Baadhi ya Mameneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wakiwa katika Mkutano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo.
Na Avila Kakingo, Globu ya jamii
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kipindi cha Desemba 2020 imekusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 2.088 ikiwa ni sawa na asilimia 101.00 ukilinganisha na lengo lililokusudiwa la kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 2.072 kwa mwezi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Daktari Edwin Mhede amesema kuwa makusanyo hayo hayajawahi kufanikiwa katika historia ya Mamlaka hiyo.
Amesema mbali na Desemba 2020 makusanyo ya kila mwezi kuanzia Julai 2020 hadi Novemba, 2020 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 wamekusanya jumla ya Trilioni 9.983 ikiwa kwa Julai walikusanya shilingi trilioni 1.284, Agosti walikusanya Shilingi Trilioni 1.399, Septemba walikusanya shilingi trilioni 1.703, Oktoba walikusanya shilingi trilioni 1.379 na Novemba walikusanya shilingi Trilioni 1.338.
Dkt.Mhede amesema kuwa makusanyo hayo ni ufanisi wa wastani wa Trilioni 1.664 kwa mwezi ukilinganishwa na wastani wa makusanyo ya Trilioni 1.500 kwa kipindi hiki kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.00.
"Kwa makusanyo haya ni dhahili kwamba walipakodi na wananchi kwa ujumla wameonesha uzalendo wa hali ya juu wa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali na nachukuwa nafasi hii kuwashukuru walipakodi wote waliotimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya serikali na kuiwezesha Mmlaka kufikia makusanyo haya." Amesema Dkt.Mhede
Hata hivyo Dkt.Mhede amesema kuwa kwa mwezi Januari ya mwaka huu 2021 Kampeni Kabambe ya Ukaguzi matumizi ya risiti za Mashine za EFD nchi zima utaanza ikizingatiwa kuwa elimu imeshatolewa sambamba na kuwatembelea wafanyabiashara mlango kwa mlango.
Hivyo wafanyabiashara wameaswa kuwa kuzingatia sheria kwa kutoa risiti kwa kila maizo wanayofanya na wananchi wanakumbushwa kudai risiti kila wanunuapo bidhaa au kupata huduma kwa wenye mashine za EFD.
Wananchi wanaaswa kuwa wazalendo kwa kuwajibika kidai risiti, kutoa taarifa ya upotevu wa mapato na kutoa mrejesho wa kuwezesha kutekeleza majukumu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ufanisi zaidi, pia wananchi wamekumbushwa kudai risiti zenye taarifa sahihi kwani sio suala la hiari ni Takwa la Kisheria.
By Mpekuzi
Post a Comment