Waziri Kalemani Aigiza Tanesco Kuwaombea Ajira Watumishi Walioajiriwa Kwa Mikataba Ya Muda Mfupi Kwa Kipindi Kirefu. |Shamteeblog.
Na Dorina G. Makaya – Shinyanga.
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la TANESCO nchi nzima, kuwaombea ajira watumishi walioajiriwa kwa vipindi vifupi na kuitumikia TANESCO kwa muda mrefu.
Waziri Kalemani ametoa agizo hilo tarehe 30 Mwezi Desemba, alipokuwa akizungumza na watumishi wa TANESCO wa Mkoa wa Shinyanga, katika kikao kazi cha kufahamiana, kusikiliza kero na kutoa maelekezo ya kazi ili kuliwezesha shirika la TANESCO nchini kufanya kazi kama timu moja kwa kasi kwa ubunifu na kwa usahihi ili kufikisha huduma ya umeme kote nchini na kuongeza mapato ya Serikali kutokana na Sekta ya Nishati.
Akizungumza baada ya kusikiliza Kero za Watumishi wa TANESCO mkoa wa shinyanga, Waziri Kalemani ameweka bayana kuwa, watumishi hao wanaoajiriwa kwa vipindi vifupi ndio wanaokutana na wateja moja kwa moja na kujenga taswira ya TANESCO (Visibility) kwa wateja wanaohitaji na kutumia huduma ya umeme hapa nchini.
Amesema, kufanya kazi kama kibarua kwa miaka mingi bila ya kuajiriwa kwa watumishi hao, kunapunguza na pengine kuondoa hari ya kufanya kazi watumishi hao, kuleta mianya ya rushwa na hata kutengeneza vishoka.
Dkt. Kalemani ameeleza kuwa, anaamini kuajiriwa kwa watumishi hao, kutawajengea kufanya kazi kwa uaminifu na kwa kujituma kwani watahitaji kutunza ajira zao na kuonya kuwa, mtumishi yeyote atakayebainika anaomba rushwa kutoka kwa wateja na kutumia lugha zisizofaa, huyo atondolewa mara moja na hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi yake.
Akielezea kuhusu umuhimu wa kikao kazi hicho, Waziri Kalemani amefafanua kuwa, ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa kazi, ipo haja ya kuonana na watumishi, kufahamiana, kujionea mazingira halisi ya kazi, kusikiliza kero zao na kuzitolea ufumbuzi na kisha kutoa mwelekeo na maelekezo ya kazi kufikia malengo yaliyowekwa kwenye Sekta ya NIshati.
“Unaweza kuwa unaagiza nataka kazi hii ifanyike leo na kukamilika leo hii hii, na kumbe unayempa maelekezo hayo ni mlemavu na hana uwezo wa kwenda kwa kasi hiyo. Ukaagiza afukuzwe kwa kushindwa kutekeleza kazi husika, lakini kumbe uliyemwagiza ni mlemavu. Hivyo ni muhimu kufahamiana. Amesema Dkt. Kalemani.”
Aidha, Waziri huyo wa Nishati ameiagiza TANESCO, kuwanunulia pikipiki watumishi walio katika vitengo vya upimaji kwa ajili ya kufikisha umeme kwa wateja ( surveyors ) ili kuwezesha utendaji kazi kwa haraka na kuwaelekeza watumishi hao kuzitumia pikipiki hizo kwa shughuli za kikazi. “msije mkazigeuza pikipiki hizo kuwa bodaboda! Tena mziandike SU. Nataka mfanye kazi kwa kasi, kwa ubunifu, na kwa usahihi, amesema Waziri Kalemani.
Nataka kila ofisi ya TANESCO ninayo kwenda nione kuna ongezeko la mapato, nione kuna ongezeko la wateja sugu kulipa madeni wanayodaiwa TANESCO.
Waziri Kalemani ameigiza TANESCO na REA kuhakisha vijiji vyote nchini viwe vimeunganishwa na umeme, ifikapo Septemba 2022.
Dkt. Kalemani pia ameiagiza TANESCO kutumia nguzo za zege kwenye maeneo korofi yenye maji (Swamp areas) ili kuepusha gharama za matengenezo zinazotokana na nguzo kuanguka mara kwa mara na wateja kukosa umeme wakati matengenezo yanapokuwa yanafanyika kurejesha umeme. Aidha, Waziri Kalemani ameielekeza TANESCO nchini, kutoza gharama za uunganishwaji wa umeme kwa wateja kwenye vijiji na vitongoji kwa gharama ya shilingi 27,000 tu kwa wateja wanaotumia njia moja ya umeme isipokuwa katika maeneo ya majiji.
By Mpekuzi
Post a Comment