Na Damian Masyenene, Shinyanga
Mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Paulina Daud (30) mkazi wa Mageuzi kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mme wake kutokana na ugomvi wa kifamilia.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana Januari 26, 2021 saa 3:00 asubuhi, ambapo marehemu akiwa nyumbani alishambuliwa kwa kupigwa ngumi na mchi mdogo (mtwangio) sehemu mbalimbali za mwili wake na mume wake aitwaye Samwel James.
Kamanda Magiligimba ameeleza kuwa Mwanamke huyo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga, ambapo mtuhumiwa alikimbia mara baada ya tukio hilo na juhudi za kumtafuta na kumkamata zinaendelea.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wanandoa kuacha mara moja tabia ya kuwashambulia wenza wao, huku akiwasihi wanawake wanaofanyiwa vitendo vya ukatili kuvunja ukimya na kueleza changamoto wanazokabiliana nazo.
“Niwaombe wanawake wote wanaofanyiwa vitendo vya ukatili mkoani shinyanga wavunje ukimya wafunguke ili matatizo yao ya kifamilia yaweze kushugulikiwa yakiwa katika hatua za awali kabla madhara makubwa hayajatokea kwani vitendo vya ukatili ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine,” amesisitiza.
from Author
Post a Comment