Na Mwandishi Wetu,
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijjini (REA), kuhakikisha wanawaunganishia umeme wateja wote waliolipia ankara za umeme jijini Mwanza na maeneo ya vijijini ndani ya miezi mitatu kuanzia tarehe 30 Desemba, 2020.
Waziri Kalemani ameyasema hayo, tarehe 29 Desemba, 2020, alipokuwa akizungumza na Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kikao kazi cha pamoja kilichofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza.
Pamoja na agizo hilo la kuwaunganishia umeme wateja hao ndani ya miezi mitatu, Waziri Kalemani, amewaelekeza watendaji hao kuhakikisha wateja wote walioko katika maeneo ya vijijini na kando kando ya miji, wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000 bila kujali umbali wa mita 30 kwani ni wajibu wa TANESCO kuwafikishia wananchi nguzo za umeme ili kuwafikia wateja hao.
“Mnataka kila mwananchi awe mita 30 ndipo muwafikishie umeme? Ni kazi yenu kupeleka nguzo hadi muwafikie wananchi hao. Nisisikie mtu anaongelea suala la mita 30.” amesema Kalemani
Vilevile, Waziri Kalemani, ameitaka TANESCO kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja ili kuhakikisha wateja wanapatiwa huduma bora na kwa wakati ili kuwaondolea adha ya kufuatilia maombi ya kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi za TANESCO wilayani.
Amewataka watendaji wa TANESCO kuwafuata wateja mahali walipo na kuepuka kutumia lugha ya kukatisha tamaa kwa wateja ili kujenga mahusiano mazuri na wateja jambo litakalopelekea kupanua wigo wa wateja na kuongeza mapato kwa Shirika.
” Masurveyor ndio wanaolalamikiwa sana kwa kutoa lugha zinazokatisha tama, ninawasihi mbadilike kuanzia sasa, atakayebainika anatumia lugha mbaya kwa mteja, huyo tutaachana naye na atachukuliwa hatua za kinidhamu. Wateja wote wahudumiwe bila kubaguliwa, tunataka wateja wote wapate umeme bila kubaguliwa.”Amesema Dkt. Kalemani
Aidha, Dkt. Kalemani, amewapongeza watumishi wa TANESCO kwa utendaji mzuri na kueleza kuwa kwa zaidi ya asilimia 80 utendaji wa TANESCO ni wa Kuridhisha.
Waziri Kalemani pia ameelekeza watumishi walioajiriwa kwa muda, wanaohusika na kazi za kupimia wananchi maeneo ya kuunganisha umeme, wanunuliwe pikipiki zitakazowawezesha kuwafikia wateja kwa urahisi.
Vilevile, Waziri Kalemani amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na kwa usahihi na amewataka watumishi wa TANESCO na REA kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi hicho, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, amewataka watumishi wote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Kalemani, na kueleza kuwa atahakikisha anasimamia na kufuatilia utekelezaji wake kwa ukamilifu.
Kikao kazi baina ya Waziri Kalemani na watumishi wa TANESCO na REA, ni kikao kazi cha pili baada ya kufanya kikao na wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Geita wiki iliyopita. Lengo la vikao hivyo ni kuweka misingi ya pamoja ya utendaji kazi unaolenga kuleta matokeo chanya na ya haraka katika Sekta ya Nishati.
By Mpekuzi
Post a Comment