BRUSSELS, UBELGIJI
KUMINYWA kwa haki za binadamu na msaada wa Euro Milioni 27 takribani Shilingi bilioni 74 ambao Tanzania ilipokea mapema mwaka huu kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kukabiliana na athari za corona ni mambo ambayo yamezua mjadala katika Bunge la Umoja huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje wa Bunge hilo Dk. David McAllisster ndiye aliyehoji hayo.
Tayari Serikali ya Tanzania imefafanua kuhusu kikao kilichojadili masuala hayo zikiwemo taarifa zilizosambaa mara moja kwenye mitandao ya kijamii kwamba EU imekusudia kuifutia Tanzania mikopo na misaada yote ambayo imeomba kwenye umoja huo na mashirika yake.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kusainiwa na Sheiba Bulu ambaye ni Kaimu Mkurugenzi-Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, mbali na kukana taarifa za EU kukusudia kuifutia Tanzania misaada ilisisitiza kuwa kikao kilichojadili masuala hayo ni utaratibu wa kawaida.
“Tarehe 19 Novemba 2020, Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Umoja wa Ulaya (European Parliament’s Committee on Foreign Affairs) ilikutana katika kikao cha kawaida na kujadili masuala mbalimbali ya ndani na nje ya Umoja wa Ulaya ikiwa ni sehemu ya kikao cha Bunge la Umoja huo kinachoendelea Jijini Brussels nchini Ubelgiji.
“Kikao hicho kimejadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya kisiasa Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu, huu ni utaratibu wa kawaida wa Bunge hilo kufanya tathimini ya aina hiyo kwa kila nchi mbia wake inapokuwa imemaliza uchaguzi mkuu”
Kuhusu kusudio la kuifutia msaada wa Euro milioni 626 sawa na shilingi Trilioni 1.6 inazopata kila mwaka ka ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje mbali na kukana ilieleza kuwa Kamati hiyo haina mamlaka ya kuchukua uamuzi huo isipokuwa Bunge la Umoja wa Ulaya linaloundwa na wabunge 705.
“Kamati hiyo haina mamlaka ya kutoa maazimio na kilichofanyika ilikuwa ni kusikiliza maoni ya baadhi ya wajumbe wake”
Hata hivyo Taarifa hiyo ya Mambo ya Nje haikufafanua lolote kuhusiana na hoja ya fedha zilizotolewa na EU kwa ajili ya kukabiliana na corona lakini pia uvunjifu wa haki za binadamu.
Zaidi taarifa hiyo ilihakikishia umma kwamba uhusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ni mzuri na kwamba unazidi kuimarika na wanashirikiana katika maeneo mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa pande zote mbili.
Dk. David McAllisster ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje wa Bunge hilo la EU alihoji vigezo vilvyoitumiwa na uongozi wa EU kutoa msaada kwa Tanzania ambayo ameituhumu kwa kutokuwa wazi juu ya taarifa za corona na kutofuata miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Ninapata wakati mgumu kwamba tunatoa fedha kwa Tanzania ambayo haifuati kanuni za WHO, serikali haina ushirikiano…
“Nataka kujua vigezo na taratibu zilizotumika kutoa fedha, kufanya nini na zimetumikaje?” alihoji Dk. McAllister ambaye alitoa saa 48 (kuanzia jana asubuhi) kupata majibu kutoka kwa maofisa wa EU.
Mwenyekiti huyo pia aligusia juu ya kuminywa kwa haki za binadamu na kutaka EU na washirika wake wahakikishe watetezi wa haki za binadamu wanalindwa Tanzania.
Baadhi ya mitandao nchini Tanzania iliripoti juu ya tukio hilo na kudai kuwa Bunge la EU limepitisha azimio la kuiwekea vikwazo Tanzania, taarifa ambazo zimekanushwa na serikali ya Tanzania.
Taarifa juu ya msaada huo awali zilitolewa Septemba 14 na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
Taarifa hiyo ilimnukuu Rais wa Baraza la EU Charles Michel akisema kuwa msaada huo unalenga kujenga miundombinu ya maji na umeme kwenye zahanati na hospitali za serikali.
“Umoja wa Ulaya umesema uko tayari kutoa kiasi cha Euro milioni 27 sawa na takriban shilingi bilioni 70 za Tanzania kwa lengo la kusaidia mipango ya kukabiliana na janga la Covid 19 na madhara yake ya kiuchumi”
Nia ya msaada huu wa Umoja wa Ulaya ulikuja wakati Tanzania ikiwa imekwisha tangaza kumalizika kwa ugonjwa wa Corona nchini humo.
Katika mkutano wa kampeni za uchaguzi, Rais wa Tanzania John Magufuli alisema kuwa shetani alitaka kuitawala dunia kupitia virusi vya corona lakini hana nafasi nchini Tanzania.
Magufuli alisema kuwa; ”Haiwezekani kwa uchumi wa dunia kufungwa kwasababu ya ugonjwa”
Akizungumza katika mkutano huo Chato Geita, Magufuli alisema; bahati nzuri, serikali yake haikukubali shinikizo la kufunga shughuli za kiuchumi na kukaa nyumbani ”lockdown”.
Shirika la Utangazaji la Uingereza limeandika kuwa; Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na EU, Jestus Nyamanga amekanusha vikali juu ya ripoti za kupitishwa kwa azimio la Bunge la EU dhidi ya Tanzania.
Ameeleza kuwa kikao kilichoketi kilikuwa cha Kamati ya Mambo ya Nje na si Bunge lote.
from Author
Post a Comment