Mzee mwenye miaka 75, amerejea nyumbani kwao katika kijiji cha Kolait, Teso Kaskazini, kaunti ya Busia nchini Kenya baada ya kutoweka kwa miaka 46 kutafuta ajira.
Francis Indek Arachabon anaripotiwa kuondoka nyumbani kwao mwaka 1975, akiwa na miaka 29 akielekea Kimilili kumtembelea mjomba wake lakini aliamua kurefusha safari yake hadi Soy kutafuta ajira ambapo alipoteza mawasiliano na familia yake.
Kwa mujibu wa Nation, familia yake ilimtafuta kwa jamaa zake, vituo vya polisi na hata katika hifadhi ya maiti.
Lakini baada ya miaka 46, Arachabon alirejea nyumbani mnamo Jumapili, Januari 17,2021 na alipokelewa na kaka yake mwenye miaka 71, Erneo Okadapao.
Okadapao aliongezea kuwa mchungaji mmoja kutoka nchini Uganda alimuahidi kuwa kaka yake atarejea na kweli unabii huo umetimia.
Arachabon alisema kwa miaka ambayo alitoweka, alimuoa Susan Tabolei na wamejaliwa watoto watatu na ni kutokana na familia yake mpya ndio ilimchochea kufuta mawazo ya kurejea nyumbani.
Mzee huyo aliongezea kuwa alikuwa akilima mashamba ya watu na kufanya vibarua vingine vidogo ili kujichumia riziki.
Katika taarifa tofauti, wakazi wa kijiji cha Nabisiongo, eneo bunge la Matayos katika kaunti ya Busia walishtuka baada ya mwanamume aliyedhaniwa kufariki na kuzikwa kujitokeza miezi minne baadaye.
Familia ya Steven Ogolla ilikuwa imeandaa mazishi yake baada ya kutoweka kwa miezi minne. Kaka yake Ogolla, Steven Ouma alichana mbuga akidhania kuwa ameona zimwi kwani walikuwa wamemzika.
By Mpekuzi
Post a Comment