Koku David, Dar Es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango anatarajiwa kushuhudia wahitimu 389 waliohitimu katika Chuo cha Kodi (ITA) na kutunukiwa vyeti katika mahafali ya 13 yatakayofanyika kesho chuoni hapo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Chuo cha ITA, Profesa Isaya Jairo alisema kuwa idadi hiyo itakuwa imewezesha chuo kufikisha wanafunzi 5153 ambao wamehitimu katika chuo hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008 hadi sasa.
Alisema ITA ambayo ni sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni chuo pekee nchini katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini chenye usajili na ithibati ya kudumu kutoa mafunzo ya forodha na kodi kwa wadau mbalimbali.
Alisema kati ya wahitimu hao, wahitimu 165 watatunukiwa cheti cha Uwakala wa Forodha cha Afrika Mashariki (EACFFPC) na wahitimu 18 watunukiwa Cheti cha Usimamizi wa Forodha na Kodi (CCTM).
“Wahitimu wengine 71 wanatarajiwa kutunukiwa Cheti cha Stashahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi (DCTM) huku wahitimu 117 watatunukiwa Cheti cha Shahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi (BCTM) wahitimu 18 watatunukiwa Cheti cha Stashahada ya Uzamili katika Kodi (PDGT),” alisema Profesa Jairo.
Alisema kutokana na hatua hiyo, chuo cha ITA kinajivunia mafanikio mengi katika kutoa mafunzo ya forodha na kodi yaliyopatikana tangu kuanza kwa chuo hicho.
Alisema chuo hicho hivi sasa kinatoa mafunzo yanayoendana na mabadiliko ya sayansi, teknolojia na kiuchumi na kwamba ndio maana kimeboresha mtaala wake wa masomo ili kukidhi mahitaji ya sera ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi na viwanda.
“Mtaala huu utawezesha vijana wanaohitimu katika chuo hiki kukidhi mahitaji ya soko la ajira katika Nyanja za forodha na kodi ndani na nje ya nchi,” alisema Profesa jairo.
Alisema pamoja na kutoa mafunzo, ITA pia inatoa ushauri na kujengea uwezo watumishi wa TRA, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na mamlaka zingine za Mapato na kodi za Afrika.
Profesa Jairo aliongeza kuwa, ITA inaendeleo na mazungumzo ya kuendelea kuijengea uwezo Mamlaka ya Mapato ya Sudan Kusin pamoja na kuanzisha mchakato wa kuijengea uwezo Mamlaka ya Mapato ya Komoro katika ukusanyaji wa kodi.
“Wakuu wa mamlaka hizo na ujumbe wao tayari wapo hapa nchini ili kuhakikisha wanaweka misingi ya makubaliano ya kutekeleza mipango mikakati iliyopo,” alisema Profesa Jairo.
from Author
Post a Comment