Na WINFIRIDA MTOI, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, yupo katika maandalizi kabambe ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiwapa kazi maalum Luis Miquissone na Meddie Kagere baada ya kumaliza majukumu ya timu za Taifa na kupewa tizi maalum.
Luis na Kagere walikosa mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union kutokana na majukumu hayo.
Simba inatarajia kuikabili Plateau United ya Nigeria katika mchezo utakaopigwa Ijumaa hii, nchini Nigeria, ikiwa ni hatua ya awali ya michuano hiyo.
Wanamsimbazi hao, waliendelea kujichimbia jijini Arusha baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Coastal Union, walioibuka na ushindi wa mabao 7-0 kwenye Uwanja Sheikh Amri Abeid, jijini humo.
Uongozi wa Simba, kupitia mitandao yao, umethibisha nyota hao kuungana na wenzao na juzi walifanya mazoezi ya pamoja, tayari kwa safari ya Nigeria.
“Meddie Kagere na Luis, wameanza mazoezi na wachezaji wenzao baada ya kurejea kikosini wakitokea katika zao za Taifa,” ilisema Simba.
Naye Sven katika mtandao wake wa instagram, alisema wana changamoto kubwa inawakabili Ijumaa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Ilikuwa ni wikiendi nzuri kwa wanafamilia ya Simba, changamoto kubwa ipo mbele yao wikiendi ijayo(Ijumaa) katika Ligi ya Mabingwa Afrika,” aliandika Sven.
Meneja wa kikosi hicho, Abbas Ally, alisema wanatarajia kuondoka leo kuelekea nchini Nigeria kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Simba ina kibarua kigumu katika michuano hiyo ambayo wanahitaji kurejesha heshima yao waliowahi kujitengenezea baada ya kutinga robo fainali kutokana na msimu uliopita kutolewa hatua ya awali.
from Author
Post a Comment