Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema ipo mbioni kuajiri walimu wapya 5,000 kwa Shule za Msingi na Sekondari ikiwa ni muendelezo wa ahadi aliyoitoa Rais Dk John Magufuli mwaka jana ya kuajiri walimu 13,000 nchi nzima.
Akizungumza katika mkutano wa pili wa umoja wa Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (Tapsha), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema walimu hao watakaojiriwa watapelekwa kwenye zile shule zenye uhitaji na hasa za vijijini.
Mhandisi Nyamhanga amewataka walimu wakuu ambao watawapokea walimu hao wapya wajitahidi kuwaelekeza maadili ya ualimu pamoja na kuwasimamia ili waweze kuwa walimu bora watakaolea na kutoa elimu bora kwa wanafunzi wanaowafundisha.
Katibu Mkuu Nyamhanga ametoa onyo pia kwa walimu wote ambao wamekua wakihusika na uvujaji wa mitihani ambao amesema kitendo hiko ni kukiuka miiko na maadili ya kazi yao huku akiahidi kuwa serikali itawashughulikia wale wote wenye tabia hizo.
" Serikali tunalaani sana vitendo hivi vya uvujaji wa mitihani ambavyo vinafanywa na walimu wetu, yeyote ambaye tutambaini hatutomvumilia na sheria itachukua mkondo wake, niwasihi kupitia mkutano huu mkawe sehemu ya kukemea vitendo hivi.
Ni jambo la kusikitisha kuona walimu wanahusika na uvujaji wa mitihani, mwaka jana zaidi ya wanafunzi 1,000 tuliwafutia matokeo yao kwa sababu ya kashfa hii ya mitihani, na walimu baadhi ndio waliohusika na uvujaji huu na kuwaharibia maisha wanafunzi hao," Amesema Mhandisi Nyamhanga.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na walimu nchini lakini bado wapo walimu wachache wanaoharibu taswira ya walimu nchini kwa kujihusisha na vitendo vya uvujaji wa mitihani pamoja na kushindwa kusimamia miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali kwenye shule zao.
Amewataka walimu hao kutumia jukwaa hilo la siku tatu kujadili pia mienendo yao kama walimu na kusahishana wenyewe ili kuendelea kuwa na walimu wanaojua weledi wao na kusimamia miiko na maadili ya kazi yao.
Nae Mwenyekiti wa TAPSHA, Rehema Ramole ameipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli kwa kuboresha sekta ya Elimu nchini ikiwemo kujenga miundombinu mizuri ya madarasa, vyoo na nyumba za walimu.
" Tunamshukuru sana Rais wetu Dk Magufuli kwa kututhamini sana walimu, licha ya janga kubwa la Corona mwaka jana lililopelekea shule kufungwa lakini bado aliendelea kutulipa mishahara yetu kama kawaida, tunamuahidi kuwa tuko pamoja nae na tunamuombea kwa Mungu azidi kumpa afya njema," Amesema Mwl Ramole.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mhandisi Joseph Nyamhanga akizungumza na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara katika mkutano wao unaoendelea jijini Dodoma.
Walimu Wakuu kutoka Mikoa Mbalimbali ya Tanzania Bara wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mhandisi Joseph Nyamhanga wakati wa Mkutano wao unaofanyika jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli akizungumza katika mkutano wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara unaofanyika Dodoma kwa siku tatu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (TAPSHA) Rehema Ramole akisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi kwenye mkutano wao unaofanyika jijini Dodoma kwa siku tatu.
By Mpekuzi
Post a Comment