Breaking : BENARD MEMBE AIPIGA CHINI ACT WAZALENDO |Shamteeblog.


Aliyekuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo na mshauri wa Chama hicho, Bernad Membe leo Januari 1,2021 ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama hicho.

Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kati ya 2007 hadi 2015 ametangaza uamuzi huo leo akiwa nyumbani kwake kijijini Rondo Chiponda, Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi ambapo amesema hajafanya uamuzi huo kwa shinikizo lolote na kwamba kwa sasa atakuwa mshauri wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi ya Tanzania na kupigania demokrasia ya kweli.

Mwanadiplomasia huyo alitangaza kuhamia Chama cha ACT Wazalendo miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2020 baada ya kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 28 Februari 2020 na Kamati Kuu ya chama hicho, kisha uamuzi huo kubarikiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), tarehe 10 Julai 2020.

Membe alifukuzwa kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya CCM, pamoja na kuonywa mara kadhaa, pasina kubadilika.

Baada ya kuhamia ACT Wazalengo, Membe alitangaza kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Akijiunga ACT Wazalengo Membe alisema ; “Kwa hiari yangu nimeamua kujiunga katika familia kubwa ya ACT Wazalendo inayotaka mabadiliko yenye lengo la kuwanufaisha Watanzania wengi hasa wakulima, wafanyabiashara, watumishi wa serikali, wafanyakazi mbalimbali na wote wanaoitakia kheri Tanzania yetu. Nataka kupigania mabadiliko ya kweli ya hii nchi kupitia ACT na azma yangu itatimia".

Hata hivyo kuliibuka migogoro ndani ya chama hicho baada ya Viongozi wa ACT Kutangaza kumuunga mkono Mgombea Urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu licha ya Membe kuwa mgombea Urais kupitia ACT Wazalendo.

Ijumaa Oktoba 16, 2020 Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alitangaza kumpigia kura mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni mjini Kigoma.

Mbali na Zitto, Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad aliwahi kutangaza kuwa chama hicho kitamuunga mkono Lissu katika Urais ambapo pia Lissu pia aliwahi kutangaza kuwa Chadema itamuunga mkono Maalim Seif katika urais wa Zanzibar.

Hata hivyo Membe alisisitiza kuwa yeye ni mgombea halali wa Urais kupitia ACT Wazalendo.

“Mimi Bernard Membe ni mgombea halali wa ACT-Wazalendo wa nafasi ya Urais. Na chama chetu ni kizuri kabisa ambacho nitakipeleka 28 Oktoba 2020 vizuri kabisa”,alisema.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post