Mbatia awageukia viongozi wa kidini kuomba mwafaka |Shamteeblog.

Na LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameshauri kufanyika kwa mazungumzo ili kupata mwafaka wa kitaifa utakaoliwezesha taifa kwenda mbele baada ya kuwapo kasoro mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mbatia aliwataka viongozi wote wa kidini kutumia ndimi zao vizuri, kukubaliana kwamba masilahi ya Tanzania kwanza, mambo mengine baadaye na kamwe wasikubali kukichoma moto kichaka kilichowahifadhi.

Mbatia alisema kuwa hisia za wanasiasa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu haziwezi kuelezwa kwa maneno, bali watu wote wenye upendo na Tanzania wanaweza kuziona hisia hizo.

Hata hivyo alisema kuwa pamoja na watu mbalimbali kuwa na hisia hasi zinazokinzana na utu, maadili ya Kitanzania pamoja na tunu zilizoelezwa kupitia Wimbo wa Taifa za umoja na amani, zinaweza kuchoma kichaka ambacho wamejihifadhi ambacho ni Tanzania.

 “Maneno hayatoshelezi kuelezea hisia, labda kwa kupitia nafsi. Hisia zetu kwa ujumla kuhusu mchakato wa tukio lililoitwa Uchaguzi Mkuu wa 2020, haziwezi kuwakilishwa kwa maneno, lakini wote wenye nia nzuri na mama yetu Tanzania kwa kupitia nafasi zao wanaweza kusikia au kuelewa hisia za wengi kwa muda huu.

“Licha ya kwamba kwa miaka 59, hatujaweza kumtumia vizuri mama Tanzania ili tuweze kujipatia mahitaji msingi kwa wote na kwa furaha ya kweli, sasa tuko kwenye kumwangamiza,” alisema Mbatia.

Alisema kuwa kwa miaka 28 chama chake kimekuwa kikiimba wimbo wa kupata Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba sasa gharama zake zimekuwa kubwa.

“Maneno yetu sasa yanasikika dunia nzima, kwani dunia nzima imeshuhudia vitendo vinavyokiuka makubaliano yetu ya kitaifa ya miaka 28 iliyopita, kwamba maendeleo endelevu yanatokana na demokrasia ya vyama vingi vya siasa. 

“Kama taifa tumekiuka hata makubaliano ya kitaifa, kwa mfano kufunga baadhi ya mitandao ya kijamii,” alisema Mbatia.

Aliongeza kuwa endapo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere angekuwapo leo, angewaeleza kuwa hii si Tanzania na demokrasia aliyowaachia na angewataka kujikusanya waanze upya.

“Hii siyo kwa wanasaiasa peke yao, ni la Watanzania wote, hatuwezi kuangalia tu wakati mama anaamka na huzuni na kulala na hasira,” alisema Mbatia.



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post