Watu 6 akiwemo Padri Sixtus Masawe wafariki dunia katika ajali ya gari |Shamteeblog.
Jumla ya watu 6 akiwemo Padre Sixtus Massawe, paroko wa parokia ya Masakta Babati, mkoani Manyara, wamefariki dunia kufuatia ajali ya gari baada ya gari yao kuligonga lori kwa nyuma, maeneo ya kambi ya kijeshi ya Sofa iliyopo mkoani Arusha, wakati wakitoka kwenye msiba wilayani Rombo.
Taarifa hiyo imetolewa Novemba 26, 2020, na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Salum Hamduni, ambapo ameeleza kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa 8:20 usiku wa kuamkia Novemba 26, huku akikitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva wa gari la kanisa kwani alikuwa anaendesha gari kwa mwendokasi pasipokuchukua tahadhari.
Aidha Kamanda Hamduni amesema kuwa waliofariki katika ajali hiyo ni wanaume 5 na mwanamke mmoja na kati ya hao aliyetambulika ni mmoja tu ambaye ni Father Sixtus Massawe, na kuongeza kuwa gari hilo lililogongwa kwa nyuma lilikuwa limesimama katika eneo hilo baada ya kupata hitilafu ya kiufundi na miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Monduli kwa ajili ya uchunguzi.
Kamanda Hamduni pia ameyataja majina ya majeruhi sita wa ajali hiyo, akiwemo Francis Gitayane (57), Muiraq na mkazi wa Masakta, Marko Slaa (56), Muiraq na mkazi wa Masakta, Patrice Faustine(34), Silas Giani, Timoth Faustine na Dismas wote wakazi wa Masakta na wote wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Mount Meru.
By Mpekuzi
Post a Comment