Hospitali ya Elidad kutoa matibabu bure siku ya Mapinduzi ya Zanzibar |Shamteeblog.

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Hospitali ya Elidad ya Boko Basihaya jijini Dar es salaam itaadhimisha sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar (Januari 12)  kwa kufanya vipimo vya afya bure kupitia kampeni ya Afya Bure.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospiatli hiyo Dk Harry Matoyo alisema kuwa zoezi hili litafanyika Jumanne ijayo hospitalini hapo na siku hiyo watafanya uchunguzi wa magonjwa tofauti na kuwapa matibabu ya awali.

DK Matoyo alisema kuwa zoezi hilo litafanyika kuanzia asubuhi  na watafanya uchuguzi wa magonjwa ya mifupa na viungo, uchunguzi wa magonjwa ya moyo na uchunguzi wa magonjwa wa kisukari.

Alisema kuwa wameamua kuadhimisha sikukuu hiyo kwa kutoa huduma bure ili kuunga mkono jitihada za Rais Dk John Magufuli za kuondoa adui maradhi ambayo serikali haitaweza kufanya peke yake.

 “Kuona kuwa serikali inapambana na adau maradhi, hospitali ya Elidad iliamua kuunga mkono serikali kwa kuanzisha Afya Bure Kampeni kwa lengo la kupambana na adui maradhi na kulijenga taifa lenye raia wenye afya njema,” alisema Dk Matoyo.

Alisema kuwa huduma ya vipimo na matibabu ya awali yataolewa kwa watu wenye rika zote na kuwataka wananchi kujitokeza siku hiyo kwani watakuwa na timu ya madakari wa kutosha.

Alisema kuwa hospitali ya Elidad ilianza mwezi Juni mwaka jana na kutoa matibabu ya magonjwa ya ujumla lakini ikijikita zaidi kwenye magonjwa ya mifupa yatokanayo na ajali na yasiyo ya ajali.

“Pia tunatoa huduma za dharura (emergency), maabara, huduma za duka la dawa,  huduma za physiotherapy,  huduma za wagonjwa wa nje (opd), huduma za wagonjwa wa kulazwa (ipd), x ray, ultrasound, upasuaji wa aina mbalimbali na huduma za kutoa ushauri nasaa (counselling,” alisema dk Matoyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Utabibu wa hospitali hiyo Dk Cynthia Bashaija alisema kuwa kwa muda mfupi tangu waanze kutoa huduma wameweza kutambua kuwa siyo kila mtanzania ana uwezo wa kujifanyia uchunguzi na kuweza kutambua au kugundua magonjwa mbalimbali yakiwa katika hatua ya awali.

Dk Bashaija alisema kuwa wagonjwa wengi wamekuwa wakienda katika hospitali yao wakiwa katika hatua mbaya za mwisho na hivyo kufanya huduma za uponyaji kuwa ngumu na gharama zaidi.

“Aidha wapo wana nchi ambao hawaji hospitali kwa kuwa hawana uwezo na wengine ni kwasababu ya kupuuzia au uelewa mdogo.  Kwa kuzingatia hilo, hospitali ya elidad imeona ina wajibu wa kuona taifa la Tanzania linakuwa na afya bora na kuanzisha kampeni hiyo,” alisema Dk Bashaija.

Alisema kuwa upimaji huo pia utahusisha kupima sukari, uzito, urefu, BMI, shinikizo la damu na magonjwa ya mifupa na hasa mgongo na magoti. Aliongeza kuwa zoezi hili lina lenga kugundua magonjwa hatua za awali na namna ya kuzuia hivyo haitahusisha gharama za matibabu hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Elidad ya Boko Basihaya jijini Dar es Salaam Dk Harry Matoyo akizungumzia kampeni ya kupima vya afya bure ambayo itafanyika Januari 12 kwenye hospitali yao.

Mkuu wa Utabibu wa hospitali ya Elidad Dk Cynthia Bashaija akizungumzia kampeni hiyo ambayo wagonjwa wenye matatizo mbalimbali watapatiwa huduma ta vipimo na ushauri bure.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Elidad ya Boko Basihaya jijini Dar es Salaam Dk Harry Matoyo (kulia) akifafanua jambo wakati wa kutangaza kampeni ya Afya Bure ambayo hospitali hiyo itafanya kwa wananchi wote. Pembeni yake ni Mkuu wa Utabibu wa hospitali hiyo Dk Cynthia Bashaija.

Muonekano wa jengo la Hospitali ya Elidad ya Boko Basihaya jijini Dar es Salaam




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post