Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Uchindile kata ya Uchindile Jimbo la Mlimba wakimsikiliza Mbunge wao, Godwin Kunambi (hayupo pichani) alipofika katika kijiji hicho kuwashukuru wananchi hao kwa kumchagua."Ahsanteni akina Mama" Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akiwashukuru akina Mama wa Kijiji cha Lugala kwa kumchagua katika uchaguzi mkuu uliopita. Kunambi amefanya mkutano na wananchi hao na kuchangia mifuko 50 ya Saruji kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati.Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lugala katika Kata ya Uchindile alipofika kuwashukuru na kuchangia mifuko 50 ya saruji.Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akiwa katika kikao cha pamoja na wawekezaji wa kiwanda cha karatasi cha Mufindi Paper Mills (kulia kwake) na wengine ni viongozi wa Kata ya Uchindile. Mbunge Kunambi amefanya mazungumzo na wawekezaji hao na wamekubali kujenga kituo cha afya katika kata hiyo ya Uchindile.Mbunge wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Naibu Meneja wa Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi Paper Mills, Maharambati Kumar alipotembelea kiwanda hiko kwa ajili ya kujenga mahusiano na wawekezaji hao.Charles James, Michuzi TV
UHAI kwanza! Ndiyo kauli ambayo Mbunge wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro (CCM), Godwin Kunambi ameitoa katika ziara yake ya kwanza toka achaguliwe ambapo ameanza na ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Lugala kata ya Uchindile wilayani Mlimba.
Kunambi amechangia mifuko 50 ya Saruji yenye thamani ya Sh Milioni Moja ili ujenzi wa Zahanati hiyo uanze haraka lengo likiwa ni kumaliza changamoto ya afya kwa wananchi wa Kijiji hicho huku pia akiahidi ifikapo Januari 15 mwaka 2021 ujenzi wa kituo cha afya kitakachohudumia kata nzima ya Uchindile utaanza.
Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Lugala na Uchindile, Mbunge Kunambi amesema uhai ni muhimu kuliko kitu chochote kwenye maisha ya binadamu na ndio maana amechagua kuanza na ujenzi wa Zahanati na Kituo cha Afya na baadae atahamishia nguvu zake kwenye maeneo mengine ikiwemo miundombinu.
" Nimefika leo kwa kazi mbili, moja kuwashukuru kwa kumchagua Rais Dk John Magufuli na kweli kura zote mlimpa, yapo mengi niliwaahidi wakati wa kampeni lakini mimi nimeona uhai ni bora zaidi, hivyo tutaanza ujenzi wa Zahanati ya kijiji chetu hivyo nachangia mifuko 50 ya saruji ili ujenzi uanze mara moja, lengo langu ni kuona wote mnatibiwa katika Zahanati hii.
Hivyo mimi kama Mbunge wenu leo natoa kiasi cha Sh Milioni Moja na ninakabidhi kwa Mtendaji wenu wa Kijiji hapa Lugala ili mifuko 50 ya Saruji inunuliwe na ujenzi uanze mara moja na itakapofika hatua ya kupaua nitakuja tena kuleta mabati," Amesema Kunambi.
Katika ziara yake hiyo, Mbunge Kunambi pia ametembelea kiwanda cha karatasi cha Mufindi Paper Mills kwa ajili ya kuboresha mahusiano na wawekezaji wa kiwanda hicho na katika mazungumzo yake na uongozi wa kiwanda hiko wamekubali na kuahidi kujenga Kituo cha Afya katika Kata hiyo ya Uchindile.
" Ni faraja kubwa kuwa na wawekezaji wanaotoa mchango wao kwa Jamii inayowazunguka, ndugu zetu wa Mufindi Paper Mills nimewaomba watusaidie katika sekta ya afya na wamekubali kujenga Kituo cha Afya katika Kata yetu ya Uchindile na ujenzi huo utaanza Januari 15 mwakani na mimi nitakuepo tuchimbe wote Msingi," Amesema Mbunge Kunambi.
Kunambi ambaye alikua Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kabla ya kugombea Ubunge Jimbo hilo la Mlimba amewashukuru wananchi wa Mlimba kwa kumchagua kwa kura nyingi za kishindo Rais Dk John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu uliopita lakini pia akiwashukuru kwa kumchagua yeye bila kupingwa katika nafasi ya Ubunge pamoja na Diwani wa Kata hiyo ya Uchindile.
Kwa upande wao wananchi wa Kata hiyo ya Uchindile wamemshukuru Mbunge Kunambi kwa moyo wake wa kukumbuka ahadi alizotoa wakati wa kampeni hasa hiyo ya ujenzi wa Zahanati lakini pia kufanikisha kuletwa kwa walimu wanne katika kata hiyo.
" Mbunge wetu tunashukuru sana kwa ujio wako hapa, katika kata yetu haijawahi kutokea Mbunge amechaguliwa halafu akarudi kushukuru na kuleta mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati, wewe umefanya hivyo na zaidi umeahidi kituo cha afya kitaanza kujengwa Januari, tunakuombea uendelee na moyo huo huo," Amesema Mzee Ndagalasi mmoja wa wanakijiji wa Lugala.
By Mpekuzi
Post a Comment