Kalemani azindua mradi usambazaji gesi majumbani Sinza |Shamteeblog.

Na Faraja Masinde, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amezindua mradi wa usambazaji wa gesi asilia majumbani katika mtaa wa Nzasa, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Mradi huo uliozinduliwa Januari 23, 2021 unahusisha kuunganisha wateja 506, kati yao wateja 170 wako eneo la Nzasa, Kijitonyama, na 336 katika eneo la Polisi Barracks-Mgulani.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Waziri Kalemani amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kuhakikisha linaongeza kasi katika kutekeleza mradi huo.

“Mmeeleza kuwa mradi huu utachukua hadi miezi 12 kukamilika, naomba utekelezaji uanze haraka na mhakikishe mradi umekamilika ndani ya miezi sita, ili watu waanze kutumia rasilimali hii majumbani kwao,” amesema Dk. Kalemani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk. James Mataragio ameeleza kuwa mradi utagharimu fedha za kitanzania takriban Sh bilioni 2 na kwamba bomba hilo la kusambaza gesi asilia katika maeneo ya Sinza litakapokamilika, litakuwa na uwezo wa kusambaza gesi kwa zaidi ya nyumba 1,000.

Amesema katika mwaka huu wa fedha 2020/21, Shirika limetenga Sh bilioni 10 kwa ajili ya kuunganisha wateja wa majumbani wapatao 1,000 katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.

“Kwa Mwaka ujao wa fedha Shirika limepanga kutekeleza uunganishaji wa wateja wengine wapya 300 katika Jiji la Dar es Salaam,” amesema Dk. Mataragio.

Aidha ameeleza kuwa matumizi ya gesi hiyo ni rahisi kwani mteja ataunganishwa na kuwekewa mita ambayo ataitumia kufuatilia matumizi yake na kununua rasilimali hiyo kwa njia ya mtandao kama ilivyo kwa luku za umeme.

“Kama ilivyo kwa luku, mteja atalipia gesi hii kwa kadri ya matumizi yake, na atanunua kwa kiasi cha uniti kwa utaratibu unaojulikana kama malipo kabla ya kutumia (pre-paid),” aliongeza.

kwa mujibu wa TPDC hadi sasa kiasi cha gesi asilia kipatacho futi za ujazo trilioni 57.54 zimegundulika hapa nchini. Gesi hii inatumika kwa kuzalisha umeme, viwandani, majumbani pamoja na kwenye magari.

Shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini zinaendelea kwa kupitia makampuni ya kimataifa ya mafuta pamoja na TPDC, chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post