Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu amewataka wachungaji kuhubiri neno la Mungu na kuachana na mambo ambayo hayampendezi Mungu.
Akizungumza leo, Desemba 6,jijini hapa wakati wa ibada ya kuwasimika wachungaji watano wa kanisa hilo ambayo ilienda sambamba kuwasimika Naibu Katibu Mkuu anaeshughulikia fedha katika Kanisa hilo, Erick Makigi na Naibu Katibu anaeshughulikia Mipango, Uchumi na Utawala, Rodrick Limo.
Askofu Kinyunyu amesema wachungaji wanatakiwa kwenda katika makanisa yao kama watumishi wa Mungu na kwa ajili ya kuhubiri neno la Mungu na kuachana na mambo ambayo hayampendezi Mungu.
“Mtu asiwadanganye jambo lolote kwamba kuna miujiza zaidi ya Yesu,miujiza anayo Yesu pekee.Muwe wachungaji wa Mungu sio kwa ajili ya ujira, muwe kwa ajili ya bwana na sio kwa ajili ya ujira, tatueni matatizo na ninyi nyote mmeamua kufanya kazi kwa ajili ya Kristo hakuna ambacho kitashindikana.
“Nyinyi mnaobarikiwa kwa kuwa mmeitwa kuwa wachungaji tufahamu utukufu wenu muwe wachungaji wa Mungu, mtende matendo mema kila mahali bila kuangalia mpo katika mazingira yapi,”amesema.
Aidha, Askofu Kinyunyu amewataka Watanzania kuwaunga mkono katika jitihada za kanisa za kuhakikisha kunakuwa na Kanisa kubwa na lenye ubora katika eneo la Ikulu cha Chamwino.
Amesema Ikulu ni mahali penye hadhi hivyo kanisa la KKKT linahitaji kujenga kanisa kubwa ambalo atakuwa akisali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Usharika wetu wa Chamwino Ikulu unahitaji kuboreshwa uwe sawa na hadhi ya Ikulu na kule Askofu Mkuu anawajibika moja kwa moja,tutahitaji kujenga Kanisa la Ikulu na wote tutachangia kufanikisha ujenzi huo bila kujali eneo ulilopo,niombe katika hili tuungwe mkono,”amesema Askofu Kinyunyu.
from Author
Post a Comment