TEMBO WAUA SITA, WAJERUHI SABA |Shamteeblog.





Mmoja ya mwathirika aliyejeruhiwa na Tembo, Lobulu Mollel Mkazi wa Kijiji Cha Monduli juu, wilayani Monduli, akionyesha mguu wake  wa kulia uliojeruhiwa na Tembo na kunusurika kifo miezi miwili iliyopita(picha na Woinde shizza.)


Na Woinde Shizza,Arusha
WANANCHI Sita wameuawa na wengine saba kujeruhiwa vibaya kwa kushambuliwa na Tembo katika Kijiji Cha Makuyuni wilaya ya Monduli ,Mkoani Arusha katika kipindi cha miaka miwili na kusababisha wakazi wa Kijiji hicho kuishi kwa hofu.

Aidha Tembo hao wanadaiwa kuvamia pia mashamba ya wananchi hao na kufanya uharibifu wa mazao yao jambo lililosababisha wakose chakula katika kipindi Cha miaka miwili na kuishi maisha ya tabu.

Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa Kijiji Cha Makuyuni,wilayani humo Ngayoo Measi katika mazishi ya Mkazi mmoja wa Kijiji hicho, Ester Sindiyo (55) aliyeuawa na Tembo Desemba 21 mwaka huu wakati akiokota kuni na kuiomba serikali kusaidia kuwaondoa Tembo hao.

Amesema Vifo hivyo na majeruhi vimetokana na makundi ya Tembo yanayovinjari Kijijini hapo nyakati za usiku huku kukiwa hakuna jitihada zozote zinazochukuliwa na serikali katika kuwadhibiti wanyama hao wanaotoroka kutoka hifadhi ya Tarangire na Manyara kusaka malisho. 

Mwenyekiti huyo aliwataja marehemu waliouawa na Tembo kwa nyakati tofauti kuwa ni Janeth Silla,Mamalai Kakuyu, Lemomo Lenguriny, Kastuli Jumalei, Emanuel Leroo na Ester Sindiyo wote wakazi wa Kijiji hicho.

Pia aliwataja majeruhi wa tembo hao kuwa ni Lobulu Mollel, Julius Thobias ,Saiguran Mika, Mnyak Lenguriny,Mjomba Soingei bado amelazwa katika hospital ya rufaa KCMC, Lobikyeki Sanare na Kalai Lomayani wote wakazi wa Kijiji Cha Makuyuni na kwamba taarifa za matukio hayo wamekuwa wakizitoa katika ngazi mbalimbali.

Naye diwani wa kata hiyo Elius Odupoi aliwataka wananchi kuchukua tahadhali ya kujilinda wenyewe na kuacha kutembea nyakati za usiku ikiwemo kufanya shughuli za kijamii majira ya usiku.

"Watu wetu wanauawa na Tembo na wengine wanajeruhiwa tunaendelea kuikumbusha serikali iongeze nguvu ya kudhibiti Hawa Tembo ,na sisi wananchi tupunguze kufanya shughuli zetu nyakati za usiku na suala la ulinzi linaanza na sisi."alisema Diwani.

Mmoja ya mwananchi wa Kijiji hicho,Peter Laisangai alimeiomba serikali kuongeza fidia kwa wahanga wa wanyamapori kwani kiasi cha Sasa kinachotolewa na serikali Cha sh.500,000 kwa aliyejeruhiwa na shilingi 1,000,000 kwa aliyefariki ni kidogo .

"Tunaiomba serikali kupitia upya kiasi kinachotolewa kama kifuta jasho kwa waathirika wa wanyamapori kwani hakiendani na thamani ya mwananchi anayelinda rasilimali hizo."alisema Leisangai

Naye afisa wanyamapori wilaya ya Monduli, Seraphino Mawanja aliyehudhuria mazishi hayo alisema katika kipindi cha miaka miwili maeneo hayo yamekuwa na changamoto kubwa ya ongezeko la Tembo ambao walihama kutoka hifadhi ya Tarangire baada ya mvua nyingi kunyesha na maeneo yao kujaa maji.

Alisema serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa kuwaondoa Tembo hao wanaovamia maeneo ya makazi kwa kuweka askari wa doria.

Hata hivyo alisisitiza kuwa serikali inajitahidi kufidia wananchi wanaoathiriwa na Tembo kwa kutoa kifuta jasho cha shilingi Milioni moja kwa aliyeuawa na Tembo na sh. laki tano kwa majeruhi.









By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post