Na Shukrani Kawogo, Njombe.
Katika kuuaga mwaka mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ameshiriki na wananchi katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa kwenye shule ya msingi Mbongo sambamba na kuchangia mifuko 100 ya saruji kwaajili ya shule hiyo na shule ya sekondari Manda.
Pamoja na kuchangia mifuko hiyo ya saruji mbunge huyo ametoa fedha taslimu laki tisa kwaajili ya ununuzi wa bati za kumalizia uezekaji wa ofisi ya kijiji cha Mbongo huku akiahidi kuchangia milioni moja kwaajili ya madawati katika shule ya sekondari Mchuchuma.
Vyumba hivyo viwili vya madarasa vinajengwa kwa nguvu ya wanaludewa wanaoishi ndani na nje ya wilaya ambao wameunda kundi la Whatsapp linalojadili Maendeleo ya wilaya na kuchangishana fedha kwa ajili ya kuboresha Maendeleo mbalimbali ya Wilayani yao pamoja na kundi la Mbongo family.
Mbunge huyo akiwa ni mmoja wa kundi hilo la Whatsapp la wilaya ya Ludewa amesema licha ya kutoa mchango ndani ya kundi lakini ameona aongeze mchango wake wa mifuko hiyo ya saruji ili kuhakikisha ujenzi huo unaenda bila kukwama.
Aidha ameyashukuru makundi hayo kwa kuonyesha ushirikiano wao katika kuleta maendeleo katika wilaya hiyo na kuwasihi kuendelea kujitoa katika kuleta maendeleo zaidi hata katika maeneo mengine ya wilaya hiyo yenye changamoto.
" Napenda niwashukuru Sana kundi la wilaya ya Ludewa pamoja na kundi la Mbongo family ambayo yametoa mchango mkubwa sana katika ujenzi huu wa madarasa haya, nami ni mmoja wa kundi la wilaya hivyo ninaimani kundi langu hili litaendeleza kuchangia Maendeleo ya wilaya yetu hata katika maeneo mengine pia", alisema Kamonga.
Naye mmoja wa kundi la Mbongo family alifika kuangalia maendeleo ya ujenzi huo kutokea jijini Dar es Salaam akiwakilisha kundi lake Obed Kasambara amesema wanatarajia ujenzi huu utakamilika haraka ili madarasa hayo yaanze kutumiwa hivyo amewaomba wanakikundi wenzie kuendeleza michango ili waweze kufikia malengo.
Pia amemuomba mhandisi wa majengo na timu yake kutoka wilayani kufika kwa wakati pale wanapohitajika ili ujenzi huo uende kwa haraka maana wanapochelewa kwenda kukagua husababisha ujenzi huo kwenda taratibu.
" Mimi nimefika hapa nimekuta msingi umesha jengwa na ujenzi unaendelea kwa hatua nyingine, lakini jana mhandisi alipokuja akasema msingi upo chini Sana hivyo unatakiwa kupandishwa zaidi kwahiyo endapo wangekuja kukagua mapema sasa hivi tungekuwa tunaendelea na hatua nyingine badala ya kupandisha msingi", alisema Kasambara.
Naye mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mbongo Joseph Mapunda amewashukuru wadau wote wanaojitoa katika ujenzi huo na kuongeza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa saruji hivyo anaomba wadau hao kuendeleza michango yao ili waweze kupata saruji.
Amesema kwa upande wa wanakijiji wanajitoa sana katika kuchangia nguvu kazi ambapo wamekuwa wakichota maji, kusogeza mawe, mchanga na shughuli nyinginezo.
Aidha kwa upande wa mmoja wa wanachi wa kijiji hicho Chedi Mapunda amewashukuru makundi yote yanayotoa michango ya ujenzi huo na kusema kuwa madarasa hayo yatakuwa msaada mkubwa sana kwa watoto wao kwani madarasa wanayotumia Sasa ni machakavu.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akimimina mchanga kwaajili ya kuvhanganyia saruji wakati akishiriki ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Mbongo iliyopo kata ya Manda wilayani Ludewa.
Aliyetamgulia ni Mwenyekiti wa kijiji cha Mbongo Joseph Mapunda akimuongoza mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga pamoja na wananchi kumuonyesha jengo la ofisi ya kijiji ambalo bado halijamaliziwa.
Mmoja wa kundi la Whatsapp la Mbongo family (kulia) akihakiki fedha alizotoa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kushoto) huku wakishirikiana kuhesabu fedha hizo na mwenyekiti wa kijiji hicho Joseph Mapunda (wakati kati).
Mwenyekiti wa kijiji cha Mbongo Joseph Mapunda(kushoto) akimuonyesha mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga, eneo lililopelea bati katika jengo la ofisi ya kijiji ambapo mbunge hiyo alitoa hapo hapo kiasi cha shilingi laki 9 kwaajili ya ununuzi wa bati hizo.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Mbongo iliyopo katika kata ya Manda ambapo kwa sasa wapo katika hatua ya kuinua msingi.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga, akiwa ameongozana na wananchi wa kijiji cha Mbongo wakikagua miradi mbalimbali ya ujenzi iliyopo katika kijiji hicho.
By Mpekuzi
Post a Comment