UJENZI WA BARA BARA KUTOKA MBINGA MPAKA MBAMBABAY UMEKAMILIKA KWA ASILIMIA 99 |Shamteeblog.

 Na Muhidin Amri,Mbinga

KAMPUNI ya Chico inayojenga barabara kwa kiwango cha lami kilomita 66 kutoka Mbinga hadi Mbambabay wilaya ya Nyasa imesema kazi ya ujenzi wa barabara hiyo umekamilika  kwa wakati kama ilivyoahidi kwa Rais Dkt John Magufuri wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo mwezi April 2019.

Meneja msaidizi wa mradi huo Sam Han alisema, barabara hiyo  kwa sasa imekamilika kwa asilimia 100 ambapo  kazi kubwa ilikuwa kukata milima,kuondoa kifusi kisicho hitajika barabarani  pamoja na kujenga makalavati kazi ambayo imeshafanyika kwa ufanisi mkubwa.

“ Kazi kubwa  katika ujenzi wa barabara  ilikuwa kukata milima,kutoa udongo wa juu usiohitajika na kujaza kifusi kipya na kujenga makalavati,hivyo matumaini yetu  kwamba ifikapo Disemba mwaka huu mradi  utakamilika kama tulivyohaidi kwa Mheshimiwa Rais Dkt John Magufuri”alisema Sam.

Hata hivyo Sam alisema, changamoto kubwa waliyokutana nayo katika ujenzi wa mradi huo ni kuwepo kwa milima mikubwa,kona nyingi na mawe mengi hasa eneo la Chunya,  lakini kutokana na uwezo na umahiri mkubwa wa Chico katika ujenzi wa miundombinu hasa ya barabara kazi inaendelea  na itakamilika kwa muda muafaka.

Sam alisema, ni matumaini ya Chico kuwa,  baada ya kukamilika barabara hiyo  itachochea kukua kwa uchumi na kuharakisha maendeleo ya wakazi wa Nyasa na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla  na ameiomba Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya ujenzi kushirikiana na Chico katika ujenzi wa barabara  na miradi mingine hapa nchini.

Alisema,  baada ya kukamilika  wananchi wameanza kunufaika  kwa kubadilisha maisha yao  ikiwemo  kupunguza gharama ya usafiri na kusafirisha mazao,bidhaa mbalimbali  na  samaki  wanaopatikana  kwa wingi katika ziwa nyasa kwenda katika masoko mbalimbali ya ndani na nje  ya  mkoa wa Ruvuma.

Kwa mujibu wa Sam, kujengwa kwa barabara hiyo kumehamasisha watu wengi kutoka ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma kwenda kuwekeza wilayani  humo  katika miradi mbalimbali ikiwemo nyumba za kulala wageni,biashara ya usafirishaji,kilimo na uvuvi hivyo kuchangia sana kukua kwa uchumi wa wananchi wa kawaida na wilaya ya Nyasa.

Alisema, Chico imefanya kazi usiku na mchana, ili  kuhakikisha barabara hiyo  inakamilika kwa muda uliopangwa na imejengwa kwa  ubora mkubwa  na kuwa mfano kwa barabara nyingine hapa nchini.


“sisi kama kampuni ya Chico tunaamini  barabara hii ni mfano, kwani tumitumia uzoefu wetu na weledi wa hali ya juu katika ujenzi wake,tunataka watanzania watukumbuke  na watumie barabara hii kujiletea  maendeleo na kukuza uchumi wao”alisema Sam.

Baadhi ya wananchi wameishukuru Serikali ya awamu ya tano kupitia wizara ya ujenzi  kwa jitihada zake za kuwaondolea kero ya usafiri iliyowasumbua kwa muda mrefu.

Wameipongeza kampuni ya Chico kutokana na uwezo mkubwa kwa kujenga barabara hiyo  na  matumaini yao, mara itakapo kamilika itakuwa mkombozi na kuharakisha maendeleo ya Nyasa na wilaya mama ya Mbinga.

Boniface Ndunguru mkazi wa kijiji cha Nyoni wilayani Mbinga alisema, kampuni ya Chico imeonesha weledi  wa hali ya juu katika utekelezaji wa mradi huo na kuiomba Serikali kuendelea kuitumia kampuni hiyo katika miradi mbalimbali ya ujenzi.

Nyoni alisema, kujengwa kwa barabara hiyo ni faraja kubwa kwa wananchi wa wilaya hizo mbili na mkoa wa Ruvuma kwa jumla, kwani imeanza kufungua mawasiliano ya barabara kati ya wilaya ya Nyasa na maeneo mengine.

Mkazi mwingine Alex Massimba amesema,  kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara kuna faida kubwa kwa wananchi wa kipato cha chini kwa sababu  gharama za usafi zimeanza kupungua na kufika kwa wakati katika shughuli zao za kila siku.

Alisema, kabla ya kujengwa kwa barabara hiyo wananchi waliteseka sana  na wapo waliopoteza maisha kwa kushindwa kufikia katika vituo vya kutolea huduma kwa muda sahihi kutokana na miundombinu duni ya barabara.

“kwa kweli tunaipongeza sana kampuni ya Chico kujenga barabara hii kwa ubora na weledi wa hali ya juu ikilinganishwa na baadhi ya barabara za lami zinazojengwa katika mikoa mingine hapa nchini,tunamuomba Rais Dkt John Magufuri na Serikali yake iwape upendeleo mkubwa ndugu zetu wa CHICO kwenye miradi mbaimbali,hii kampuni imeonesha uwezo mkubwa”alisema.

Alisema,  ni faraja  kwa wananchi wa Nyasa kuona  wanaondoka katika mateso makubwa yaliyotokana na ukosefu wa miundombinu ya uhakika kwa kuwa wapo baadhi ya wananchi wakiwemo wanawake wajawazito waliopoteza maisha kwa  kuchelewa kufika zahanati,vituo vya afya na Hospitali kutokana na tatizo la miundombinu duni ya barabara, hivyo kukamilika kwa barabara hiyo kutaokoa maisha ya watanzania wengi hasa wale wenye kipato cha chini.

,Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya akipiga magoti  katikati ya barabara ya lami inayojengwa na kampuni ya Chico, kama ishara ya kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kujenga barabara  hiyo kutoka Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa km 66 ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99.
Mwanasheria wa kampuni ya Chico inayojenga barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Mbambabay wilaya y,a Nyasa mkoani Ruvuma Gaudence Ndomba kulia, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya  changamoto walizokutana wakati wa ujenzi wa barabara hiyo ambayo inatajwa itachochea kukua kwa uchumi wa wananchi wa wilaya hizo mbili,wa kwanza kushoto meneja msaidizi wa mradi wa ujenzi kutoka kampuni ya Chico Sam Han,wa pili kushoto mkuu wa wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba.
 Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Isabela Chilumba wa pili kushoto akimsikiliza meneja msaidizi wa mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami Mbambabay hadi Mbinga yenye urefu wa km 66  ya Chico Sam Han,baada ya mkuu wa wilaya kutembelea ujenzi wa barabara hiyo eneo la Mbambabay wilayani humo,kulia mwanasheria wa Chico Gaudence Ndomba. Picha zote na Muhidin Amri.

By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post