MAHAKAMA WILAYANI LUDEWA YAWATAKA WAZAZI KUTOKOMEZA UBAKAJI KWA WATOTO. |Shamteeblog.


Na Shukrani Kawogo, Njombe.

Ikiwa ni wiki ya sheria hapa nchini ambayo imeanza kuadhimishwa January 23 na kilele chake ni January 30 Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Amon Kahimba, amewataka wazazi pamoja na jamii kwa ujumla kushirikiana kutokomeza vitendo vya ubakaji kwa watoto na wanafunzi ambavyo vinaonekana kukithiri katika wilaya hiyo na kuhakikisha kuwa watuhumiwa hao wanapatiwa adhabu stahiki.

 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kahimba amesema kumekuwa na wimbi kubwa la kesi za ubakaji pamoja na mimba kwa wanafunzi ambazo hujitokeza ndani ya wilaya hiyo huku baadhi ya watuhumiwa ni watumishi wa umma wakiwemo walimu ambao ndio wamepewa dhamana ya kuwalea watoto hao kutoka kwa wazazi wamekuwa wakifanya mazungumzo na familia mwisho mashauri hayo huishia kufutwa kutokana na walalamikaji kutotokea mahakamani.


Amesema kuwa kesi za namna hiyo zinapojitokeza zimekuwa zikicheleweshwa kuripotiwa kituo cha polisi kutokana na wazazi hao kufanya mazungumzo kwanza na wanaposhindwana ndipo hupeleka shitaka hilo polisi kitu ambacho kwa wakati huo wanakuwa wamekwisha poteza baadhi ya ushahidi hasa wa vipimo.

Amesema kinachomsikitisha zaidi baadhi ya watuhumiwa wengine ni watumishi wa serikali wakiwemo walimu ambao ndio wamepewa dhamana ya kuwatunza watoto lakini wao ndio wamekuwa wakwanza kuwaharibu watoto hao na mwishowe kesi huisha bila kuchululiwa hatua yoyote.

Amesema hadi kesi hizo zinawasilishwa mahakamani  bado wamekuwa wakiendelea na majadiliano majumbani na wanapofikia muafaka mshitaki hatokei mahakani au anaweza kufika lakini anabadili maelezo kuwa anayeshitakiwa si muhusika sahihi wa kesi hiyo na kupelekea mtuhumiwa kuachiwa huru.

"Tumefuta kesi nyingi sana kutokana na washitaki au mashahidi kutotokea mahakamani, hadi tunalazimika kufunga jalada ukipita mitaani unawakuta mshitaki na mshitakiwa wanatembea na kula pamoja", alisema  Kahimba.

Aidha wakati huo huo Kahimba amewataka wakazi wa Ludewa  kuacha kuuana kwa mambo ya kishirikina au wivu wa mapenzi kwani kwa kufanya hivyo ni kumkosea Mungu na serikali pia.

Amesema watu wamekuwa wakiuana kwa imani hizo hasa anapoona mambo yake hayaendi wanaanza kuhisi mtu fulani ndo kaniroga ndo maana mambo hayaendi na kupelekea kuchukua sheria mkononi ya kumuua mtu anayemuhisi kitu ambacho ni kosa kisheria na adhabu yake ni kifungo cha maisha.

Ameongeza kuwa katika wiki hii ya sheria, wameamua kutoa elimu kwa jamii kuhusu sheria mbalimbali ili waweze kupata uelewa katika masuala haya na kuzitambua haki zao ambapo wameweka vituo 10 katikati maeneo mbalimbali ili kutoa elimu hiyo na msaada kisheria.

Amesema sambamba na kutoa elimu kwa wananchi pia wameandaa mechi ya mpira wa miguu kati ya watumishi wa umma na wananchi ambayo itachezwa siku ya ijumaa January 29 ambapo mshindi wa mechi hiyo atakabidhiwa zawadi ya mbuzi.

Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Amon Kahimba alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari.

 


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post