Koku David, Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imevunja rekodi yake katika makusanyo baada ya kufanikiwa kukusanya kiasi cha Sh trilioni 2.088 ambacho ni sawa na ufanisi wa asilimia 101.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Edwin Mhede amesema kuwa makusanyo hayo ni ya mwezi Desemba mwaka 2020 ukilinganisha na lengo la kukusanya Sh. trilioni 2.072.
Amesema mbali na makusanyo hayo, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba mwaka wa fedha wa 2020/21 walifanikiwa kukusanya Sh. trilioni 9.983.
“Makusanyo ya mwezi Desemba hayajawahi kufikiwa katika historia ya Mamlaka ya Mapato na kwamba yamevunja rekodi ambayo Mamlaka ilijiwekea.
“Makusanyo ya kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba ni ufanisi wa wastani Sh trilioni 1.664 kwa mwezi ikilinganishwa na wastani wa makusanyo ya trilioni 1.500 kwa kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 na kwamba hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 11.00,” amesema Dk. Mhede.
Dk Mhede amesema, mafanikio hayo katika makusanyo ni dhahiri kwamba walipakodi na wananchi kwa ujumla wameonyesha uzalendo wa kuendelea kulipa Kodi kwa hiyari na kwa wakati licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali.
Amesema kuwa, TRA inawashukuru walipakodi wote waliotimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya serikali na kuiwezesha kufikia lengo katika makusanyo, pia inaishukuru serikali, taasisi za fedha pamoja na wadau mbalimbali kwa kuiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Aidha, amesema mwezi huu wa Januari TRA itaanza kufanya kampeni kabambe nchini ya kutoa elimu ya mashine za (EFD) hasa wakizingatia kuwa elimu kuhusu matumizi ya mashine hizo imeshatolewa nchi nzima.
Amesema msingi wa makadirio ya kodi kwa haki ni utunzaji sahihi wa kumbukumbu za mauzo hivyo wafanyabiashara wanahimizwa kufuata sheria kwa kutoa risiti kwa kila mauzo na wananchi wanatakiwa kudai risiti baada ya kuhudumiwa.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, James Dotto amesema kuwa wanaipongeza TRA kwa kuvunja rekodi waliojiwekea na kwamba wakati serikali ya awamu ya tano wakati inaingia madarakani ilikuta makusanyo ya Sh. bilioni 850 lakini kutokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa ikiwemo kuzuia mianya ya upotevu wa mapato ikafanikiwa kuongeza kiwango cha makusanyo hadi kufikia Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi na baadae kiwango kilipanda hadi kufikia Sh. trilioni 1.5.
Amesema kuwa, pia wanawapongeza walipakodi kwa kuonyesha ushirikiano mzuri uliowezesha kukusanya makusanyo makumbwa ambapo hivi sasa kwa mwezi kiwango cha kukusanya kimepanda hadi kufikia Sh. trilioni 1.664.
“Kukusanya kodi si utashi ila ni kwa mujibu wa katiba na kwamba TRA ina jukumu la kukusanya kodi lakini pia kuishauri serikali sera na sheria za kodi,” amesema Dotto.
Kuhusu mashine za EFD, amesema ni lazima kutoa na kudai risiti zinazotokana na mashine za EFD pindi biashara inapofanyika na kwamba kwa kutokufanya hivyo ni kinyume na sheria na kwamba watafanya linalowezekana ili kuhakikisha aibu ya kupoteza kodi inaisha.
Kwa upande wake Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Msafiri Mbibo amesema kuwa TRA itaendelea kutekeleza matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira nazuri kwa walipakodi.
Amesema pia wataendeleza mahusiano mazuri na walipakodi ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa watumishi wa mamlaka ya mapato ili waweze kufanyakazi kwa ufanisi na ufasaha.
from Author
Post a Comment