Na Amiri Kilagalila,Njombe
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) mkoa wa Njombe,iko tayari kuwachukulia hatua waajili wanaokwepa kuwasilisha makato ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Njombe Kassim Ephrem wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi ya mwezi Oktoba hadi Disemba 2020,amesema katika utekelezaji wa majukumu yao wamepata taarifa juu ya wadaiwa wa taasisi,mamlaka au wakala wa serikali wasiolipa madeni yao kwa wakati hatua inayowalazimu kuanza kufuatilia wadaiwa hao.
“Tunaomba waajili wote wanaopaswa kupeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi kama NSSF,walioikata kutoka kwa watumishi wahakikishe wanaiwasilisha haraka,na ni vizuri kwa watumishi mhakikishe mnawasiliana mara kwa mara kuhakikisha michango yenu je inawasilishwa? Na kama haiwasilishwi njoo tupe taarifa mapema tuchukue hatua kwasababu ni haki michango yenu kuwasilishwa sehemu husika”alisema Kassim Ephrem
Amesema ni wajibu kwa waajili kupeleka makato ya watumishi kwenye mifuko ikiwemo NSSF na PSPF,kwa mkoa wa Njombe kwa kuwa kutofanya hivyo ni kuwadhulumu wafanyakazi.
Vile vile amesema wameendelea kufuatilia fedha za umma kwenye miradi ya maendeleo (Pets) na kuweza kukagua miradi mbali mbali ikiwemo ya afya,elimu na maji yenye thamani ya shilingi 4,146,020572.42 kwenye halmashauri zote 6 za mkoa wa Njombe.
Mbali na ufuatiliaji huo amesema wameendelea kushirikina na na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika operesheni ya urejeshaji wa fedha zilizokuwa zimekopwa na wanachama au kufanyiwa ubadhirifu na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika vya AMCOS,SACCOS na NJOCOBA.
“Katika utekelezaji wa jambo hilo kuanzia tarehe 23/10/2020 hadi 31/12/2020 tumefanikiwa kuokoa kiasi cha shs.10269,430/= kutoka AMCOS na SACCOS na shs. 5,426,646/= kutoka NJOCOBA hivyo kufanya jumla ya fedha zilizookolewa kwa kipindi hicho kuwa shilingi 15,696,076/=” alisema Kassim Ephrem
Aidha amesema kwa kutambua umuhimu wa kutoa elimu juu ya rushwa katika jamii,wameanzisha utaratibu wa Mobile PCCB yaani Takukuru inayotembea kwa kutenga siku moja kila mwezi huku ikiwafuata wananchi mitaani kwa lengo la kusikiliza pamoja na kutatua kero zao,ambapo kwa mkoa wa Njombe wameweza kusikiliza kero tarehe 22 katika mtaa wa Maheve mjini Njombe.
By Mpekuzi
Post a Comment