NEMC yawaonya watapishaji vyoo wakati wa masika |Shamteeblog.

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na maofisa mazingira wa majiji, manispaa and halmashauri zote  nchini, wamejipanga  kudhibiti wakazi wenye tabia ya  kutapisha vyoo hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Mhandisi Dk. Samuel Gwamaka alisema Baraza halitakuwa na huruma wala kurudishwa nyuma na watu wachache ambao wamekuwa kikwazo katika kulinda na kutunza mazingira.

“Hivi karibuni, mtakumbuka kuwa nchi yetu imeingia katika uchumi wa kati na hiyo imetokana na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya tano katika nyanja ya uchumi, afya, mazingira na sekta zingine. Hatutataki kurudi tena zama za kipindupindu hasa katika jiji la Dar es Salaam,’’ alisema Dk. Gwamaka.

Katika kuhakikisha wanadhibiti hali ya utapishaji, Dk. Gwamaka alisema Baraza limejipanga kushirikiana na maofisa  mazingira wa majiji, manispaa na halmashauri kudhibiti hali hiyo sambamba na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wote.

 “Baraza  linashirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuhakikisha maofisa mazingira wa jiji, manispaa na halamashauri zote nchini wanasimamia sheria, taratibu na kanuni za mazingira ikiwemo suala la utapishaji kwenye maeneo ya makazi ya watu,’’ alisema.

Dk. Gwamaka aliwaomba Watanzania kuendelea kushirikiana na NEMC hususani kupitia kitengo chake cha timu ya dharura ambacho kinafanya kazi kwa saa 24 kila siku kwani mafanikio makubwa yameshapatikana.

“Wito wangu kwa Watanzania wasichoke kutoa ushirikiano kwa Baraza hasa kwa kitengo chetu cha dharura ambacho kimekuwa kikifanya kazi nzuri  kwa saa 24  ili kukabiliana na changamoto za mazingira kwa kuwa watumishi wa chombo hicho hawawezi kuwa kila mahali,’’ alisema.

Aidha, aliwashauri Watanzania kuunganisha nguvu ya pamoja kama wanadhani gharama za kutumia magari ya taka ni kubwa ili kuepuka adhabu kali ikiwemo kufikishwa mahamani kwa sababu ya upishaji wa maji taka na utapishaji vyoo.

“Kuna taarifa tunazipata kutoka kwa watu mbalimbalin kuwa changamoto inayochangia watu kutapisha vyoo ni gharama za ukodishaji magari ya taka ambayo yamekuwa yakinyonya majitaka katika makazi ya watu. Nawashauri  kuunganisha nguvu ya watu wawili au watatu ili waweze kupata gari ambayo itanyonya majitaka kuliko kuyatiririsha kwenye makazi ya watu kinyume na sheria ya mazingira,’’ alieleza.

Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Baraza limeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha mazingira yanalindwa ipasavyo ikiwemo kudhibiti uchafuzi wa kelele, kusimamia ipasavyo katazo la mifuko ya plastiki pamoja na udhibiti wa utupaji wa taka hatarishi.



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post