Wahamiaji haramu 52 wakamatwa |Shamteeblog.

Na SHEILA KATIKULA- MWANZA

JUMLA ya wahamiaji haramu 52 kutoka Ethiopia wamekamatwa Novemba 23 mwaka huu mkoani Mwanza wakiwa katika harakati za kwenda nchini Afrika Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza, Bahati Mwaifuge alisema wahamiaji hao walikamatwa Novemba 23 mwaka huu katika makundi mawili tofauti.

Mwaifuge alifafanua kuwa kundi la kwanza la watu wanne lilikutwa katika nyumba ya kulala wageni katika mtaa wa Mabatini na wengine 48 walikutwa mtaa wa Buguku Kata ya Buhongwa.

Alisema waliokamatwa katika Kata ya Buhongwa walikuwa wanaishi ndani ya nyumba bila kutoka nje ambapo huduma zote walizipata bila kutoka nje.

“Tumeshirikiana na Jeshi la Polisi kuwakamata wahamiaji hawa kwani walikuwa wanaishi kwenye nyumba ndogo wote kwa siri kiasi kwamba hakuna hata jirani mmoja aliyefahamu kama kuna mtu anaishi katika nyumba hiyo,”alisema.

Aidha alisema kuwa kipindi hiki kuna ongezeko kubwa la wahamiaji kutoka Ethiopia wanaopita hapa nchini, ambapo Novemba peke yake wamekamatwa wahamiaji haramu 59.

Hata hivyo aliwataka watu wanaojihusisha na biashara ya kusafirisha wahamiaji hao waache mara moja, kwani endapo watagundulika adhabu yake ni faini ya Sh milioni 20 na kufungwa jela miaka 20 na kutaifisha mali zake.

“Tukikugundua unajihusisha na biashara hii tutakuchukulia hatua kali ikiwamo kifungo cha miaka 20, utatozwa faini ya Sh milioni 20 na kutaifisha mali zako zote ili iwe fundisho kwa watu wengine,”alisema Mwaifuge.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema wanaojihusisha na kuwahifadhi wahamiaji hao watatafutwa mpaka wapatikane.

Mongela alisisitiza kwamba wamiliki wa nyumba walikokutwa wahamiaji hao wasipojitokeza mali zao zitataifishwa na kuwa ya umma kwa mjibu wa sheria ya makosa ya uhamiaji.



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post