Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WATANZANIA wameshauriwa kuwa na utaratibu wa kusoma vitabu na kuwanunulia vitabu watoto wadogo ili wajenge tabia ya kujisomea tangu wakiwa wadogo.
Hayo yalielezwa juzi jijini hapa na Mtunzi wa Vitabu Dk. George Adriano, wakati akizindua vitabu vyake vya ‘The Power of Choice’ na ‘Why not today’.
“Ni kweli mazingira ya vijijini kwa kiasi kikubwa si mazuri na Watanzania kwa kiasi kikubwa hatupendi kusoma vitabu, lakini ukijaribu kuangalia ni mfumo wa maisha mtoto yupo shule ya msingi hajui kitabu huyu mtoto anapokuwa ukimletea kitabu anaona ni kitu kipya kabisa.
“Baada ya kuandika vitabu hivi tukawa na wazo la kuwa shirika lisilo la Serikali ambalo litakuwa na lengo la kuona namna ambayo tunaweza kupenyeza mawazo ya watoto kupenda kusoma na tuandike vitabu ambavyo vitawajenga watoto.
“Sisi kama Cupelife Tanzania tutavipitia na kuvisambaza kwa wadau sisi tuvipeleke katika shule za msingi za pembezoni ambazo hazifikiwi ili watoto hawa waweze kusoma,”alisema.
Akikizungumzia Kitabu cha The Power of Choice, alisema kinaelezea nguvu iliyopo kwenye kuchagua jambo fulani.
“Kwa mfano umeamua kusoma sayansi, kama ni mwanafunzi unaweza kuelekea kuwa mwanasayansi, kama umesoma masomo ya biashara unaweza kuelekea kwenye biashara, kwahiyo chochote ambacho unaweza kuchagua na nguvu ya kukupelekea huko ulikochagua.
Pia alisema kimezungumzia habari ya uhuru wa mtu kuchagua jambo jema ambalo litamsaidia kutoka katika hali duni kwenda katika hali chanja.
“Kwa hiyo kuna vitu vingi vimeelezwa ikiwa ni pamoja na namna ya kufikiri,vitu gani vinaathiri uchaguzi mojawapo ni kufikiri mazingira,utamaduni, imani,hivyo vitu vinaweza vikakuathiri na ukachagua vitu ambavyo havikufai.
Akikizungumzia kitabu cha Why not today alisema kuna wakati unakutana na vikwazo vingi hivyo ameweka wazi jinsi ya kukabiliana navyo.
“Mimi ni Daktari niliamua kufanya biashara ndani ya fani yangu hii kwahiyo kuna wakati unakutana na vikwazo sasa ni namna gani ya kuweza kuvitatua.
“Kwenye kitabu nimeandika kuna wakati ukiona mambo yanaenda vizuri sana na yametulia uwe makini kwani wakati mwingine ndio pale ambapo huwa unajisahau na nidhamu yako inakuwa ya kawaida sasa kwenye kitabu naonya ukiona vitu vinaenda vizuri uwe makini.
“Watu wengi biashara zinakufa sababu ya kujiachia anaanza kula mpaka mtaji nimezungumza faida gani mtu anapata anapotaka kuanza kitu,na unaponaza ndio inafungua mipango hatua gani ifuate,anaaenza ndio ambaye anapata ‘saport’”alisema.
Alisema vitabu hivyo ni vya Kiingerreza hivyo anampango wa kuvibadilisha na kuviweka katika lugha ya Kiswahili.
from Author
Post a Comment