Vita Ya Magonjwa Yasiyoambukiza Inahitaji Juhudi Za Kila Mmoja Wetu” – Mganga Mkuu Wa Serikali |Shamteeblog.


Na Englibert Kayombo WAMJW – GEITA
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amesema juhudi za kila mwananchi mmoja mmoja zinahitajika ili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kubadili mtindo bora wa maisha, ulaji wa chakula bora pamoja na kufanya mazoezi.

Prof. Makubi amesema hayo akiwa kwenye kikao cha viongozi ndani ya Mkoa wa Geita kilichofanyika mkoani huyo kujadili miundombinu ya sekta ya afya.

“Sasa tumeingia katika vita nyingine ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, magonjwa haya hayana dalili ya kukushtua kwenda Hospitali, haya ni hatari zaidi kuliko yale magonjwa ya kuambukiza” amesema Prof Makubi.

Amesema dalili za magonjwa yasiyo ya kuambukiza huwa hazijitokezi kwa haraka zaidi hivyo mtu huwa anajiona kuwa yuko salama ili hali akiwa mgonjwa ambapo dalili huja baadae kwa uzito mkubwa na mtu huwa amechelewa kuanza kupata matibabu.

“Magonjwa ambayo ni ya kuambuzika yana dalili, utajisikia homa au uchovu, magonjwa yasiyoambukiza hayana hizo dalili za kukushtua kwenda hospitali, utaanza kuona matatizo baadae na kugundulika moyo au figo imefeli, hizo ndo dalili za kwanza” amefafanua Prof. Makubi

Prof. Makubi amesema ni lazima tuelewe magonjwa hayo kama vile presha, moyo, kisukari, kufeli kwa figo ni hatari kuliko hata yale ya kuambuza yakiwemo Malaria, Ukimwi na Kifua Kikuu ambapo mtu asipojitambua mapema kufanya vipimo, kubadilisha tabia, mwenendo wa chakula huishia kuathirika kiuchumi yeye na familia yake kwa kuwa magonjwa hayo yana gharama kubwa za matibabu.

“Usipojitambua mapema kufanya vipimo, kubadilisha mtindo wa maisha na mwenendo wa chakula utajikuta uko kijana wa umri wa miaka 30 hadi 50 unapata matatizo ambayo yatakufanya ushindwe kushiriki katika majukumu yako ya uzalishaji na kuiingiza serikali katika gharama kubwa ya kukuhudumia” amesema Prof. Makubi

Amesisitiza wananchi kubadili mtindo wa maisha, mwenendo wa chakula na kuzingatia kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kupambana na magonjwa hayo ambayo yameshika kasi hasa kwa vijana na watu wazima.

“Zamani tulikuwa tunafanya mazoezi, tunalima, tunaendesha baiskeli, kutembea sasa hivi hatufanyi hivyo na ndio maana tumejikuta tunapata haya matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza kwa haraka sana, tufanye mazoezi na kubadilisha mtindo wa maisha yetu tunayoishi sasa na kuzingatia mwenendo bora wa vyakula vyetu” amesisitiza Prof. Makubi

Aidha, amewataka viongozi hao kuendelea kutoa elimu ya afya kwa wananchi ili kuweza kubadilisha mtindo wa maisha na wananchi hao waanze kujenga mazoea ya kupima afya zao mara kwa mara ili kutambua dalili za haraka za magonjwa hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi. Robert Gabriel amewataka wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa hayo

“Tumeambiwa maisha yamebadilika, mazoezi ndio mpango mzima wa afya, tumekuwa ‘busy’ mno kila siku kwenye magari maisha yamebadilika na magonjwa haya yasiyoambukiza huja na mtetemo mkubwa na kupona huwa ni shida, tukumbushane na kubadilika ili tuweze kupambana na magonjwa hayo” Amesisitiza Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Mhe. Robert Gabriel ametoa wito kwa wananchi kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kubadili mtindo wa maisha kuepukana na magonjwa hayo ambayo amesema huathiri uchumi wa familia na nchi kuingia gharama kubwa ya matibabu.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post