Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Ndugu, Noely Byamungu (wa kwanza kulia) akiwa kwenye majadiliano ya mapendekezo ya paketi zitakazotumika katika majaribio ya programu ya unywaji maziwa shuleni Operesheni Meneja wa kiwanda cha Milkcom Ndugu, Walid Nahdi (wa pili kulia) wakati alipotembelea kiwanda hicho jana jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Afisa Usindikaji Bodi ya Maziwa, Fathiya Rashid akifuatiwa na Meneja wa Ubora wa Maziwa Ndugu, Shahibu Rashid ( wa pili kushoto).
Kikao cha pamoja kati ya Bodi ya Maziwa na uongozi wa kampuni ya Maziwa ya Milkcom kilicholenga kujadili ushirikishwaji wa makampuni za kusindika maziwa katika mpango wa majaribio wa Programu ya Unywaji Maziwa Shuleni unaotegemewa kuanza hivi karibuni katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na Unywaji wa Maziwa katika ofisi za Umma.
Hayo amesema jana jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea kiwanda cha Maziwa cha Milkcom Dairies kilichopo Kigamboni jijini Dar es salaam kwa lengo la kuangalia namna bora ya ushirikishwaji wa wasindikaji maziwa katika mpango wa majaribio wa Programu ya Unywaji Maziwa Shuleni pamoja na unywaji wa maziwa katika ofisi za serikali.
Kiwanda cha Milkcom kinasindika takribani lita 20,000 tu za maziwa chini ya uwezo wa kiwanda uliosimikwa wa kusindika lita takribani 100,000 kwa siku.
Bymungu, amesema kuwa Bodi ya Maziwa ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Mpango wa majaribio wa Programu ya Unywaji Maziwa shuleni utakaoanza hivi karibuni katika mikoa mbalimbali nchini utakaoimarisha masoko ya maziwa kwa wenye viwanda.
Byamungu amesema kuwa mpango huo utasaidia viwanda kupata masoko ya maziwa kwa wingi lakini pia kuimarisha afya ya mwili na akili za watoto pindi wawapo darasani na hivyo kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Sanjari na hilo, Byamungu amesema kuwa Bodi ya Maziwa itahakikisha ofisi za serikali zinakuwa wanunuzi wa kubwa wa maziwa kwa kutumia maziwa yanayozalishwa ndani ya nchini ili kuongeza unywaji wa maziwa nchini ambapo kwa sasa wastani wa unywaji maziwa kwa mtu kwa mwaka ni lita 54.7 tu ukilinganisha na lita 200 zinazopendekezwa na WHO pamoja na FAO.
Byamungu amesema kuwa ongezeko la unywaji wa maziwa litasaidia kuimarisha kipato cha mfugaji na kuimarisha uchumi wa viwanda vya ndani.
Nae Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Milkcom, Abubakar Faraji, amesema usindikaji huo mdogo umesababishwa na miundo mbinu mibovu ya uzalishaji maziwa ikiwemo Barabara pamoja na umeme vinavyosababisha kiwanda kusindika maziwa chini ya uwezo wake.
Faraji amesema kukatika kwa umeme mara kwa mara na kwa muda mrefu kunaisababishia kampuni hasara kwani kampuni hulazimika kutumia genereta katika usindikaji wa maziwa ili kuepuka hasara ya maziwa kuharibika.
"Kutokana na changamoto hiyo, kampuni imejikuta ikitumia gharama kubwa za uendeshaji wa biashara ya maziwa kuliko ilivyotarajiwa na hivyo kusindika chini ya uwezo wake" Alisema
Hivyo, Faraji ameitaka Bodi ya Maziwa kuja na mikakati itakayosaidia wasindikaji kupata masoko ya maziwa ili kuweza kuzalisha maziwa kwa wingi ikiwemo kutoa hamasa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari juu ya umuhimu wa maziwa na hatimaye kuongeza unywaji wa maziwa na bidhaa zake nchini.
By Mpekuzi
Post a Comment