajengi zaidi ya kuleta uhasama, misemo na yeye anaona ni vizuri, tunasema kwa umri wake anapaswa kubadilika.
Si huyu tu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa naye bila aibu alifyatuka kwa kusema ‘Wametandikwa majimboni kwao’, ole wao wajaribu kuandamana.
Inasikitisha mno makamanda walioaminiwa na kuwekwa kwenye miji mikubwa ndiyo wanakuwa na kauli za ajabu ajabu hizi.
Mwingine ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Hai (OCD), yeye bila aibu alimtakia mgombea Ubunge wa Hai, Freeman Mbowe kwamba hatashinda kiti hicho na kweli hakushinda. Inawezekana hakuwa nania mbaya, lakini matamshi yake yanaweza kumhukumu.
Tunatambua jeshi la polisi linafanya kazi zake kwa kufuata mwongozo uliopo, ni vema makamanda hawa wakabaki kwenye mstari kuliko hivi wanavyofanya.
Ndiyo maneno ya aina hii, husababisha wananchi waone kama jeshi hili linatumia na chama fulani wakati si kweli. Kumbe ni askari wachache ambao wanaweza kulipaka matope.
Sisi MTANZANIA, tunamshauri IGP Sirro kwa mara nyingi tena awakanye makamanda wake wafanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni, miongozo ili kuepukana na kuchafua chombo hiki ambacho kinafanya kazi nzuri usiku na mchana.
Tunatambua IGP ana mamlaka makubwa hata ya kufanya mabadiliko, lakini si nia yetu kumshikiza, bali kuwakumbusha PGO inasemaje kwa kamanda wa polisi au kiongozi wa jeshi anapaswa kusema nini kwa wakati gani.
Kazi nzuri iliyofanywa na jeshi hili wakati wa uchaguzi na inaendelea kufanyika, isichafuliwe na makamanda wachache ambao wakati mwingine wanasahau mipaka yao ya kazi. IGP Sirro safisha nyumbani kwako.
from Author
Post a Comment