TUTAWAONDOA VIONGOZI WASIO WAZALENDO - DKT. GWAJIMA |Shamteeblog.














Na Catherine Sungura, WAMJW - Mbogwe


SEKTA ya afya imejipanga kuwaondoa viongozi wote wasio na sifa ya uongozi,umahiri,weledi,utashi,ujasiri na uthubutu wa kufanya kazi kwa ubunifu ili kuchochea maendeleo kwa kasi zaidi. 

Hayo yamesemwa jana tarehe 26/1/2020  na Waziri wa  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mbele ya Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa ufunguzi wa majengo ya kituo cha afya Masumbwe kilichopo kwenye halmashauri ya wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita.

“Sekta ya afya tumejipanga hivyo viongozi wasio na sifa na wanaofanya mambo kwa mazoea na kuwakatisha tamaa watumishi wasio viongozi na ambao wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana na kushindwa kuyapatia ufumbuzi mambo madogo madogo ambayo yapo ndani uwezo wa taasisi,wanaorekebishika tutawarekibisha ili tupate viongozi wanaoweza kusimamia uongozi kwa uzalendo kwa nguvu zao zote na kwa kujitoa.” Alisisitiza Dkt. Gwajima.

Alisema lengo ni kuhakikisha usimamizi  wenye tija wa rasiliamali ambao umefanyiwa uwekezaji na Mhe. Rais kwa moyo thabiti.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema  mambo mengi yamefanywa  katika sekta ya afya kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya uchaguzi mkuu wa CCM wa mwaka 2020-2025“ hakika umetuachia jukumu kubwa la kusimamia na kuhakikisha uwekezaji huu unaendelea kuwanufaisha wananchi maskini na wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu”.
 
Kwa upande wa  huduma bora zinatolewa kuanzia ngazi za zahanati hadi hospitali za rufaa za ngazi ya Taifa amesema Wizara  itahakikisha dhana ya huduma kwa mteja(customer care) inatekelezwa ili wananchi wafurahie huduma na kuhamasika  kujiunga na mifuko ya  bima ya afya katika kuelekea bima ya afya kwa wote kwani bima ya afya kwa wote itawezesha kuimarisha na kuboresha zaidi huduma na kuwa za gharama nafuu na karibu zaidi na wananchi.

Hata hivyo katika kutekeleza mkakati wa kupunguza gharama za uendeshaji Dkt. Gwajima alisema Wizara itajielekeza kwenye viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba zikiwemo bidhaa za tiba asili na kuahidi kusimamia kwa nguvu zote kwani nchi imejaliwa  miti mingi na ujuzi mwingi ili eneo hili liweze kunufaisha na kuimarisha afya za watanzania kupitia tiba asili.

Vile vile Dkt. Gwajima alisema eneo la Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,wizara yake itahakikisha sekta hii inaimarishwa katika mifumo yake ili kuwa na jamii iliyoendelea katika nyanja zote na kuwa daraja imara katika maendeleo ya afya.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amewataka Viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kusema  bila kificho matunda mazuri  yaliyofanywa na Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kituo cha afya Masumbwe kwani wananchi walikua wakihangaika kupata huduma za afya.

Waziri Jafo alisema wapo watu waliodharilika kwa kukosa huduma za afya,hivyo viongozi waliopewa dhamana wanapaswa kusemea hayo ili watanzania waliotahabika kwa kipindi kirefu sasa wamepata mkombozi.

“leo hii tumefikia hospitali 99 ikiwemo hospitali ya Uhuru ambayo pesa ulizitoa mwenyewe,ila zipo halmashauri tatu ambazo zimejiongeza na zimeaanza kujenga hospitali za wilaya kwa mapato yao ya ndani zikiwemo halmashauri ya jiji la Arusha, Mwanza na Kinondoni na hivyo kufanya hospitali za wilaya kufikia 102.

Aidha,Waziri Jafo alisema wilaya ya Mbogwe imeanza kujenga hospitali ya wilaya na tayari shilingi milioni 500 za awamu ya pili zimeshatolewa na hivyo kwa mkoa wa Geita hospitali nne  za wilaya ikiwemo ya wilaya hii zinatarajiwa kujengwa.

Kituo cha afya Masumbwe kilitengewa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga majengo manne  ikiwa ni mpango wa kuimarisha vituo vya afya 487,halmashauri imetumia shilingi milioni 249 ikiwemo kujenga  maabara,wodi ya wanaume na wanawake ,nyumba moja ya Daktari pamoja na jengo la kuhifadhia maiti pamoja na kukarabati majengo ya kituo hicho cha afya ambacho hivi sasa kinafanya kazi kama hospitali ya wilaya.






By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post