Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Tarime wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani kwenye ukumbi katika shule ya Sekondari JK Nyerere iliyopo kijiji cha Nyamwaga kata ya Nyamwaga
Na Dinna Maningo,Tarime
Madiwani wamempa miezi sita Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa kuhakikisha anajenga ukumbi wa kufanyia vikao vya Baraza la Madiwani nakwamba hawawezi kuendelea kufanya vikao kwenye ukumbi wa chakula na kukalia viti vya wanafunzi katika shule ya Sekondari JK Nyerere iliyopo Kijiji cha Nyamwaga kata ya Nyamwaga wilayani Tarime.
Ilikuwa ni vuta ni kuvute jana kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ambapo Madiwani walimtaka Mkurugenzi huyo kuwapatia viti na meza mali ya halmashauri na siyo kuketi kwenye viti vya wanafunzi huku wakiwa hawana meza za kuweka makablasha yao nakulazimika kuweka makablasha kwenye magoti.
Diwani wa kata ya Manga Steven Gibai alisema"Mkurugenzi tunataka utuletee meza na viti vyetu,madiwani hatuwezi kukalia viti vya wanafunzi istoshe huu ukumbi ndiyo wanaotumia wanafunzi kwa ajili ya chakula,kusomea na kufanya mtihani kukalia viti vya wanafunzi ni kutuondolea heshima".
Diwani wa Kata ya Regicheli John Bosco alimtaka Mkurugenzi kutafuta eneo jingine halmashauri kujenga ukumbi mdogo wakati huo unafanyika mchakato wa kujenga majengo ya halmashauri.
"Mkurugenzi atenge eneo ujengwe ukumbi mdogo wakati huo wanafanya mchakato wa kujenga majengo ya halmashauri hatuwezi kusubiri wakati hatujui hayo majengo yataisha lini,inaweza chukua hata miaka mitatu bado tukiendelea kufanya vikao shuleni na kukaa kwenye viti vya wanafunzi", alisema Bosco.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa alisema kuwa awali makao makuu ya halmashauri yalikuwa mjini Tarime na baada ya Rais John Magufuli kuzitaka halmashauri kuhamia kwenye maeneo yao ya utawala,Octoba,21,2019 walihamishia makao makuu ya halmashauri katika kijiji cha Nyamwaga kata ya Nyamwaga.
Tindwa alisema kuwa kwa sasa halmashauri hiyo inatumia majengo ya ofisi ya kijiji na kwamba tayali Serikali imetoa fedha zaidi ya Bilioni moja kujenga jengo la utawala na aliwaomba madiwani kumpatia muda wa miezi mitatu kujenga ukumbi wakufanyia mikutano.
"Kutokana na miundombinu ya barabara inakuwa vigumu kuleta meza na viti kila kikao tuwe tunavisafirisha vitaharibika,hata sisi tunatumia majengo ya ofisi ya kijiji,tayali tumeshapokea fedha Billion moja tutaanza kujenga ukumbi,Mwenyekiti naomba mnipatie miezi mitatu ntakuwa nimekamilisha ukumbi", alisema Tindwa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani wa kata ya Nyakonga Simion Samwel aliwaomba madiwani kumpa muda Mkurugenzi kwakuwa tayali kuna fedha, ambapo alimpatia miezi sita kukamilisha ukumbi na endapo usipokamilika madiwani watahoji kwenye vikao sababu za kuwadanganya kwa kutotokeleza ahadi yake ambapo madiwani wote walikubali kumpa muda huo.
By Mpekuzi
Post a Comment